Thursday, March 2, 2017

SERIKALI YANUNUA MTAMBO WA KISASA WA MILIOINI 101.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamenunua mtambo mpya wa kisasa unaojulikana kama ‘Energy Dispersive X-Ray Fluorescence Spectrometer’ (EDXRF) kwa ajili ya kurahisisha uchunguzi wa kimaabara.

Mtambo huo uliogharimu kiasi cha shilingi 101,785,200 umesimikwa katika Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Mbeya kuanzia Februari 21 hadi 23 mwaka huu.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali. Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matumizi ya mtambo huo.

Prof. Manyele amesema kuwa mtambo huo umesimikwa mkoani mbeya ikiwa ni moja ya hatua za kuboresha maabara za Kanda zilizopo Arusha, Dodoma, Mbeya, Mtwara na Mwanza, kusogeza shughuli za uchunguzi karibu na wananchi ili kupunguza gharama za kusafirisha sampuli kuja mkoani Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.

“Kuwepo kwa mtambo huo ni suluhisho kwa Serikali, Wizara, Viwanda, Mashirika, Wachimbaji wa madini, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla ambao walikuwa wanahitaji kufahamu ubora na usalama wa bidhaa mbalimbali za viwandani na mashambani, kutambua uwepo wa madini ya thamani kwenye udongo na bidhaa za vito pamoja na sampuli zinazohusiana na usalama wa afya na mazingira,”alisema Prof. Manyele.

Ameyataja matumizi mengine ya mtambo huo kuwa ni kufanya uchunguzi wa sampuli za migodini, kupima bidhaa za mbao ili kubaini kiwango cha kemikali zinazotumika kutibu mbao, kupima sampuli za mafuta ya kula kwa kuangalia kiwango cha madini ya phosphorus, kupima sampuli za pembejeo za kilimo pamoja na kufanya uchunguzi wa sampuli na vielelezo vinavyohusiana na makosa ya jinai.

Prof. Manyele amefafanua hoja zitakazojibiwa na matumizi ya mtambo huo zikiwemo za kufahamu dhahabu kiasi gani ipo katika udongo unaohitaji kuchenjuliwa, kufahamu mbogamboga zinazolimwa bondeni zina kiasi gani cha madini yanayoathiri watumiaji, kufahamu kiasi cha uranium katika ardhi na vyanzo vya maji pamoja na kufahamu athari za aina ya madini yaliyopo katika maji ya visima virefu na vifupi kwa watumiaji.

Aidha, Mkemia Mkuu amebainisha kuwa baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo, Maabara ya Nyanda za juu kusini itakua na majukumu ya kukusanya sampuli za vinasaba vya binadamu (DNA) pamoja na kuwa kituo rasmi cha kukusanyia sampuli nyingine mbalimbali.

Maabara hiyo kwa sasa ipo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ambapo kuanzia mwezi Aprili mwaka huu itahamia katika eneo la Lwambi lililopo mkoani humo.
Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kazi kwa mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X Ray Fluorescence (EDXRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara.Kutoka kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Huduma za Ubora wa Bidhaa, Bw. Daniel Ndiyo, Mkurugenzi Idara ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali Nchini, Bw. Sabanitho Mtega kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Biashara Bw. George Kasinga pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi Jinai na Huduma za Vinasaba,Bw. David Elias.
Baadhi ya watumishi wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele (hayupo pichani) leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza kuhusu kuanza kazi kwa mtambo mpya wa kisasa wa Energy Dispersive X Ray Fluorescence (EDXRF) kwa ajili ya kufanyia uchunguzi wa kimaabara. Mtambo huo umefungwa kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoani Mbeya.
Mtambo wa Energy Dispersive X – Ray Fluorescence (EDXRF) kushoto unaotumika kupima sampuli mbalimbali zenye asili ya yabisi na vimiminika kama vile vyakula, bidhaa za mafuta, maji, simenti, makaa ya mawe, bidhaa za chuma ili kutambua kiwango cha madini kilichomo ndani ya sampuli hizo. Mtambo huo umefungwa kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoani Mbeya.

No comments: