Na mwandishi wetu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe Angellah Kairuki amesema kwamba
serikali itahakikisha kwamba Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC) tawi la Mbeya
kinakuwa na majengo yake ili kupunguza gharama za uendeshaji.
Kwa sasa chuo hicho kinatumia majengo ya
kukodi ambayo ni mali ya Halmashauri ya Jiji la Mbeya,majengo hayo yapo eneo la
soko Matola, Chuo kinahudumia wakazi wa
Nyanda za Juu Kusini.
Akiwasilisha taarifa ya Chuo cha Utumishi wa
Umma Tanzania tawi la Mbeya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge Utawala na
Serikali za Mitaa Waziri Kairuki alisema gharama ya kodi ya shilingi
milioni 24 kwa mwezi ni kubwa na kwamba serikali iko katika mchakato wa
kuhakikisha kwamba chuo hicho kinamilikishwa mjengo hayo ili kupunguza gharama
za uendeshaji.
Aidha Waziri
huyo alisema kwamba serikali itahakikisha kwamba chuo kinakuwa na wakufunzi wa
kutosha ili kuendesha kozi zake kwa ufanisi.
Mkuu wa TPSC Dk.Henry Mambo aliiambia kamati
hiyo kuwa tawi la Mbeya linakua kwa kasi kwani kwa sasa lina wanafunzi 1236,
tawi hilo lilizinduliwa mwaka 2014 likiwa na wanafunzi 453.
“Tawi linakuwa kwa kasi na sisi kama chuo
tunaziona changamoto za kukua kwa chuo na tunajitahidi kukabiliana nazo, baadhi
ya changamoto hizo ni mahitaji ya miundombinu ya kufundishia,”
Alisema pamoja na changamoto hizo, serikali
imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba chuo kinafanya kazi zake kwa
ufanisi na kutoa elimu kwa watumishi wa umma na watumishi wa umma wa tarajiwa.
Naye Mwenyekiti
wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge Utawala na Serikali za Mitaa Josson Rweikiza
alikipongeza chuo hicho na kusema kuwa kina mchango mkubwa kwa maendeleo ta
taifa hili.
“Changamoto ni muhimu
katika uhai wa kila kitu, kama hakuna changamoto basi hakuna maisha,
tunawapongeza na kuwatia moyo katika kutekeleza majukumu yenu,” alisema.
Awali Waziri Kairuki alisema kuwa TPSC
hutoa ushauri wa kitaalam kwa Wizara, Idara, Wakala za Serikali , Mamlaka za Serikali
za Mitaa na sekta binafsi.
Baadhi ya shauri hizo za kitaalam ni katika
maeneo ya miundo na mifumo ya utumishi , mpango mkakati ,Mkataba wa huduma kwa
mteja , tathmini na uchambuzi kazi , tathmini ya utoaji huduma katika utumishi
wa umma na usimamizi wa mchakato wa ajira.
Waziri aliyataja baadhi ya majukumu ya Chuo
kuwa ni kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watumishi wa wa umma ili kuwajengea
uwezo katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Mafunzo hayo ni katika Nyanja
mbalimbali zikiwemo menejimenti ya usimamizi na rasilimali watu, menejimenti,
uongozi na utawala, utunzaji wa kumbukumbu na usimamizi wa fedha .
Pia kinatoa mafunzo ya muda mrefu katika ngazi
ya cheti na stashahada katika maeneo ya menejimenti na utawala, utunzaji wa
kumbukumbu na uendeshaji wa ofisi, mafunzo ya uhazili,usimamizi wa fedha
za umma , ununuzi na ugavi,huduma za maktaba utawala wa serikali za mitaa,
sheria na teknolojia ya habari na mawasiliano.
Chuo kina matawi sita mbayo ni Dar es Salaam,
Mtwara, Tabora, Singida Tanga na Mbeya.
No comments:
Post a Comment