Wednesday, March 1, 2017

RIWAYA KUPATIKANA KUPITIA PROGRAMU MAALUM NCHINI


Picha na Daudi Manongi-MAELEZO.

Na Daudi Manongi-MAELEZO
Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira (UWARIDI) umezindua mfumo maalum wa kuuza,kununua na kusoma riwaya kwa njia ya simu iitwayo “UWARIDI APP” leo Jijini Dar es Salaam.

Akizindua Programu hiyo Katibu Mkuu wa Umoja huo Bw. Bw.Ibrahim Gama amesema kuwa wameamua kuanzisha programu hii ili kuwawezesha wanachama wa UWARIDI kuweka riwaya zao kwa ajili ya kuuzwa na wao kujipatia malipo kutoka kwa mtengenezaji wa app hiyo.

“Kwa miaka mingi waandishi wa riwaya wamekuwa wakijaribu kutafuta njia mbalimbali za kunadi kazi zao ili kuwafikia wasomaji wao kwa urahisi,na tukaona changamoto wanazopata katika kuzipata kazi zetu na hivyo tukaamua kuandaa program hii itakayowawezesha kupata riwaya zetu kwa urahisi zaidi kwani utahitaji kuwa na programu hii tu kwenye simu yako ili kusoma muda wowote”,Aliongeza Bw.Gama.

Katika mfumo huo kutapatikana riwaya za waandishi mchanganyiko ikijumuisha waandishi nguli na wachanga  ambapo mpaka sasa zaidi ya waandishi 20 wameweka riwaya zao katika mfumo huo na zinaendelea kuongezeka kila siku.

Aidha sababu kuu za kuanzisha mfumo huu ni wauzaji wa vitabu vya riwaya wamekuwa hawapati malipo ya vitabu vyao kwa wakati wanapozikabidhi kwa wachuuzi wa vitabu kwa utaratibu wa kupata malipo baada ya kuuza vitabu hivyo, pia kukosekana kwa maduka rasmi ya vitabu vya riwaya nchini na wasanii wachanga na wanaochipukia kutokuwa  na uwezo wa kifedha wa kuchapa vitabu.

Kwa upande wake Rais wa UWARIDI Bw.Hussein Tuwa alieleza faida za mfumo huo kwa watumiaji wake kwa kusisitiza kuwa kazi zitakazokuwa katika mfumo huo zitakuwa salama kwa kutoweza kunakiliwa na kuuzwa nje ya mfumo,pia waandishi wake watapata pesa kwa wakati,waandishi wachanga ambao hawajaweza kuchapisha vitabu vyao wataweza kuweka kazi zao kwa urahisi tofauti na kusubiri kuzi kuchachapwa kitabuni pamoja na wasomaji walioko mbali na maeneo walipo waandishi watazipata riwaya hizi kwa urahisi na wakati wowote.

UWARIDI ni umoja uliosajiliwa rasmi serikalini mwaka 2016 ukiwa unaundwa na mchanganyiko wa waandishi mahiri na wale wanaochipukia katika uandishi wa riwaya nchini.
 Katibu wa Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira(UWARIDI) Bw.Ibrahim Gama akizungumza na waandishi wa habari juu ya uzinduzi wa programu(App)  ya kuuza ,kununua na kusoma riwaya kwa njia ya simu iitwayo “UWARIDI APP” iliyozinduliwa na Umoja huo leo Jijini Dar es Salaam.Kulia kwake ni Rais wa UWARIDI Bw.Hussein Tuwa.
 Rais wa Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira(UWARIDI) Bw.Hussein Tuwa akizungumzia uanzishwaji wa programu(App)  ya kuuza ,kununua na kusoma riwaya kwa njia ya simu iitwayo “UWARIDI APP” iliyozinduliwa na Umoja huo leo Jijini Dar es Salaam.Kushoto ni Katibu wa Umoja wa umoja huo Bw.Ibrahim Gama na Abdillahi Muna kutoka Dau Technology ltd.
 Mwakilishi kutoka Dau Technology Limited Bw.Abdillahi Muna(wa kwanza kulia) akieleza jinsi program ya “UWARIDI APP” iliyozinduliwa leo na Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira(UWARIDI) kwa ajili ya kuuza ,kununua na kusoma riwaya kwa njia ya simu.Dau Technology ndio watengenezaji wa App hiyo.Wengine ni Rais wa Umoja huo Bw.Hussein Tuwa na katibu wake Bw.Ibrahim Gama.

Viongozi wa Umoja wa waandishi wa Riwaya wenye Dira(UWARIDI)Rais wa umoja huo  Bw.Hussein Tuwa na Katibu wake  Bw.Ibrahim Gama wakionyesha  waandishi wa nembo ya program yao mpya waliyoizindua leo Jijini Dar es Salaam.

No comments: