Tuesday, March 28, 2017

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA NA SERIKALI YATEMBELEA WALENGWA WA TASAF KATIKA KIJIJI CHA MLANDA IRINGA VIJIJINI.

NA ESTOM SANGA-TASAF

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wametembelea kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa kukagua shughuli zinazotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini-PSSN.

Wakiwa kijijini hapo wajumbe wa kamati hiyo wameonyesha kuridhishwa kwao na namna Mpango huo ulivyohamasisha wananchi kuboresha maisha yao ikiwemo ujenzi wa nyumba za mabati,kusomesha watoto,kuanzisha miradi midogo midogo ya kuichumi na kuboresha afya za familia za kaya hizo.

Akizungumza na walengwa wa Mpango huo na viongozi, Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Venance Mwamoto, ametaka serikali wilayani humo kuhakikisha kuwa wataalamu wa ugani wanawatembelea walengwa wa Mpango huo kuwapa ushauri wa namna bora ya kuendesha miradi wanayoianzisha.

‘’Tusiiachie TASAF kwani nyie ndiyo mko karibu na walengwa hao,ili waweze kufanikiwa zaidi wanahitaji hamasa na utaalamu wenu’’ alisisitiza Mhe. Mwamoto.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki ametoa rai kwa watendaji kuhakikisha kuwa watu wanaolipwa ruzuku ya TASAF ni wale tu waliokidhi vigezo vya umasikini vilivyowekwa.

Aidha Waziri Kairuki amesema ni dhamira ya serikali kuboresha maisha ya wananchi ili kuwaondolea kero ya umasikini. Hata hivyo amesisitiza kuwa walengwa wa Mpango huo waunde vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kunufaika na utaratibu wa mikopo inayotolewa na hivyo kukuza uwezo wao wa kukopesheka.
 Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na  Serikali za Mitaa wakionyeshwa  mabati aliyoyanunua mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mlanda ,Iringa Vijijini ,Bi. Konjeta Lyambafu aliyevaa kitambaa kichwani. Kushoto kwake Mwenyekiti wa kamati hiyo Venance Mwamoto akimkabidhi fedha zilizochangwa na wajumbe kuongeza uwezo wa mlengwa huyo kukamilisha mabati ili aezeke nyumba yake iliyoko nyuma yao kwa bati.

 ‘’Ninaishukuru serikali kupitia TASAF kwa kuniwezesha kuboresha maisha kwa kujenga nyumba ya bati na kumudu kuwatunza na kuwasomesha wajukuu zangu wanane ’’ ndivyo mmoja wa walengwa wa Mpango wa kunusuru kaya masikini Bi. Claudia Kanyita mkazi wa kijiji cha Mlanda, wilaya ya Iringa Vijijini anavyoelekea kuwaeleza wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Angellah Kairuki .

 Mmoja wa walengwa wa TASAF katika kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa Vijijini Claudia Kanyita akiwa na wajukuu zake watatu alioachiwa baada ya watoto wake kufariki, akitoa maelezo kwa kamati ya kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyotembelea kijiji hicho kuona utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF. Nyumba inayoonekana nyuma yao imejengwa na Mlengwa huyo kwa ruzuku ya TASAF.Wa  kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga.

 Wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge wavutiwa na jitihada za mlengwa wa TASAF Bi.Claudia kijijini Mlanda na kumchangia fedha ili aanzishe mradi wa kumwongea kipato, fedha hizo alikabidhiwa na Waziri Kairuki.

 ‘’Mgeni njoo mwenyeji apone ’’ndivyo ilivyo kwa mlengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini wa  kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa vijijini  Konjeta Lyambafu aliyechangiwa fedha na wajumbe wa  kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ili aweze kuongezea fedha anazozipata kupitia ruzuku inayotolewa na TASAF kuanzisha mradi wa kujiongezea kipata. Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Venance Mwamoto akimkabidhi fedha hizo mlengwa, kulia kwao ni Waziri Angellah Kairuki . Nyumba iliyoko nyuma yao imeezekwa na mlengwa huyo kwa bati alizozinunua kupitia ruzuku kutoka TASAF  na hivyo kuboresha makazi yake.

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti na Utumishi wa Umma na Utawala bora, Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na mmoja wa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na TASAF katika kijiji cha Mlunda ,Iringa Vijijini, wakati kamati ya kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa ilipotembelea kijiji hicho kukagua namna walengwa wa Mpango huo wanavyonufaika na mpango huo.

 Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa , Venance Mwamamoto, Waziri Kairuki na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini katika kijiji cha Mlanda , wilaya ya Iringa Vijijini wakati kamati hiyo ilipofanya ziara kijijini hapo kuona namna walengwa wa Mpango huo unaotekelezwa na TASAF wanavyonufaika na ruzuku itolewayo kupitia mfumo wa Uhawilishaji fedha. 



Wajumbe wa kamati ya Kudumu ya bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa wakilakiwa kwa shangwe na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii,TASAF,katika kijiji cha Mlanda wilaya ya Iringa mkoani Iringa kuona namna walengwa hao wanavyonufaika na fedha za Mpango huo.

No comments: