AFISA Ustawi wa Jamii Wilaya ya Wete Haroub Suleiman Hemed amewatumia zigo la lawama baadhi ya wakuu wa Taasisi na Idara za Serikali kwa akidai kwamba hawana mchango wowote katika kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji .
Amesema baadhi ya wakuu hao wa Idara na Taasisi za Serikali wameshindwa kuonyesha nguvu zao katika kuunga mkono mapambano dhidi ya matendo hayo yanayoendelea kuiathiri jamii wakiwemo watoto wadogo .
Akizungumza kwenye kikao cha Maofisa wa Serikali ya Wilaya ya Wete , kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya , amesema wakuu hao wa Idara na Taasisi ni kikwazo kinachoviza mafanikio ya kuyatokomeza matendo hayo.
Ameeleza kwamba baadhi ya watumishi wa Serikali wanaokabiliwa na kesi ya udhalilishaji , hawahudhurii kikao wakiitwa huku hata wakuu wao wa taasisi hizo nao pia wameshindwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii kutafuta ufumbuzi wa masuala hayo.
“Baadhi ya wakuu wa Idara NA Taasisi za Serikali wanakuwa ni kikwazo katika kufanikisha mapambano dhidi ya matendo ya udhalilishaji , kwa kuwa wanashindwa kutoa ushirikiano wanapotakiwa kufanya hivyo ”alisema.
“Kuna kesi ya utelekezaji wa watoto inayomuhusu mtumishi wa Serikali , lakini kila nikimwita Ofisini hafiki , pia nimejaribu kumpa taarifa mkuu wake wa Idara naye ameshindwa kunipa ushirikiano ”aliongeza.
Sambamba na hayo ameendelea kusema kuwa baadhi ya kesi hushindwa kuendelea mahakamani kwa kukosa ushahidi baada ya jamii kutofika kutoa ushihidi kutokana na kuwepo kwa vitendo vya rushwa muhali .
Kwa upande wake Afisa wa wanawake Wilaya hiyo Siti Suleiman amesema wizara yake inaendelea kuchukua hatua za kuwaelimisha viongozi wa dini na kwamba kwa sasa wanaendelea na kazi ya kutoa taaluma kwa wananchi kupitia njia tofauti .
Aidha amesema kutokana na elimu inayoendelea kutolewa imewawezesha wanawake kuwa na mwamko katika kuyaripoti matukio yanapotokea katika maeneo yao .
“Wizara imekuwa ikichukua hatua za makusudi kuwaelimisha viongozi wa dini kushiriki kutoa elimu dhidi ya matendo ya udhalilishaji na kwa kiasi Fulani tumeweza kuleta mabadiliko ”alieleza.
Katibu tawala wilaya hiyo Mussa Ali Mohammed kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo ambapo amewataka wakuu hao wa idara na taasisi za serikali kuhakikisha wanasimamia vyema majukumu ya kazi zao .
Alitaka kupewa jina na taasisi ya Mkuu wa Idara ambaye ameshindwa kushirikiana na Ofisi ya Ustawi wa Jamii kumshuhulikia mtumishi wa Serikali ambaye anadaiwa kuendesha vitendo vya udhalilishaji .
“Hautuwezi kuwakumbatia watumishi wa aina hii , kama mtumishi wa Serikali anatakiwa kuwa mstari wa mbele kushiriki mapambano dhidi ya vitendo hivi ambapo kampeni yake ilifunguliwa na Rais Dr Shein ”alisisitiza.
Kikao hicho ni cha kawaida chenye lengo la kukumbushana wajibu wa kila Mkuu wa Idara na Taasisi ya katika kuwatumikia Serikali wananchi .
Na Masanja Mabula –Pemba
No comments:
Post a Comment