Tuesday, April 4, 2017

MAMA SAMIA AWATAKA WAFARANSA KUENDELEA KUWEKEZA TANZANIA.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa Tanzania ni Moja ya nchi salama kwa ajili ya uwekezaji barani Afrika kwa sababu haina matatizo ya migogoro ambayo yanaweza kuhatarisha usalama wa mali ya wawekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo wakati akifungua maonyesho ya Kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.

Makamu Rais Mhe Samia Suluhu Hassan pia amewakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini Ufaransa kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hasa katika kilimo, nishati, utalii,usafiri kutokana na hali ya amani na utulivu iliyopo nchini.

Makamu wa Rais amesema maonyesho hayo ya kibiashara ambayo yataambatana na kongamano kubwa la Kibiashara kati ya nchi hizo Mbili ni fursa ya kipekee kwa wafanyabishara wa Tanzania na Ufaransa kukutana na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali ya kibiashara na uwekezaji.

Ameeleza kuwa katika kuelekea katika uchumi wa viwanda Tanzania haiwezi kufanya kazi hiyo peke yake bali kwa kushirikiana na mataifa makubwa ambayo yamekuwa na teknolojia ya kisasa katika uwekezaji ikiwemo taifa la Ufaransa.

Makamu wa Rais amewahakikishia wawekezaji wote wanaokuja kuwekeza nchini kuwa serikali itafanya kila linalowekezekana kuendelea kujenga mazingira bora kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira bora ya uwekezaji barani Afrika serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuimarisha miundombinu mbalimbali ikiwemo bandari, reli, barabara, usafiri wa anga ili kurahisisha kazi ya usafiri na usafirishaji nchini.

Kwa upande wake, Balozi Ufaransa hapa nchini Malika BERAK amesema kuwa ufunguzi wa Kongamano hilo kubwa la Kibiashara kati ya Tanzania na Ufaransa linalolenga kujenga na Kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi hizo Mbili.

Balozi huyo amesema kuwa kongamano hilo litajikita katika kujadili kwa kina fursa za uwekezaji hapa nchini hasa kwenye maeneo ya nishati, usafirishaji, teknolojia ya habari na Mawasiliano na miradi ya maendeleo.
Kongamano hilo la siku Nne la Kibiashara kati ya Ufaransa na Tanzania litawakutanisha wafanyabiashara wa Kitanzania na wenzao wa Ufaransa katika kujadili na kubadilisha uzoefu katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kibiashara kama hatua ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Ikulu- Dar es Salaam.
4-April-2017


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Jukwa la Wafanyabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania jana Jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo ya siku nne yanafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.
Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bibi. Melika Berak akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Jukwa la Wafanyabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania jana Jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo ya siku nne yanafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa. Kushoto ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Jukwa la Wafanyabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania jana Jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo ya siku nne yanafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa. Kushoto ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Bibi. Melika Berak wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa Maonyesho ya Jukwa la Wafanyabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania jana Jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo ya siku nne yanafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa.Wapili kushoto ni Mwenyekiti wa Mfuko wa Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dkt. Reginald Mengi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akifurahia jambo alipotembelea banda la Kampuni ya Supperdoll (wasambazaji wa Matairi aina Michellin) wakati wa hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya Jukwa la Wafanyabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania jana Jijini Dar es Salaam. Maonyesho hayo ya siku nne yanafanyika katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa. Kutoka kulia kwake ni Balozi wa Ufaransa hapa nchini Melika Berak na Mkurugenzi Mtendaji wa Supperdoll Seif Seif(kushoto).

No comments: