Wednesday, April 19, 2017

Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete Ahitimisha Ziara ya Kamisheni ya Elimu kwa Kutembelea Nchi 15 Afrika

Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kugharamia Fursa za Elimu Duniani Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekamilisha ziara yake ya kuhamasisha utekekezaji wa Ripoti ya Kamisheni hiyo ijulikanayo kama 'Kizazi Cha Elimu' (The Learning Generation).

Katika ziara hiyo iliyomfikisha katika nchi 15, Rais Mstaafu Kikwete amekutana na Wakuu wa Nchi 12 wa nchi za Uganda, Malawi, Msumbiji, Congo, Tunisia, Ghana, Chad, Gabon, Ivory Coast, Namibia, Afrika Kusini na Botswana. Aidha amekutana na Makamu wa Rais wa Nigeria na Mawaziri Wakuu wa Ethiopia na Tanzania. Pamoja na viongozi wa nchi na Serikali, Rais Mstaafu amekutana na viongozi wa Taasisi za Kikanda 3  ambao ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Madhumuni ya ziara hizo yalikuwa ni kufikisha ujumbe wa Kamisheni na Ripoti yake juu ya umuhimu wa nchi za uchumi wa kati na chini (low and middle income countries) kufanya mapinduzi makubwa ya elimu ili kukabiliana na janga kubwa la elimu linaloinyemelea dunia. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamisheni hiyo, ubora wa elimu inayotolewa na nchi zinazoendelea za uchumi wa kati na chini ni ile ambayo imetolewa na nchi zilizoendelea miaka 70 iliyopita. Aidha, nchi zinazoendelea ziko nyuma sana katika vigezo vitatu muhimu vya elimu vya fursa  ya kujiunga na elimu (access to education), kumaliza elimu (completion) na ufaulu na kuelimika (learning outcomes). 

Vile vile, Ripoti ya Kamisheni inaonyesha kuwa Barani Afrika ni asilimia 5 tu ndio wenye elimu ya Chuo Kikuu na asilimia 20 ndio wenye Elimu ya Sekondari jambo ambalo linafanya bara la Afrika kuwa 'Bara la Wahitimu wa Elimu ya Msingi'. Hali hii ni ya kukatisha tamaa wakati ambapo nchi za Asia za Japan, Korea Kusini na Thailand zikitazamia kufikia lengo la asilimia 80 ya wanafunzi wake kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu ifikapo mwaka 2050. Barani Afrika, inatarajiwa kufikia asilimia 15 tu ya wanafunzi wake, ambapo asilimia 10 kati ya hiyo ni Afrika ya Kaskazini na Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kubakia na asilimia 5 tu.

Kamisheni inatahadharisha kwamba endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa, inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2030, watoto milioni 160 barani Afrika watakuwa nje ya mfumo wa Elimu wakati ambapo, Dunia imeazimia kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuwa ifikapo mwaka 2030 pasiwepo na mtoto aliyeachwa nyuma. Aidha, stadi zinaonyesha kuwa mapinduzi ya teknolojia yatafuta ajira zipatazo bilioni 2 duniani ambapo asilimia 70 ya ajira hizo ziko barani Afrika. Bila kuwekeza katika Elimu, Bara la Afrika halitakuwa na nafasi huko tuendako.

Kamisheni inapendekeza nchi zinazoendelea kufanya mageuzi katika mifumo yao ya elimu kwa kufanya yafuatayo:

1. Kuongeza Ufanisi kwa kuhimiza usimamizi mzuri na kuziba mianya ya rushwa na upotevu katika mfumo wa elimu;

2. Kupanua fursa za elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bila kujali jamii anayotoka, jinsia au ubaguzi wa aina yoyote;

3. Matumizi ya Teknolojia na mbinu bora za kitafiti za utoaji wa elimu ikiwemo kuainisha mitaala iendane na mabadiliko ya dunia; na

4. Kuongeza uwekezaji wa fedha katika elimu ili kuwezesha utoaji wa elimu bora yenye kukidhi viwango na mahitaji ya sasa na baadae.

Katika ziara yake katika nchi 14 zilizochaguliwa kuongoza mapinduzi ya elimu (Pioneer Countries) za Botswana,Chad,Congo,Ethiopia,Gabon, Ghana,Ivory Coast, Malawi, Msumbiji, Nigeria,Namibia, Tanzania,Tunisia na Uganda, Rais Mstaafu Kikwete ameridhishwa na jitihada na utashi wa hali ya juu unaoonyeshwa na viongozi na serikali zao katika kupanua fursa za elimu na kuinua hali ya elimu ya watoto wao. Changamoto kubwa iliyoainishwa ni uwezo mdogo wa serikali hizo kugharamia kikamilifu fursa za elimu. Tayari nchi hizo zinatumia wastani wa asilimia 18 hadi 20 wa bajeti zao katika elimu, na bajeti ya elimu ni kubwa katika nchi zote alizotembelea. Imejidhihisha kuwa ni vigumu kwa nchi hizi kuvuka ukomo wa bajeti huo bila kupata chanzo kingine cha fedha nje ya bajeti zao.

Kwa ajili hiyo, Kamisheni inaendelea na jitihada zake za kushawishi Jumuiya ya Kimataifa kuongeza misaada na fedha za mikopo kugharamia elimu katika nchi zinazoendelea. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamisheni, fedha za wahisani katika elimu zimekuwa zikipungua kutoka asilimia 13 mwaka 2003 hadi asilimia 10 mwaka 2013. Aidha, stadi imeonyesha kuwa fedha za elimu zimekuwa zikipungua wakati ambapo fedha kwa ajili ya miundombinu na afya zimekuwa zikiongezeka.

Kamisheni ya Elimu inaendelea na jitihada za kushawishi nchi wahisani, mashirika ya fedha ya kimataifa na washirika wa maendeleo kuongeza fedha na uwekezaji katika elimu kwa manufaa ya dunia na kizazi kijacho. Lengo ni kushawishi ongezeko la misaada katika elimu (ODA) kufikia asilimia 15  na fedha za mikopo kufikia walau asilimia 0.5 ya GDP zao ambayo ni sawa na dola za kimarekani bilioni 50 ifikapo mwaka 2030.

Kwa ajili hiyo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete amejumuika na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Uingereza Mstaafu Gordon Brown kukutana na Mawaziri wa Fedha wa nchi 14 na Wakuu wa Mashirika ya Fedha pembezoni mwa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia unaondelea jijini Washington D.C. kushawishi kutekelezwa kwa azma hiyo.

No comments: