Tuesday, April 4, 2017

USHAURI WA KUANZISHA KOZI YA UKALIMANI NI FURSA MPYA YA AJIRA KWA WATANZANIA.

Jovina Bujulu –MAELEZO

Ubora na thamani ya lugha ya Kiswahili duniani unadhihirika kwa kukubalika kwake,  hali hii inayopelekea lugha adhimu ya Kiswahili kuendelea kukua na kutumika katika nchi mbalimbali duniani kijamii, kiuchumi na hasa kibiashara na ushirikiano wa kimataifa.

Mchango wa lugha hii inaipa hadhi kubwa nchi yetu ambayo ni kitovu cha lugha hii inayotumika kama lugha rasmi ya mawasiliano katika nyanja mbalimbali na pia ndiyo lugha unganishi inayotumiwa na watu wengi nchini.

Kihistoria, lugha ya Kiswahili imekuwa na mchango mkubwa kutokana na kutumika katika harakati za ukombozi  na pia kuwaunganisha Watanzania na kuwafanya wawe wamoja.

Mara baada ya Uhuru Tanzania ilianzisha Baraza la Kiswahili (BAKITA) na kupewa jukumu la kuimarisha na kueneza lugha hii , pia kuhakikisha inatumika kwa ufasaha pamoja na kukuza msamiati wake ili iweze kukidhi matumizi yake.

Mwaka 1968, lugha hii ilianza kutumika  kufundishia katika shule za msingi hapa nchini. Hatua hii ilimaanisha kila mwanafunzi wa shule ya msingi kuifahamu vizuri kwa kuiandika, kuisoma na kuielewa.

Aidha, historia ya kuikuza na kuieneza lugha hii imeanzia mbali, mwaka 1962 hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliitumia kuhutubia Bunge la Tanganyika, baada ya utawala wake, Rais aliyemfuatia, Ali Hassan Mwinyi aliendeleza matumizi ya Kiswahili katika shughuli mbalimbali za mawasiliano.

Naye Rais wa Awamu ya Tatu, Mhe.Benjamin Mkapa na Rais wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete walifanikisha maendeleo ya lugha hii kwa kuhimiza matumizi fasaha katika nyanja za elimu, shughuli zote za Serikali, katika shughuli au mikusanyiko rasmi pamoja na matumizi mengine ya mawasiliano.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hakikuwa nyuma katika kuhakikisha kinakuza, kinaeneza na kinakifanya Kiswahili kitambulike zaidi duniani.Miongoni mwa jitihada hizi ni pamoja na kuanza kutumia Kiswahili kama lugha rasmi ya mawasiliano chuoni hapo ili kuipa msukumo kwa wananchi wa mataifa mengine yanayohitaji kujifunza lugha hii.

Katika kutambua juhudi hizi za Chuo, Balozi wa kwanza wa Kiswahili Barani Afrika, Mama Salma Kikwete, hivi karibuni alimkabidhi tuzo ya Kiswahili  Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Rwekaza Mkandara, ikiwa ni utambuzi wa mchango wake  kwa kurasimisha lugha hiyo  kutumika katika shughuli zote za Chuo na kitaaluma ikiwemo mikutano ya Baraza la chuo.

Aidha, Mama Salma alitoa wito kwa taasisi mbalimbali kuwekeza katika kuendeleza lugha Kiswahili ili kuieneza kibiashara ndani na nje ya Bara la Afrika.

Kutokana na umuhimu wake katika mawasiliano hivi karibuni Bunge la Shirikisho la Jumuiya ya Afrika Mashariki limeidhinisha lugha Kiswahili itumike katika mikutano yake ya Bunge.

Bunge hilo linajumuisha Wabunge kutoka katika nchi sita za jumuiya hiyo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudani Kusini zimepitisha lugha hiyo kutumika katika nchi zao. Hatua hiyo ni mwanzo mzuri wa kukipaisha Kiswahili kimataifa.

Ni kutokana na muktadha huo, baadhi ya wataalamu wa lugha wameishauri Serikali kuanzisha kozi ya ukalimani katika vyuo vyake ili kuongeza idadi ya wakalimani hapa nchini hatua ambayo itawaongezea ajira wahitimu wa kozi hiyo.

Hadi sasa inakadiriwa kuwa idadi ya wakalimani nchini haizidi 20 mbao ndio wanaotoa huduma katika mikutano mbalimbali ya kimataifa.

Akizungumza jijini Dar es Saaam hivi karibuni Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili (BAKITA), Dkt. Selemani Sewangi alisema kuwa huu ni wakati muafaka kwa Tanzania kuanzisha kozi hiyo ili kupata wakalimani wa kutosha na wenye weledi, uwezo na maarifa katika kukalimani lugha ya Kiswahili kwenda lugha nyingine mbalimbali duniani.

Aliendelea kusema kuwa Tanzania haina kozi hiyo nyuoni, hivyo uwepo wa wataalamu hao hasa kipindi hiki ambacho nchi inapokuwa kiuchumi kwa kasi, kazi hiyo itoe mchngo wake ikizingatiwa sekta ya utalii inaendelea kuimarika na kuwa na ongezeko la wageni mbalimbali wakiwemo watalii, wawekezaji na wengine hatua ambayo itakuwa fursa ya kutangaza utajiri na maliasili zilizoko nchini mwetu.

 “Kuwa kuna baadhi ya watu ambao wanatafsiri lugha ya Kiswahili wakidhani wanafanya taaluma ya ukalimani, jambo ambalo si sahihi kitaaluma, watu hawa hawawezi kupata ajira kutokana na kukosa vigezo vya elimu rasmi ya ukalimani” alisema Dkt. Sewangi.

Akifafanua juu ya maana hasa ya ukalimani Dkt. Sewangi alisema kuna mkanganyiko  kati ya kutafsiri na kukalimani, ambapo alisema kuwa kutafsiri kunaweza kufanywa na mtu yoyote, lakini kukalimani ni lazima mtu asomee kozi maalumu  ili aweze kutambulika kimataifa.

Katika kuonyesha msisistizo wa kuhakikisha kuwa Kiswahili kinapaa kimataifa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa Kiswahili ni lugha ya Waafrika na inazungumzwa katika nchi nyingi na imekubalika kutumika katika mikutano ya Umoja wa Afrika, hivyo aliwashauri Watanzania kuipenda lugha hiyo.

Hivi karibuni Tanzania ilitembelewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mhe. Haile Mariam Dessalegn ambapo alisema kuwa nchi yake imekubali kuchagua Chuo Kikuu kimoja ili lugha ya Kiswahili ifundishwe nchini mwake kwa kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, Rais Dkt. Magufuli aliahidi kupeleka wataalamu wa lugha ya Kiswahili ili wafundishe katika chuo kitakachoteuliwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia kufundisha lugha hiyo.

Kwa kuzingatia umuhimu wa lugha ya Kiswahili huu ni wakati muafaka kwa watunga Sera, Mamlaka husika na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia kuanzisha kozi ya ukalimani katika vyuo vyetu ili wahitimu wapate fursa za ajira katika nchi mbalimbali  na hivyo kuzidi kuipa hadhi  na kuieneza lugha ya Kiswahili ambayo inakisiwa kuwa ni lugha ya 10 miongoni mwa lugha 600 zinazozungumzwa duniani.

No comments: