Tuesday, April 4, 2017

SABABU ZA ANGUKO LA JUMUIYA ZA WATANZANIA UGHAIBUNI

Jumuiya ya waTanzania Rome- Italia 
Picha kwa hisani ya Tanzania Community Rome- Italy

Na Vijimambo Blog
Natumaini wote hamjambo na mnaendelea vizuri na majukumu ya kila siku ya maisha yanayotukabili kila siku ya uhai wetu. Baada ya salamu ningependa kuanza moja kwa moja na swala ya jumuiya za waTanzania nje ya nchi tuipendayo Tanzania, kumekuwepo na migogoro mingi kwenye hizi jumuiya na mishikamano inayoleta umoja kupungua siku hadi siku mpaka inasikitisha na kutia huruma.

Jumuiya za waTanzania ughaibuni zilikua imara sana wakati zilipoanzishwa miaka ya nyuma hasa mwanzoni mwa miaka ya 80 na jumuiya zilikua imara sana wakati huo ikiwemo wanajumuiya wanachama kuwa hai kwa kuchangia michango yao ya kila mwezi hadi mwaka.
Sababu moja wapo kubwa ya jumuiya hizi kuwa hai ni idadi ndogo ya waTanzania iliyokuwepo ughaibuni iliyofanya urahisi wa mawasialino kwa kujuana na kutembelea kama ndugu waliotoka nchi moja tofauti na sasa waTanzania wamekua wengi mpaka wengine imekua vigumu kujuana.
Jumuiya hizi zilianza kugawanyika na kuwa makundi makundi pale viongozi waliochaguliwa kupitisha muda wao na kung'ang'ania kuendelea kuwepo madarakani bila ridhaa ya wanaowaongoza.
Sababu nyingine kubwa na ambayo ndio sababu kuu ni viongozi hawa kutafuna fedha za michango ya jumuiya zao na kutokua wazi na makusanyo ya fedha kutoka kwenye michango mbalimbali ya jumuiya zikiwemo sherehe zilizofanyika kwenye jumuiya hizo zilizohusisha makusanyo ya fedha milangoni au kwa kuuza biadhaa mbalimbali ambazo zimetokana na wanajumuiya wenyewe kuzileta hapo mahali husika, sababu hizi zilikatisha tamaa ya waTanzania ughaibuni kutokuana faida ya kujiunga na jumuiya zao na kuamua kutochangia kwa kuhofia kwa fedha kuliwa kitu kilichosbabisha jumuiya nyingi zishindwe kujiendesha kwa kukosa fadha.

Sababu nyingine ni viongozi wa jumuiya hizi kushindwa kutofautisha faida ya mwanachama hai na asiyekuwa mwanchama hai mfano inapotokea shughuli mwanachama hai atalipa kiingilio sawa na asiyekuwa mwanchama hai, sababu hii inamfanya mTanzania ughaibuni asione umuhimu wa kujiunga na jumuiya.
Sababu nyinginge ambayo ndio inayoonekana kwa wengi ni kuingiliwa na vyama vya siasa kwenye jumuiya za waTanzania ughaibuni. Tangia kufunguliwa kwa matawi ya vyama vya siasa ndani ya jumuiya za waTanzania ughaibuni limeongeza tatizo kubwa  la utengano kwenye jumuiya hizo na kuleta matabaka ya itikadi na inapofanyika uchaguzi unageuzwa kuwa wa kisiasa badala kuwa wa kijumuiya, hii imekua sumu kali katika jumuiya za waTanzania ughaibuni. Pamoja na matatizo yaliyokuwepo awali hili la vyama vya siasa wakiwemo viongozi wakubwa wa vyama hivyo kuja ughaibuni kunadi sera na kufungua matawi ya vyama vyao kitu ambacho kimeondoa mshikamano na umoja wa waTanzania ughaibuni ikiwemo wale wasiopenda mambo ya siasa kuondokwa na msisimuko wa kujiunga na jumuiya zao.
Kitu ambacho viongozi wengi wa vyama hizi vya siasa wanachotakiwa kutambua ni kwamba unapokua raia wa nchini ya ughaibuni huruhusiwi kujihusisha na siasa ya vyama nje ya nchi na kufanya hivyo ni kuvunja sheria ya nchi za ugahaibuni.
Tatizo lingine linaloleta mgawanyiko katika jumuiya zetu ughaibuni ni waTanzania wanakuwa hawapo tayari kuongozwa na waliowachagua wakidhani kuwa viongozi waliowachagua watafanya kazi bila wao huku wakisahau kwamba "JUMUIYA NI WATU SIO VIONGOZI" Viongozi huitwa vingozi kunapokua na watu wa kuwaongoza bila watu hawawezi kuitwa viongozi. Huu mtindo wa kuwachagua viongozi na kuwaacha peke yao ni sababu moja wapo ya anguko za jumuiya za waTanzania ughaibuni na lisiporekebishika hili Jumuiya zote zitakufa.
Sabu nyinini ni viongozi waliokuwepo madarakani kugoma kutoa ushirikiano kwa viongozi wapya ikiwemo kuwashawishi mpaka wafuasi wao wasitoe ushirikiano kwa viongozi wapya waliochaguliwa, hii inaleta mgawanyiko kwenye jumuiya za waTanzania ughaibuni huu mganwanyiko ni mbaya zaidi na wenye ushawishi mkubwa wa kuuwa jumuiya kwani uongozi ni dhamana kwa watu unaowaongoza na waliokuamimini kukuweka madarakani na muda unapokwisha kubali kuondoka na toa ushirikiano kwa viongozi waliochagulia kuokoa jumuiya yako.

Kitu gani kifanyike kunusuru jumuiya za ughaibuni.
1. Kuondokana na vyama vya siasa.

2. Kuwa wazi kwenye mswala ya fedha.

3. Kukubali kuongozwa na viongozi mliowachagua.

4. Viongozi waliopita na wafuasi wao kuwakubali viongozi wapya waliochaguliwa na kuwapa ushirikiano..

5. kumbuka uongozi wa jumuiya hizi ni wakujitolea leo tupo ya kesho ayajuaye ni mwenyezi Mungu Upendo ni silaha kubwa kwenye Jumuiya zetu kuliko unavyofikiri unapoweka upendo mbele hivyo vitu vinne hapo juu havitakuwepo, siku zote umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu, matabaka yawe mwisho tuokoe jumuiya zetu ughaibuni.

Mungu ibariki Tanzania, 
Mungu zibariki jumuiya za waTanzania ughaibuni.

1 comment:

Mbele said...

Shukrani kwa kuanzisha mada hii. Kuhusu hiki kipengele cha matawi ya vyama vya siasa, wakati ule baada ya wana-CCM kuanzisha matawi huku ughaibuni, niliandika makala, Januari 2009, kuhoji jambo hili, katika blogu yangu.