Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akionesha masuke ya zao la
mtama wakati akikagua mojawapo ya mashamba ya wakulima wa Kata ya
Mwaweja wakati wa ziara yake.
Mkulima
wa mtama, Mariam Nkinga (kulia) akiwaonesha Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,
Nyabaganga Taraba na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack
Kangese mtama uliochanua katika shamba lake.
Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (katikati) akiangalia mtama
katika shamba lililopo kata ya Mwaweja wakati wa ziara yake.
Katibu
Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese (kulia) na Ofisa Kilimo
halmashauri ya wilaya hiyo, Sarai Pura wakiangalia mtama uliostawi
katika shamba.
Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba (wa pili kulia) akibadilishana
mawazo na mkulima, Sendama Luhende, Ofisa Kilimo, Sarai Pura na mkulima
Mariam Nkinga wakati wakikagua shamba.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu akiendelea kukagua shamba la mtama katika Kata ya Mwaweja.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga akikagua shamba darasa lililolimwa na Ofisa ugani Kata ya Uchunga, Aristidia Tasingwa.
Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewaagiza
maofisa ugani wa kata zote kuhakikisha wanawafikia wakulima na
kuwafundisha mbinu bora za kilimo chenye tija.
Ameagiza
pia wananchi kulima mazao yanayostahimili ukame hususan mtama na uwele
badala ya kuwa na kasumba ya kung’ang’ania kilimo cha mahindi ambacho
katika sehemu kubwa ya wilaya hakifanyi vizuri.
Taraba
alitoa agizo hilo wakati wa ziara yake kwenye mashamba ya mtama katika
kata za Uchunga, Mwaweja na Ukenyenge kujionea na kufanya tathmini ya
kilimo wilayani humo.
Aliwataka
maofisa hao kujiwekea utamaduni wa kutembelea mashamba ili kuwafundisha
namna ya matumizi ya mbegu bora kwani wengi wao hupanda bila utaalamu.
Aliwataka
kusimamia Sheria ndogo ya mwaka 2008 ya Halmashauri ya Wilaya ya
Kishapu inasisitiza kuwa kila kaya wilayani humo iweze kulima ekari
mbili za mazao yanayostahili ukame ambayo ni mtama.
Mkuu
wa wilaya hiyo alisema kuwa hata hivyo wakulima wengi wilayani humo
wameweza kutekeleza sheria ndogo hiyo lakini wamepata changamoto
mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maarifa ya matumizi ya aina sahihi za
mbegu.
“Ziara
hii imetufundisha mambo mengi kwa mfano shambani hapa tumeshuhudia
wakulima hawa wametumia mbegu za aina tano tofauti katika shamba moja
sasa kama wangepata elimu wangetumia mbegu za aina moja zisizoshambuliwa
na ndege.
”Hivyo
naagiza wataalamu wa kilimo wahamie mashambani kufundisha wakulima na
wawe na mashamba darasa yawe mfano wa kujifunzia wananchi nao waige na
kusonga mbele,” alisisitiza Taraba.
Aidha,
alipiga marufuku wakulima kuuza wa mazao kwa ajili ya matumizi mengine
pasipo kujiwekea akiba na kuonya atakayefanya hivyo atachuliwa hatua
kali ikiwemo kupigwa faini.
Taraba
ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya alionya
kuwa wapo baadhi ya wakulima wana tabia ya kufanya biashara ya mtama kwa
ajili ya kutengeneza pombe huku wao wakibaki bila ya chakula.
Akizungumza
kwa niaba ya wenzake mkulima wa mtama katika Kata ya Mwaweja, Mariam
Nkinga kwa niaba ya wenzake aliomba Serikali iwapelekee mbegu fupi
zinazokua kwa haraka.
Alisema
wanapata changamoto ya mtama wao kuliwa na ndege aina ya kwelea pamoja
na wadudu ukiwa shambani kutokana na mbegu wanazotumia kuchelewa kukomaa
na hivyo kukaa muda mrefu shambani.
Nkinga
alioimba wataalamu wawe wanapita mara kwa mara kunyunyizia dawa mazalia
ya wadudu na ndege waharibifu wa mazao ili wasiweze kuzaliana na kufika
mashambani.
Aliwashauri
wananchi kulima zao la mtama kwa wingi na kuacha kasumba ya kuchagua
chakula na kulima mahindi ambayo matokeo yake hawastawi yanakufa
kutokana na ukame.
No comments:
Post a Comment