Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo akitoa ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa
Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo
MD Kayombo akisisitiza jambo
Na Mathias Canal, Dar es salaam
Maafisa Watendaji wa Kata 14, Watendaji wa Mitaa 91 pamoja na Wahasibu wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wameonywa kutopokea Rushwa wala hongo ya aina yoyote kutoka kwa wamiliki wa biashara mbalimbali katika Manispaa hiyo kwani kufanya hivyo watadhoofisha ukusanyaji wa mapato ya serikali kama ilivyokusudiwa.
Kauli ya onyo imetolewa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati akitoa ufafanuzi wa muongozo wa ukusanyaji wa mapato na kutoa maelekezo ya majukumu ya kazi kwa Maafisa Watendaji wa Kata na Mitaa kwenye kikao cha kazi kilichofanyika leo Jumamosi Machi 18, 2017 katika ukumbi wa Ofisi za Manispaa hiyo ilipo Mtaa wa Kibamba CCM.
Kayombo ameeleza kuwa kwa mtumishi yoyote wa Manispaa kwa ngazi yoyote atakayebainika kujihusisha na ubadhilifu kwa kuchukua Rushwa kwa walipa kodi atachukuliwa hatua Kali za kisheria kwa kuiibia serikali kwani kuihujumu serikali kwa kuiibia mapato au kuzuia ukusanyaji wa mapato ni kosa kwa mujibu wa taratibu na sheria.
“Nina amini kwamba mnaishi vizuri na wananchi wenu kwahiyo mnawafahamu vizuri wafanyabiashara wanaokwepa kulipa Kodi lakini hata walipaji wazuri hivyo jambo la ukusanyaji mapato litakuwa jepesi sana kwenu kutokana na uzoefu mlionao” Aliongeza Kayombo
Mkurugenzi huyo amewasisitiza Watendaji hao kusimamia vyanzo vyote vya mapato ikiwemo Hotel Levy, Service Levy, Mabango makubwa na madogo (Bill Board), Leseni za biashara na Vileo, Upimaji afya kwa ngazi za Mitaa hususani katika Migahawa.
Hata hivyo amewataka Watendaji hao kufanya kazi kwa ushirikiano, Uaminifu, na Weledi mkubwa kwani kufanya hivyo kutasababisha ukusanyaji mkubwa wa Mapato kwa mwaka 2016/2017.
Kayombo Amewataka Watendaji wote kukagua Maduka yote katika maeneo yao ya kazi ili kubaini Maduka yasiyokuwa na leseni na Yale yenye leseni kuwa na Leseni za Manispaa ya Ubungo kwani wafanyabiashara wa Maduka mengi wamekuwa na kisingizio cha kukata leseni na Kodi mbalimbali katika Manispaa ya Kinondoni na kutaka kulazimisha kuitumia leseni hiyo kama halali kwa Manispaa ya Ubungo.
Sambamba na hayo pia MD Kayombo amewataka Maafisa biashara kutochelewesha leseni za wafanyabishara waliokamilisha taratibu zote za kumiliki leseni kwani kufanya hivyo ni kuchelewesha huduma kwa wananchi na kuongeza makwazo kwa wafanyabishara kwa sababu tu ya kuchelewa kusaini leseni.
Alisema kuwa litakuwa ni jambo la aibu na lisilovumiliwa kwa kuruhusu sheria zitungwe kwa umakini mkubwa lakini utekelezaji wake uwe hafifu.
MD Kayombo aliongeza kwa kusema kuwa hakuna Haki bila wajibu hivyo Watendaji hawapaswi kufanya kazi kwa mazoea lakini pia kutofanya kazi kwa kuongozwa na tamaa.
MD Kayombo amesema kuwa Oparesheni hiyo ya itakayodumu kwa miezi mitatu ya ukusanyaji wa mapato itaanza jumatatu Machi 20, 2017 kwa ushirikiano baina ya watendaji kutoka Makao makuu ya Wilaya, Watendaji wa Kata, Watendaji wa Mitaa na wenyeviti wa serikali za Mitaa.
No comments:
Post a Comment