Tuesday, April 4, 2017

Balozi Seif Ali Iddi atoa pole wananchi wa Kazole Kwagube walioathirika na upepo mkali jumapili


Othman Khamis Ame, OMPR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesisitiza kauli yake inayotoa kila mara ya kuwataka Wananchi wanaoishi Mabondeni na sehemu nyengine hatarishi zenye kujaa maji wakati wa msimu wa mvua za Masika kuhama mapema ili kujiepusha na athari zinazoweza kuleta maafa.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiwapa pole wananchi wa Kazole Kwagube ambao nyumba zao zipatazo 37  zimeathirika kutokana na upepo mkali uliovuma Jumapili iliyopita ambapo kati ya hizo Nyumba  22 zinahitaji matengenezo.
Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa matangazo kuhusiana na maeneo hayo hatarishi na haitakuwa tayari kuwa na mpango wa kuweka Kambi kama inavyofanya katika miaka ya nyuma kwa ajili ya kuwahifadhi kwa muda watu wanaoishi mabondeni watakaoathirika na mvua za masika.
Alisema inasikitisha kuona kwamba wapo baadhi ya Watu wanaendelea na tabia ya kukaidi  maagizo yanayotolewa na Serikali na matokeo yake hutoa kauli zisiazostahiki licha ya kwamba wao ndio walalamikaji wakubwa wakati wanapokumbwa na kadhia kama hizo.
Akiwapa pole Wananchi hao wa Kwagube ambao wamo ndani ya Majimbo ya Kiwengwa na Mahonda Balozi Seif alisema maafa hayategemewi kama muathirika anaweza kupata muda wa kujitayarisha katika kukabiliana nayo.
Alitahadharisha kwamba hali ya Hewa hivi sasa imebadilika kiasi kwamba Wananchi Wanapojitayarisha kujenga Nyumba za makaazi wazingatie ujenzi unaoweza kukabili mazingira yoyote yanayotokezea.
Balozi Seif aliwaasa Wananchi kwamba mpango wa kujenga nyumba na kuezeka mapaa kwa kutumia njia ya kulaza mabati kwa kidhibiti cha matofali au mawe waelewe kuwa njia hiyo inaweza kuleta athari kubwa hasa wakati unapotokea upepo mkali katika maeneo yao.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema Wataalamu wa Kamisheni yake tayari wameshafanya Tathmini ya athari ya upepo huo ingawa Serikali haitakuwa na nguvu kubwa za kusaidia kurejesha hali ya kawaida kwa Nyumba zilizoharibika na upepo huo.
Nd. Juma alisema tathmini hiyo imetoa muelekeo na kubainisha gharama zilizojichomoza ndani ya zoezi hilo zinazokadiriwa kufikia kati ya shilingi Laki  Moja hadi saba kwa nyumba zipatazo 22 kati ya zile 27 zilizoathirika na upepo huo.
Katika Mkutano huo wa kuwapa pole waathirika wa upepo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Fedha kwa Familia za waathirika 22 kati ya 27 kulingana na tathmini iliyopigwa ya kila nyumba ili zisaidie nguvu za familia hizo kurejesha hali yao ya kawaida.
Waathirika hao ni Bibi Asha Salum, Bwana Makame Juma, Bwana Bakari Daudi, Nd. Ayoub Makame, Bibi Afua Faki, Nd. Suleiman Abdulla, Nd. Haji Zubeir, Nd. Silima Jongo na Nd.  Ali Khamis.
 Wengine ni Hassan Mohamed, Nd. Khamis Haji, Nd. Abdalla Ibrahim, Bwana Makame aliyetambulika kwa jina moja tu, Nd. Khamis Bakari, Nd. Hija Abdulla, Nd. Makame Wadi, Nd. Khamis Khamis, Nd. Mngwali Khamis, Nd. Zawadi Suleiman, Nd. Ussi Khamis, Nd. Yahya Aman na Nd. Khalfan Khamis Hilal.

No comments: