Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Mhe Ummy Mwalimu ameagiza kuanzishwa duka la Dawa ndani ya miezi 3 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
Hayo ameyasema wakati wa ziara ya kikazi mkoani Iringa leo tarehe ambapo ametembelea Kituo cha Damu Salama cha Mkoa pamoja na Hospitali ya wilaya ya Mafinga
“Pia naagiza Uongozi wa Hospitali zote za Mikoa na Wilaya kuanzisha Wodi za Watoto Wachanga na Watoto Njiti mara moja” alisema Mh. Ummy.
Mbali na hayo Waziri Ummy ameagiza kujengwa kwa Kitengo cha Wagonjwa wa Dharura (Emergency Unit) kwa hospitali hizo mara moja ili kuboresha huduma ya afya kwa wakazi wa Iringa.
Akitoa taarifa ya utoaji wa huduma za Afya katika mkoa mbele ya Waziri wa Afya, mhe. Amina Masenza, mkuu wa Mkoa wa Iringa alieleza hatua mbalimbali wanazochukua katika kuboresha utoaji wa huduma ikiwemo kuboresha miundombinu ya vituo vya Afya, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, utoaji wa elimu ya uzazi wa mpango pamoja na lishe kwa wananchi bila kusahau kuhamasisha wananchi kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).
Hata hivyo, zipo changamoto kadhaa zinazowakabili mkoa kufikia lengo la lao kutoa huduma bora za Afya. Mathalani katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Iringa haina wodi/kitengo cha dharura, upungufu wa watumishi, Ufinyu wa eneo la Hospitali, ukosefu wa Gari la Kubebea Wagonjwa na ukosefu wa baadhi ya vitendanishi.
Mhe.Ummy Mwalimu amewapongeza viongozi na watumishi wa mkoa kwa juhudi kubwa wanazofanya katika kuboresha huduma za afya ikiwemo kufanikisha ujenzi wa wodi ya watoto waliozaliwa kabla ya wakati na watoto wachanga. Wodi hiyo yenye vifaa vyote muhimu imejengwa kwa ufadhili wa Kampuni ya ASAS ya Mjini Iringa. Mhe Ummy amewataka wadau wengine waendelee kusaidia sekta hii hususani eneo la Afya ya Mama na Mtoto kwa kuwa linawagusa wananchi wengi hasa wa kipato cha chini.
Kufuatia malalamiko aliyoyapokea kutoka kwa wananchi waliofika kupata huduma katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa, Mhe.ummy aliagiza utekelezaji wa masuala yafuatayo; ujenzi wa wodi ya wagonjwa wa dharura na duka la dawa la Hospitali ili kuondoa usumbufu wanaoupata wagonjwa wa kwenda kununua dawa kwenye maduka binafsi. Pia,aliahidi kulifuatilia suala linalohusu gereza lililopo jirani na Hospitali ya mkoa ili liweze kuhamia sehemu nyingine na kutoa eneo kwa Hospitali. Vile vile, ametoa muda wa miezi 9 kuanzia leo tarehe 16 March kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote Nchini kuhakikisha vituo vyote vya Afya vinatoa huduma kamili za uzazi za dharura ikiwemo upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni.
Akiwa katika Hospitali ya wilaya ya Mufindi, mhe. Ummy aliagiza yafuatayo; uongozi wa wilaya uhakikishe maji yanapatikana muda wote hospitalini, waanzishe mara moja wodi maalum kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na Watoto wachanga. Pia, aliwakumbusha juu kuhakikisha kuwa wazee wote wanatambuliwa na kupewa vitambulisho lakini alipongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya kuwakatia Wazee kadi za Bima (TIKA).
No comments:
Post a Comment