Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya kata ya Pangani,Kibaha Mji,wanakabiliwa na adha ya kutembea umbali wa km.34 kila siku,hali inayosababisha baadhi yao kuwa watoro, kukatisha masomo na kupata mimba.
Aidha shule za msingi zilizopo katika kata hiyo,zina uhaba wa walimu ambapo shule yenye wanafunzi 950 ina walimu kumi pekee hivyo kusababisha muda mwingi wanafunzi kucheza.
Hayo aliyasema diwani wa kata ya Pangani,Agustino Mdachi,wakati alipokuwa akizungumzia changamoto za kielimu ,kwenye ziara ya mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha,Silvestry Koka,aliyoifanya katika kata hiyo.
Alisema,wanafunzi wanaosoma kwenye ya shule ya kata wanapata usumbufu na wapo katika wakati mgumu.
Mdachi alieleza kwamba,hakuna usafiri wa daladala zaidi ya kutumia miguu na pikipiki ambazo wanalipa 10,000 hivyo kusababisha wanafunzi hasa wa kike kurubuniwa na madereva bodaboda na kupata mimba.
“Watoto wetu huku hawamalizi shule ya sekondari,ni watoro,wanakatiza masomo na wengine wakipewa mimba ,hii inatokana na shule yetu ya kata kuwa mbali”alisema Mdachi.
Akizungumzia tatizo la upungufu wa walimu katika shule za msingi ,alisema shule ya msingi kama Lumumba na Kidimu zina wanafunzi zaidi ya 900 na walimu ni 10 pekee hivyo watoto wengi wanacheza ,hawafundishi na kufeli.
Nae mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha,Koka amemuagiza diwani na kamati ya maendeleo kata,kuandika barua ambayo ataisaini na kisha ipelekwe kwa mkurugenzi kuhakikisha anaongeza walimu katika shule hizo.
Alitoa siku 30 kwa mkurugenzi wa halmashauri ya mji huo,kushughulikia suala hilo kwa kuangalia taratibu zinazotakiwa kufuata ili kupeleka walimu watakaosaidia kupunguza adha hiyo.
Koka alifafanua,yawekwe mazingira bora kwa wanafunzi ikwemo kuongeza walimu wa kutosha ,kama ilivyo kwa shule za Mailmoja ambako shule moja ina wanafunzi 500 na walimu 30.Alimtaka mratibu wa elimu kata na idara ya elimu halmashauri ya mji wa Kibaha kusimamia changamoto hiyo kwa kushirikiana na mkurugenzi na kupanga walimu kwa uwiano .
Koka alieleza suala la kutembea umbali mrefu linaumiza watoto,hivyo ingaliwe namna ya kutafuta eneo mtaa wa Kidimu ili jamii ianze kujitolea kujenga shule nyingine na yeye ataongeza nguvu zake.
Diwani wa kata ya Pangani,Agustino Mdachi akizungumza na wananchi wa kata hiyo kwenye ziara ya mbunge wa jimbo la Kibaha Mji,Silvestry Koka aliyoifanya katika kata hiyo.
Baadhi ya wakazi wa kata ya Pangani,wakisikiliza jambo katika ziara ya mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha, Silvestry Koka kwenye kata hiyo.
Mbunge wa jimbo la Mji wa Kibaha ,Silvestry Koka,akizungumza jambo katika ziara yake kata ya Pangani .(picha na Mwamvua Mwinyi).
No comments:
Post a Comment