Thursday, March 9, 2017

MIKAKATI YA SERIKALI KATIKA KUMUINUA MWANAMKE KIUCHUMI

Jovina Bujulu – MAELEZO.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ni hatua muhimu kwa wanawake kujipambanua na kufanya tathmini jinsi wanavyoshiriki katika ujenzi wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Serikali imeweka mikakati na mipango mbalimbali yenye lengo la kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto, mama Sihaba Nkinga hivi karibuni alipokuwa akizungumzia mipango na mikakati mbalimbali iliyofanywa na Serikali katika kumkomboa na kumuinua mwanamke kiuchumi.

Pamoja na kuwa wanawake wengi wameamka na wanajishughulisha katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, Serikali pia inahakikisha inawawezesha ili waweze kufikia malengo yao katika masuala ya kujiinua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.

“Serikali ina mipango mbalimbali katika kuhakikisha kuwa wanawake wamewezeshwa kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha benki ya Wanawake ambayo moja ya majukumu yake ni kuhakikisha wanawake wanapata mikopo kwa kuzingatia viwango wanavyoweza kulipa” alisema mama Nkinga.

Aliitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuwa na mfuko wa maendeleo ya wanawake ambapo wanawake wanapewa mikopo yenye riba nafuu ambayo wanamudu kuilipa.

Aidha, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza kuwasaidia wanawake katika masuala ambayo yamekuwa yakiwasumbua kwa muda mfefu kama vile umiliki wa ardhi. Kupitia elimu hii kwa sasa wanawake wanaruhusiwa kumiliki ardhi kisheria na kuondoa utata kuhusu suala hili.

Pamoja na mikakati hiyo, Serikali imeenelea kushirikiana na wadau kuhakikisha kuwa vikwazo mbali mbali vya mitaji na mikopo vinaondolewa ili kuhakikisha kuwa wanawake wengi wanapata fursa ya kukopa na kulipa kwa muda hivyo kuwa huru kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.

“Idadi kubwa ya wakina mama wapo kwenye ujasiriamali na viwanda vidogo vidogo hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwao na kuwahimiza kukopa kwenye vyombo na taasisi za fedha kwa sababu huko wanakopa kulingana na uwezo wao na hii itawasaidia kufanikisha shughuli zao za ujasiriamali“ aliongeza mama Sihaba .

Aliwaasa wanawake kuachana na sekta isiyo rasmi na badala yake wajikite katika sekta rasmi maana huko kuna uzalishaji mkubwa ambao utawapatia soko la nje na aliwataka kuboresha bidhaa zao ili wawe tayari katika ushindani mkubwa zaidi wakati nchi yetu ikielekea katika uchumi wa viwanda.

Akizungumzia fursa na mlingano wa ajira kati ya wanawake na wanaume alisema kuwa upande wa ajira wote wanawake na wanaume wana nafasi sawa na kinachozingatiwa ni vigezo na sifa za waombaji wa ajira.

Katibu Mkuu huyo aliendelea kusema kwa sasa hakuna kazi za wanaume peke kwani upo uhalisia juu ya ushiriki wa wanawake wengi katika kazi za uhandisi, ukandarasi na udaktari.

Alitoa wito kwa wanawake, jamii na watanzania kwa ujumla kuitumia siku hii kutoa hamasa kwa wanawake na kuangalia nafasi yao katika jamii kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea katika uchumi wa kati na viwanda.

Ili kufikia azma ya uchumi wa viwanda, ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha Umoja wa nchi yetu na Utanzania wetu kwa kuwashirikisha wanawake, kwa kutoa elimu na kuwapa nafasi ili watoe mchango wao ipasavyo katika kuinua uchumi wa nchi.

Aidha, mama Nkinga alihimiza jamii kusimamia watoto wa kike na kuhakikisha wanapewa haki inayostahili ili nao wafike mahali waweze kutoa mchango wao kwa taifa.

Siku ya wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo tarehe 8, Machi kwa shughuli mbalimbali kama vile maandamano na hotuba, pia wanawake hutumia nafasi hiyo kutathmini mafanikio ya shughuli zao za maendeleo, changamoto zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo. Kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya viwanda, wanawake ni msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.”

No comments: