Wednesday, March 15, 2017

RAIA SITA WA PAKISTANI NA MMOJA WA SRI-LANKA WAPANDISHWA KIZIMBANI MAHAKAMA YA KISUTU WAKITUHUMIWA NA MASHITAKA SABA

Karama Kenyunko wa blogu ya jamii.

Raia sita wa Pakistani na mmoja wa Sri-Lanka wanaoishi  jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakamani wakikabiliwa na mashitaka saba likiwemo la kula njama, kutoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kuisabishia serikali na mamlaka hiyo hasara ya Sh. Milioni 459.

Washtakiwa hao wamesomewa mashitaka yao leo  mbele ya Hakimu Mkazi Wilbard Mashauri wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.  Jamhuri imewakilishwa na Mawakili wa Serikali Nassoro Katuga aliyekuwa akisaidiana na Mwanasheria Mkuu wa TCRA, Johannes Karungula.

Wakili Katuga amewataja watuhumiwa hao kuwa ni, Dilshad Ahmed,Rohail Yaqoob, Khalid Mahmood, Ashfaq Ahmad, Muhammad Aneess, Ramesh Kandasamy na Imtiaz Ahamad Ammar.

Katika shtaka la kwanza imedaiwa, kabla ya Novemba mwaka Jana, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kutenda kosa la matumizi ya Huduma za network kinyume cha sheria.

Katika shtaka la pili, washtakiwa hao wamedaiwa, kati ya Novemba mwaka Jana na Februari mwaka huu, bila halali na kwa makusudi washtakiwa wakiwa na nia ya kukwepa malipo halali walitoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa bila leseni ya TCRA.  

Aidha siku hiyo washtakiwa hao walitoa huduma za simu za kimataifa kwa kupokea na kutoa Huduma hizo za network bila kuwa na leseni ya TCRA.

Wakili Katuga aliendelea kudai kuwa, kati ya Novemba 20, mwaka jana  jijini Dar es Salaam, washtakiwa waliingiza nchini Tanzania vifaa vya mawasiliano bila ya kuwa na leseni ya TCRA.

 Iliendelea kudaiwa kuwa, Novemba mwaka jana, washtakiwa hao walisimika mitambo electroniki zikowemo laptop mbili bila leseni ya TCRA.  

Ilidaiwa katika shitaka la sita, washtakiwa hao kwa nia ovu na kwa makusudi, walitumia mitambo ya elektroniki ambayo ilikuwa haijathibitishwa na TCRA kutoa huduma ya mawasiliano ya kimataifa.  Katika shitaka la saba ilidaiwa kuwa, kati ya Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu, jijini Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa hawana leseni ya kuwaruhusu kufanya huduma za mawasiliano walichepusha simu za kimataifa na kuisababisha hasara ya Sh. Milioni 459 kwa TCRA na serikali.

Washtakiwa hawakutakiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya  wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi. 

upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na imeahirishwa hadi Machi 29. Mwaka huu

No comments: