Thursday, March 23, 2017

NINAYO YASHIRIKIANA NA HEIFER INTERNATIONAL KUWANUFAISHA WAKULIMA

 
Afisa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya NINAYO Jack Langworthy akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari juu ya kuanzisha ushirikiano baina ya kampuni hiyo na shirika lisilo na kiserikali la Heifer utakaowawezesha wakulima kufikia masoko kupitia njia ya mtandao wa www.NINAYO.com .Kushoto ni Mkurugenzi mkazi wa Heifer International Tanzania Bi. Leticia Mpuya.
Meneja uendeshaji wa kampuni ya NINAYO Bovan Mwakyambiki akiungumza katika mkutano na waandishi wa habari juu ya kuanzisha ushirikiano baina ya kampuni hiyo na shirika lisolo na kiserikali la Heifer International Tanzania utakaowawezesha wakulima kufikia masoko kupitia njia ya mtandao www.NINAYO.com Kulia ni Afisa mtendaji mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya NINAYO Jack Langworthy.


Kampuni ya Ninayo kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Heifer International Tanzania ambalo limejikita katika kuondoa umasikini na matatizo ya njaa leo wameshirikiana katika kuwasaidia wakulima wa Tanzania kupata taarifa zote zinazohusu mauzo au manunuzi ya mazao mbalimbali kupitia mtandao wa Ninayo.com.

Ninayo ni jukwaa la mtandao wa kibiashara unaowawezesha wakulima kuuza, kununua au kuangalia bei elekezi za mazao mbalimbali yatokanayo na kilimo pia kuwapa uwanja mpana wa kulifikia soko la bidhaa hizo kwa urahisi.

Njia hii ya mtandao imejikita katika kutatua mambo makubwa matatu ikiwemo tatizo la kushindwa kwa mkulima katika usambazaji ambapo wanunuaji/wateja hawafahamu ni mazao ya aina gani wakulima wanauza, Mahitaji yasiyofahamika ambapo wakulima hawafahamu ni kiasi gani wanunuaji wapo tayari kununua mazao yao na kukosekana kwa utaratibu wa kuwaunganisha wanapohitaji kufanya biashara za mazao yao.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ninayo Jack Langworthy alisema matumizi ya intaneti yanazidi kukua kwa kasi sana nchini Tananzia, na hivi sasa intaneti imesambaa hadi vijiji maskini.

“Tunashukuru kwa kukua kwa kasi ya mitandao hasa kupitia simu za mkononi, ni uvumbuzi ambao umeleta mapinduzi katika kila sekta duniani, kuanzia kwenye bishara ya teksi, hoteli na zaidi sasa inaweza kupatikana kwa wakulima katika masoko ya Tanzania kukabiliana na mahitaji mahitaji mbalimbali ya chakula kwa bei elekezi kwa watu wote na hivyo kupunguza upotevu wa mazao mbalimbali”.

Ninayo itasaidia kuwaunganisha wakulima kwa pamoja katika soko rasmi, na itaweka bei elekezi kwenye biashara ya mahindi, maharage, ndizi, maembe, matikiti maji pamoja na bidhaa nyingine nyingi za kilimo katika kuleta uwazi na ukweli wa bei ya soko na hivyo kuwawezesha wakulima kujivunia mazao yao.

Aliongeza kuwa Ninayo mpaka sasa imefanikiwa kuwaunganisha wakulima wa mikoa kama Iringa, Mbeya, Morogoro na Njombe pamoja na wanunuaji wa bidhaa zao, jambo lilisaidia kuongeza kipato chao.

Aliendelea kusema kuwa Ninayo inaunganisha hadi wakulima wasio na uwezo wa kupata intaneti kwa kupitia njia ya ujumbe mfupi wa maneno.kwa upande wake Mkurugenzi wa Heifer International Tanzania Bi. Leticia Mpuya alipongeza juhudi zinazofanywa kupitia mtandao huo akisema itasaidia kuwaunganisha wakulima na wateja wao nchini na Afrika mashariki yote.

Ushirikiano kati ya Ninayo na Heifer International ni katika kuelimisha wakulima jinsi ambavyo wanaweza kunufaika kwa kuuza mazao yao kwa kupitia mtandao huo. Heifer ambao wanafanya kazi na mamia ya wakulima nchini itawasaidia wakulima wake kutumia mtandao wa Ninayo ili waweze kujipatia faida kwa kuhakikisha wanauza bidhaa zao kwa bei za kujiridhisha.


“Kama shirika linalohusika na kutokomeza njaa na umaskini, huwa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuhakikisha wakulima wanauza mazao yao kulingana na bei zilizo za kibiashara na kwa manufaa kwao pia kupata wanunuzi sahihi na hivyo kupitia mtandao huu utasaidia kusulisha changamoto hiii” alisema.

No comments: