Thursday, March 9, 2017

RC Maganga apiga marufuku vitendo vya unyanyasaji kwa wanawake mkoani Kigoma,awataka waachwe wachangamkie fursa za kimaendeleo.


Na Rhoda Ezekieli Kigoma

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga amepiga marufuku vitendo vya baadhi ya wanaume Mkoani humo kuwadhurumu na kuwatishia kuwafukuza wake zao pindi wanapothubutu kutetea haki zao,badala yake amewataka washirikiane nao kutambua na kuchangamkia fursa za maendeleo zilizopo nchini.

Mkuu huyo wa Mkoa aliitoa kauli hiyo wakati akifunga maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Mkoani humo ambayo kimkoa yalifanyika katika kijiji cha kinyinya kata ya nyamutukuza wilayani kakonko Mkoani humo .
 
RC Maganga alisema kuwa pamoja na mambo mengine, wakati umefika kwa wanawake kuamka na kusimamia haki zao ikiwa ni pamoja na kutokukubali kubaki nyuma kwa kuchangamkia fursa hizo zinapozitokeza.

Alisema kumekuwa na tabia ya Wanaume wengi,Wake wanapo kuwa wakijishughulisha kutafuta fedha ili kuzitunza familia zao, wanawanyang'anya na kwenda kuzitumia kwenye  starehe zao, suala ambalo linarudisha nyuma maendeleo ya Wanawake wengi.
 
Katika kuhakikisha suala la kuwa Nchi ya viwanda, ni lazima wanawake kushirikiana na wanaume katika kufanya kazi ili kuongeza kipato katika familia na taifa kwa ujumla.

" wanawake Msikubali hawa wanaume wawanyanyase, akikutishia uondoke njoo ushitaki kwangu ataondoka yeye na akuache wewe unalea familia, nataka mpaka muda wangu utakapo fika wa kuondoka Kigoma kila mtu awe na eneo lake mwanamke na mwanaume, na eneo moja kwa ajili ya familia lazima tuhakikishe tunatoka katika mfumo wa unyanyasaji katika kuelekea, uchumi wa viwanda", alisema Maganga.

Aidha Maganga alisema ni wakati wa Wanawake kufanya mapinduzi ya ghafla katika kuelekea hamsini kwa hamsini kama kaurimbiu ya mwaka huu inavyo sema Tanzania ya Viwanda mwanamke ni msingi wa mabadiliko Kiuchumi kwa kutambua uthamani huo wanawake wanatakiwa kutumia Fursa hiyo kuunda vikundi vya ujasiliamali na kuanza kuzalisha bidhaa na kuziongezea ubora.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala aliwataka wanawake Wilayani humo kuunda vikundi vya ujasiriamali iliwaiwe rahisi kwa baadhi ya taasisi zinazo jitolea kutoa elimu za ujasiriamali na mikopo mbali mbali ilikuwawezesha iwe rahisi kupata msaada huo.

Ndagala alisema katika vikundi watakavyo anzisha wajitahidi kuanzisha vikoba pamoja na ununuzi wa hisa vitakavyo wasaidia kuinuana kiuchumi na kauri mbiu ya kuelekea katika Nchi ya viwanda kufikiwa kwa urahisi.

Nae Afisa Maendeleo ya Jamii mkoani Kigoma Zilpa Kisonzela alisema mpaka sasa Mkoa wa kigoma umekwisha toa shilingi milioni 375 kwa vikundi mbali mbali vya wajasiriamali vinavyo endelea kuwawezesha wanawake wengi kufanya biashara zao kwa kuzalisha bidhaa mbali mbali zenye ubora na kuziuza ndani na nje ya Nchi.

Sambamba na kutoa fedha hizo kumekuwa na elimu inayo tolewa kwa wajasiriamali wanao thubutu katika vikundi mbali mbali kwa kuwaelimisha jinsi ya kuzalisha bidhaa zenye ubora na usindikaji wa matunda, katika eneo la Viwanda vidogo vidogo SIDO mkoani humo kumekuwa na wajasiliamali wakubwa wanao zalisha unga wa muhogo, mafuta ya mise, Sabuni za magadi na sabuni za kusafishia chooni ni bidhaa wanazo ziuza nje na ndani ya Nchi na zinaendelea kuwaongezea kipato.

Maadhimisho ya siku ya wanawake Mkoani Kigoma yameanza kwa mkuu wa Mkoa huo Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga kuongoza zoezi usafi na uchangiaji damu katika kituo cha afya cha nyanzige na kutoa zawadi mbali mbali kwa wanawake walio jifungua na waliojitokeza katika maadhimisho hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali mstaafu Emanuel Maganga akitoa zawadi kwa mmoja wa akina mama aliyejifungua katika kituo cha afya cha Nyanzige,Wilayani Kakonko mkoani Kigoma.
RC Maganga akiwasikiliza akina mama mbalimbali waliofika katika kituo cha afya cha Nyanzige,Wilayani Kakonko mkoani Kigoma kujipatia matibabu mbalimbali,kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kakonko,Kanali Hosea Ndagala
Akina Mama wakisherehekea siku ya Wanawake hapo jana
RC Maganga akiwa ameongozana na DC wa Kakonko,Kanali Hosea Ndagala wakipata maelezo mbalimbali kutoka kwa wajasiliamali,kufuatia bidhaa zao walizozitengeneza

No comments: