Baadhi ya watu nchini kwetu Tanzania na nchi za jirani, wamekuwa wakichanganya maana ya neno utandawazi na neno mtandao. Baadhi yao, ambao waliosikika huwa wanazungumzia jambo lenye mantiki ya utandawazi lakini wakitumia jina la mtandao.
Ningependa kuchukua fursa hii kutoa mchango wangu kwenye mada ya ‘utandawazi’ na iwe kama ni mchango wangu kwa taifa na kwa Watanzania wenzangu kwa ujumla.
Kabla ya kuanza kuelezea maana ya utandawazi, ningependa kujitambulisha kuwa mimi siyo mwanaharakati, bali mimi ni mzalendo wa nchi yangu na naamini kuwa mchango wangu wowote mdogo ninaoutoa kwa ajili ya maendeleo ya nchi yangu utaleta mabadiliko kwa kiasi fulani kwa kutumia makala zangu kwa faida ya jamii au kwa taifa kama siyo dunia kwa ujumla. Lakini lengo langu katika makala hii ni kuangaza nchini kwetu Tanzania tu na kutolea mfano baadhi ya mataifa mengine ambayo ni rafiki na Tanzania juu ya suala la uchumi wa utandawazi.
Utandawazi (Globalisation) ni nini? Utandawazi ni hali ya muingiliano wa kifikra au kimatendo baina ya nchi moja na nchi nyingine, au baina ya mtu mmoja na mtu mwingine ambao wapo nchi tofauti. Kawaida muingiliano huu, unakuwa ni muingiliano wa kiuchumi au kisiasa au kiutamaduni, na katika muingiliano huu, si lazima nchi moja ifaidike zaidi ya nchi nyingine.
Sasa tujiulize, je, nadharia hii ni mbaya? Jibu ni ndiyo na hapana! Kwasababu utandawazi una faida zake na una hasara zake kwa taifa huru kama taifa letu la Tanzania, lakini mara nyingi ukiangalia hasara zake ni kubwa na zinapotoweka zinakuwa ni hasara zisizoweza kurejeleka, iwapo utandawazi utatanda kwa miaka mingi katika taifa na hususan ukitanda kwenye kila ngazi ya taifa.
Baadhi ya sababu hizo nilizielezea juu juu katika makala yangu (2013) niliyogusia utandawazi, lakini sikuuelezea kwa kina sana (2013, Nini kinachofuata baada ya katiba mpya?).
BAADHI YA FAIDA NA HASARA ZA UTANDAWAZI (GLOBALISATION)
Zifuatazo, ni baadhi ya faida na hasara za utandawazi. Lakini katika makala hii sitozielezea zote kwa kina, bali nitagusia baadhi tu ya maeneo ambayo kwa sasa yanatugusa katika taifa letu.
Baadhi ya Faida:
- Ajira kwa wananchi wa hali ya chini kabisa.
- Kubadilishana utamaduni unaofaa jamii.
- Bei nafuu za usafiri wa mbali.
- Uwekezaji.
- Kubadilishana mawazo ya kisiasa kwa manufaa ya nchi bila ya kuathiri misingi iliyojengwa ya nchi huru.
Baadhi ya Hasara:
- Kupotea kwa uhuru wa serikali kujiongoza yenyewe kutokana na misingi yake ya kitaifa.
- Upitishaji wa madawa ya kulevya, ujangili na uhamiaji haramu kuongezeka.
- Kupotea kwa utamaduni wa taifa.
- Kupotea kwa mapato ya taifa.
- Kuongezeka kwa mapatao ya aliyekuwa nacho, na kuzidi kupungua kwa mapato ya asiyekuwa nacho (Mtu maskini kuendelea kuwa maskini).
- Misaada kwa masharti yasiyoendana na maadili na utamaduni wa taifa huru.
- Mtikisiko wa kiuchumi wa kidunia.
- Na mengineyo mengi.
UTANDAWAZI WA UCHUMI NCHINI TANZANIA
Kwanza kabisa nitoe pongezi za dhati kwa rais wetu, Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya ya ari na ya kizalendo na timu yake ya awamu ya tano, katika kulichukua taifa letu kwenye uchumi wa viwanda na kuwakwamua wananchi kiuchumi na mpaka kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Naamini kwamba, kwa kasi aliyoanza nayo rais wetu wa awamu ya tano na kwa mpango maalum, naamini kabisa kuna matarajio makubwa ya Tanzania kufikia malengo yaliyowekwa.
Ningependa kutoa mchango wangu kwenye suala la uchumi katika dunia hii ya leo ya utandawazi na ningependa nianze kwa masuali matatu ambayo yanalenga tija na dira ya maendeleo ya nchi yetu, ili masuali haya yawe kama ni hamasa ya makala yangu.
Masuali matatu kama yafuatavyo:
- Hivi sasa tupo njiani katika kujikwamua kiuchumi, lakini je, tutayafikia malengo tarajiwa?
- Je, ifikapo mwaka 2025 tutakuwa tumefikia mapato ya kiwango cha kati, na taifa kama ‘taifa’ vilevile litafikia kuwa taifa tajiri (bila ya kutegemea misaada ya nje) kwa wakati mmoja?
- Au taifa litaendelea kuwa maskini na wananchi wataendelea kuwa bado maskini hata ifikapo mwaka 2025 au kupita mwaka 2025 na kusababisha tofauti kati ya aliyekuwa nacho na asiyekuwa nacho kuongezeka?
Jinsi utandawazi unavyofanya kazi hii leo, ni kwamba watu wa nchi moja hususan nchi tajiri huwekeza kwenye nchi yenye watu wengi maskini kama Tanzania, ili waweze kuzalisha bidhaa kwa wingi na kuwalipa mishahara kwa malipo ya chini kabisa kwa watu maskini wakiwa kama wafanyakazi, kwa kuwatumia wafanyakazi hao kwa kuzalisha asilimia kubwa ya uzalishaji wa bidhaa hizo, ili zikauzwe nje ya nchi kwa bei watakayoipanga wao kutokana na walengwa wa soko lao.
Sababu mojawapo inayopelekea nchi tajiri kufanya hivi ni kwamba baadhi ya nchi kiwango cha maisha cha wananchi wao ni kikubwa ambacho kwamba ikiwa watazalisha bidhaa hizo ndani ya nchi zao watalipa pesa nyingi za mishahara kwa wafanyakazi wanaozalisha bidhaa hizo na mwishowe bidhaa hizo zikifika sokoni zitafika kuuzwa kwa bei kubwa ambayo watu watashindwa kununua na watakosa soko la kuuza na watakosa faida.
Hivi sasa, nchi ambazo wao na wananchi wao wameshafikia kipato cha kiwango cha kati na asilimia ya wananchi wao inazidi kupanda kufikia kiwango cha kipato cha kati, wanakuwa hawana budi ila kutafuta uzalishaji huo nchi nyingine za kimaskini ambazo wataweza kupata wafanyakazi wa kuwalipa mishahara ya chini kabisa, kwa wafanyakazi ambao watakaoweza kuzalisha asilimia kubwa ya uzalishaji ili waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi kwa bei nafuu au kwa bei ya juu inategemea na walengwa wa soko lao.
Bidhaa hizi zinapozalishwa ndani ya nchi maskini halafu kuuzwa nje ya nchi, maana yake wananchi wa hali ya chini wataendelea kulipwa mshahara wa chini, na wataendelea umaskini ule wa kutokukidhi haja za maisha yao ya kila siku, kwa mfano chakula bora, kusomesha watoto wao, kupata afya bora na kuishi kwenye mazingira mazuri. Lakini muwekezaji ataondoka na faida kubwa kuliko mzigo atakaoachiwa nao serikali, na mwisho wa siku pesa ile ile anayoipata serikali inarudi tena kumhudumia maskini huyo huyo, na mzunguko unaendelea kuwa hapo hapo, nchi maskini na watu wake maskini na kunakuwa hakuna ‘reserve’ au pesa ya akiba kwa serikali ya kuleta maendeleo ya nchi na kwa wananchi wake.
Je, uwekezaji wa uchumi wa utandawazi wa namna hii ni mbaya? Uwekezaji wa utandawazi wa namna hii si mbaya na si mzuri. Kwasababu nchi zote mbili zinafaidika lakini kuna matarajio makubwa ya nchi moja kutofaidika na uchumi wa utandawazi wa namna hii kwa mfano mmoja wapo niliyo uainisha hapo juu na mifano mingine mingi.
Ikiwa tumeona kwamba, kuna uwezekano wa nchi maskini kutoka bila ya kufaidika na rasilimali zake kupitia uchumi wa utandawazi, basi ipo haja ya kuangalia mfumo mpya wa utandawazi kwa wawekezeji wa nje, na wakati huo huo tuangalie athari za wawekezaji wa ndani kwa wananchi na serikali katika dunia hii ya utandawazi.
Tumeshaona mchango wa wawekezaji wa nje na faida zake, lakini pia inatupasa tuangalie mchango wa wawekezaji wa ndani na faida zake. Uwekezaji wa ndani una mchango mkubwa sana kwa serikali na wananchi wake kwa ujumla. Tuangalie mfano wa wawekezaji wa ndani wenye viwanda vya ndani, ambavyo vinasemekana vinazalisha bidhaa zenye viwango zenye kutumika ndani, na vyenye kumilikiwa na wananchi wa ndani, na faida zake zinaendelea kuekezwa maeneo mbalimbali ya ndani, na kutoa ajira kwa wananchi wa ndani. Matokeo yake ni kwamba viwanda hivi bidhaa zake zitauzwa ndani, na wananchi wa hali ya chini kabisa wataweza kuzinunua bidhaa hizohizo za ndani na kuwawezesha kukidhi haja zao za msingi za kila siku.
Bidhaa za ndani asili yake ni bidhaa za bei nafuu na si za kuuzwa kwa bei ya juu hata mtu wa chini akashindwa kununua (inategemea na soko). Uuzwaji huo wa bei ya juu kwa viwanda vya ndani huwa unaongeza umaskini kwa wananchi, kwasababu wananchi wengi ni wenye vipato vya chini na wanashindwa kununua bidhaa zenye kukidhi haja zao za kila siku kwasababu ya bei. Lakini tumeona viwanda vingi sana vya ndani vimeonesha jitihada zao katika kuweka bidhaa zao bei ya chini kabisa.
Lakini kwenda mbali zaidi, ikiwa viwanda vya ndani vitaweza kuzalisha bidhaa zenye viwango vya juu kwa kutumia maliasili ya ndani na rasilimali za ndani na wakati huo huo kushusha bei chini zaidi kwa kukidhi hali ya maskini wa hali ya chini kabisa kwa malengo ya kugusa soko kwenye kila kona ya taifa na kuwapa faraja wananchi, viwanda vitapata faida ya kufikia ‘margin’ kubwa ya faida yao kwa mwaka, na wakati huo huo, wananchi wa hali ya chini kabisa watapata uafueni wa kimaisha na hatimaye kuisaidia serikali kwenye maeneo mengine ya ustawi wa jamii na maendeleo ya wananchi kwa ujumla na kuwatoa wananchi kwenye umaskini. Mfumo huu ningependa kuuita ‘utandawazi wa ndani’ na ni mfumo ningeupendekeza kwa nchi yetu ya Tanzania kwa sasa.
Kuna msemo mmoja wa Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Roosevelt, alisema:
“The test of our progress is not whether we add more to the abundance of those who have much; it is whether we provide enough for those who have too little.”
Haimaanishi kuwa tuzuie watu wa nchi za nje au wa mataifa mingine wasije kuwekeza nchini, hapana, kila mtu akaribishwe lakini kwa kufuata sheria itakayoweza kunufaisha wananchi wa Tanzania na taifa kwa ujumla kwanza. Kwasababu tumeona nchi mbalimbali za jirani na za mbali ambazo ni nchi rafiki na Tanzania zimeekeza kwa muda mrefu na tumeona faida zake kwa wananchi kupata kufaidika kwa uwekezaji huo kwa njia moja au nyingine.
Nchi rafiki na Tanzania kama nchi ya Uingereza, China, Marekani, Ujerumani, Japan, Ufaransa, Uholanzi, Canada na nchi za Arabuni na nyingine nyingi za mbali na za karibu duniani tumeona matunda ya uwekezaji wao nchini kwa wananchi wetu na tumeona faida zao nje ya nchi kwa ukarimu wao kwenye jukwaa la dunia na wamesaidia sana. Kwahiyo, wawekezaji wote wanakaribishwa lakini serikali itazame mfumo maalum wa kunufaisha wananchi na wakati huo huo kujipatia mapato yake.
Mtazamo huu wa uwekezaji wa ndani, wanauchumi wanauita “Protectionism”. Ni tofauti na mfumo nilioupendekeza wa ‘utandawazi wa ndani’, kwasababu ‘protectionism’ wakati mwingine ni mfumo ambao haujali sana watu wa hali ya chini, lakini unajali maslahi ya taifa husika. Kwa maana ya kwamba nchi inalinda viwanda vyake vya ndani na kutoza ushuru mkubwa bidhaa zinazoingizwa nchini. Ni mtazamo ambao hata rais wa Marekani wa sasa, Mheshimiwa Donald Trump, akiwa kama tajiri bilionea, na akiwa kama mmoja wa wafanyabiashara wakubwa duniani, anaona ni mtazamo mzuri kwa maslahi ya nchi yake kwa kutumia kauli mbiyu ya “America first, America first” kwa madai kuwa, utandawazi tangu uwanze karne iliyopita, haukuleta mafanikio mengi duniani kwa wananchi bali umezidisha umasikini na matajiri wamezidi kutajirika.
Wakati huo huo, rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping katika hotuba yake ya kihistoria aliyoitoa mjini Davos, Switzerland, tarehe 17 Januari mwaka 2017, amepinga Protectionism kwa madai kwamba, utandawazi wa kiuchumi hauna matatizo kimataifa iwapo nchi tajiri zinazowekeza nchi maskini zitawasaidia watu wa hali ya chini katika ngazi ya jamii ili kuleta manufaa ya utandawazi kwa watu wote wa ngazi zote.
Nilivyofahamu mimi nadharia ya Mheshimiwa Xi Jinping, ni kuwekeza kiuchumi katika nchi maskini (kama Tanzania) na bila ya kuingilia siasa za nchi huru (sovereign countries) na bila ya kuingilia utamaduni wao, bali ni kufanya biashara kiutandawazi kiuchumi tu. Hii ni nadharia nzuri sana ya Mheshimiwa Rais Xi Jinping. Lakini suali linakuja vipi watu wa ngazi zote za jamii wanaweza kufaidika kiutandawazi bila ya kuathiri utamaduni wao na bila ya kuathiri nguvu ya serikali katika siasa zake kwa wananchi wake? Na misaada hiyo itatolewa kwa urefu wa muda gani?
Wasiwasi wangu kwa kuiangalia nadharia hii ni kwamba, kusaidiwa huku lazima kutakuja kwa masharti ya aina moja au nyingine, kama siyo kutoka kwa nchi moja basi yatatoka nchi nyingine ambayo masharti hayo yanaweza kupelekea kuathirika kwa utamaduni wa taifa na serikali ikajikuta haina nguvu ya kufanya chochote kwasababu ya kutegemea misaada ya nje kwa masharti. Kwasababu China, kwa mfano, wanaweza kutupa misaada bila ya masharti yoyote kama rafiki zetu, lakini nchi nyingine ingawa ni marafiki, lakini isikubali kutoa msaada bila ya masharti.
Kwa mfano mwingine tuchukulie masharti au bila ya masharti, wanaweza kuja madaktari wa kutoka nchi mbalimbali kwa kutoa huduma za mpito. Matarajio yetu ni kwamba, msaada wa namna hii ni msaada wa kibinaadamu na si msaada wa kimpito. Ikiwa unatoa msaada ili uweze kuchukua au kupata kitu kutoka kwa mwingine, huu siyo msaada, huku ni kutoa kwa sababu ya maslahi na malengo binafsi.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Uingereza, Mheshimiwa Theresa May katika hotuba yake mjini Philladelphia, Marekani, tarehe 26 Januari 2017 alisema,
“The days of Britain and America intervening in sovereign countries in an attempt to remake the world in our own image are over.”
Kwa maana ya kwamba Uingereza na Marekani haitoingilia siasa (na utamaduni) wa nchi huru yoyote wakati wa kuitangaza Global Britain. Hii ni bishara nzuri kwa kufanya biashara na nchi nyingine duniani bila ya kuingilia utamaduni au siasa ya ndani ya nchi nyingine lakini wakati huo huo kufaidika kiuchumi.
Wakati huo huo, Rais wa Marekani wa sasa, Mheshimiwa Donald Trump katika hotuba yake siku ya kutawazwa kwake kuwa rais wa 45 wa Marekani tarehe 20 Januari 2017, wakati aliyoitangaza America First alisema,
“We will follow two simple rules, buy American and hire American. We will seek friendship and goodwill with the nations of the world, but we do so with the understanding that it is the right of all nations to put their own interest first. We do not seek to impose our way of life on any one, but rather to let it shine as an example, we will shine.”
Kwa maana ya kwamba Marekani hatoingilia utamaduni au siasa ya ndani ya nchi huru wakati wa kuitangaza America First. Hii ni bishara nzuri kwa kufanya biashara na nchi nyingine duniani bila ya kuingilia utamaduni au siasa yake ya ndani na wakati huo huo kufaidika kiuchumi.
Mifano niliyoielezea hapo juu ni kutaka kujenga hoja ya mada yangu hususan athari za utandawazi na Tanzania. Haimaanishi kuwa tunataka kuvunja urafiki baina ya Tanzania na Marekani, au baina ya Tanzania na China, au baina ya Tanzania na Uingereza, au baina ya Tanzania na nchi zote rafiki na Tanzania. Urafiki ulikuwepo wa nchi rafiki na Tanzania, urafiki upo na urafiki utaendelea kuwepo kwa maslahi ya nchi zote. Lakini nakusudia Tanzania itafanya vizuri zaidi katika kuimarisha uchumi wake na wakati huo huo kulinda amani, utamaduni na utulivu wa nchi yake na siasa zake za ndani ya nchi, iwapo nadharia ya Mheshimiwa Xi Jinping, Theresa May na Donald Trump ya kutafsiri utandawazi mzuri ni ule utandawazi wa kiuchumi na si utandawazi wa kuingilia utamaduni au siasa za nchi nyingine kwenye dunia hii ya leo. Na hii ndiyo aina ya utandawazi inayofaa kwa nchi yetu ya Tanzania.
Nchi nyingi za kimasikini duniani zinapiga vita utandawazi kutokana na kuathirika kwa utamaduni wao na siasa ya nchi zao. Madamu viongozi wa nchi tajiri katika dunia hii ya leo wameliona hilo, kwamba upo uwezekano wa mataifa kushirikiana kiuchumi bila ya kuathiri misingi muhimu ya taifa katika dunia ya utandawazi, pengine kuna mwanzo mzuri huko tunapoenda.
Kwa kuongezea na kusisitiza, misaada ya kupewa kwa masharti kwa njia ya utandawazi na utandawazi wa kisiasa na wa kiutamaduni una athari kubwa sana katika utamaduni wa taifa na siasa na serikali yake na hata kupelekea kwa nchi huru kama nchi ya Tanzania kukosa uhuru wake kujiendesha yenyewe.
Kwa ujumla, nadharia ya kusaidia watu wa hali ya chini ya Mheshimiwa Xi Jinping kwa kupitia utandawazi wa uchumi ni nzuri, lakini isiwe misaada ya kusaidia jamii kwa masharti, ambayo ikiwa nadharia hiyo haitotumika kimaslahi (pengine) ni nadharia ambayo pia kwa upande mmoja au mwingine inaowana na nadharia ya Mheshimiwa Donald Trump na Theresa May ya kutokuingilia siasa za nchi huru kiutamaduni na siasa zake za ndani.
Mwisho ningependa kushauri, suluhisho la tatizo la kiuchumi kwetu sisi na vizazi vyetu kwa sasa ni katika kuangalia mambo yafuatayo:
- Tanzania iendelee kumsaidia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli katika maendeleo ya nchi na katika kujenga uchumi wa kujitegemea kama taifa. Taifa likiweza kujitegemea lenyewe kiuchumi na kuwa nchi tajiri linaweza kutoa mchango mkubwa kimataifa na kusaidia nchi maskini na wakati huo huo kulinda maslahi na misingi ya taifa lake.
- Tuna sababu nyingi ya kusoma kwa hawa rafiki zetu wa miaka mingi wa China jinsi gani waliweza kuitoa nchi yao kuwa nchi maskini na mpaka kufikia kuwa nchi tajiri duniani na wananchi wake kufikia kiwango cha kipato cha kati. Lakini kwa ufupi tu ningesema kwamba China ilichukua muda kubainisha nini chachu ya maendeleo, na katika kubaini kwao wakaekeza elimu katika sekta zote na wakawa wakali na viongozi wao kupambana na rushwa na kulinda misingi ya kisiasa ya nchi yao (principles) kabla hawajafungua mlango kwa mataifa ya nje kwenye utandawazi.
Uzuri wa kufanya kama walivyofanya China ni kwamba, pale tunapofungua milango tuwe tupo tayari kama nchi huru kwa maana tuwe tumeshaimarisha misingi inayosimamisha uhuru (sovereign) wa nchi ili tunapofungua milango kwa mataifa mingine, nchi haitoyumba kutokana na misingi imara iliyosimamishwa chini ya serikali na chini ya chama tawala ili taifa lisiyumbe. Na hivi ndivyo walivyofanya China.
Ni muhimu sisi tuangalie tulipo na tuone tumefaidika na nini. Kilichotusaidia sisi kufungua milango yetu mapema ni kwamba tunaweza kujenga hoja kuwa tulikuwa nyuma sana na tulihitaji kiki angalau tufike hapa tulipofikia. Kwa maana nyingine, ruhsa imetusaidia kusukuma maendeleo ya nchi yetu.
Kila nyakati ina mikakati yake ya kufikia malengo tarajiwa, na mikakati iliyofanywa wakati wa uhuru na miaka ya 70 na 80 kwa hekima za baba wa taifa, ilikuwa ni mikakati muwafaka kwa wakati ule kwa malengo ya kujenga umoja wa kitaifa wa Tanzania. Baba wa taifa alivyosema, wakati wenzetu wanatembea sisi tuwe tunakimbia, ni kwasababu alichuja nchi za wenzetu zilipofikia, na nchi yetu ilipo ni lazima tukimbie ili tuweze kuwafikia wenzetu kimaendeleo. Kama nilivyosema kwenye makala yangu (2015) kwamba, maendeleo hayaji kwa usiku mmoja, lakini kiki ya ruhsa imesaidia.
Baba wa taifa, Julius Kambarage Nyerere, alisema itafika wakati lazima tubadilike ‘kifikra’. Wakati ni sasa, ni kwa kuwaandaa wananchi wote wazawa kielimu kwanza bila ya kuangalia dini zao au makabila yao kwa kuimarisha misingi ya umoja wa kitaifa, miundombinu ya usafiri na uhamiaji, na umoja na mshikamano ili taifa liendelee kuwa na amani, na kadhalika, kabla hatujafungua zaidi milango mingine ya utandawazi ili tusije kutawaliwa na hali ya huku tunajiona kuwa tupo huru, na matokeo yake watakaofaidika watakuwa ni wachache kuliko wengi kwasababu watu wetu wengi wao hawapo tayari kukabiliana na mabadiliko yanayotokea duniani kwa kasi kubwa katika dunia hii ya leo. Lazima tubadilike kifikra, hizi ni zama nyingine. Na tumeona bidii za Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alivyoingia kwa kishindo cha kuweka elimu kipaumbele kwa kutimiza ilani ya chama tawala ya kutoa elimu bure kwa watoto wote wa Tanzania kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari. Hili ni jambo la kupongezwa.
Katika kutimiza azma hiyo, ushauri wangu ni kwamba:
- Katika ujenzi wa viwanda, viwanda vingi ambavyo tunavipigania hivi sasa ni viwanda vya nguvu kazi (manual) wakati wenzetu wanatengeneza viwanda vya 3D vya teknolojia ya kisasa. Maaana yake kilichokosekana kwetu ni teknolojia. Kwahiyo nampongeza Rais Magufuli kwa hatua zake anazozichukua kwasababu kila kitu kina mwanzo na ninaamini kwa kasi yake tutafika huko. Na nampongeza Mheshimiwa Joyce Ndalichako kwa kuwasimamia kidedea bodi ya VETA kuwezesha kutotoa wataalamu na wabunifu wa maendeleo ya viwanda kwa ujumla.
- Kutengeneza, kubuni na kusimamia viwanda vinahitaji elimu. Waalimu wetu wengi wao hawana elimu ya teknolojia ya kuweza kututoa hapa tulipo kwenye elimu ya vibonyezo vya tarakimu (digital), elimu ya anga, na kadhalika. Ushauri wangu ni kwamba, wakusanywe baadhi ya wanafunzi wa elimu ya juu waliofanya vizuri bila ya kuangalia makabila yao au dini zao au kanda zao, ili wapelekwe nchi kama China au nchi yoyote kusoma teknolojia za viwanda ili waweze kujua vipi wenzetu walifikia hapo walipofikia ili na sisi tuweze kutoka. Katika zama hii ya leo, laana kubwa itatupata ya kimaendeleo nchini kwetu Tanzania kwa miaka mingi ijayo, kama siyo milele, ni laana ya kukandamiza elimu kikanda, kidini au kikabila. Badala yake tuhamasishe na tuwape fursa watoto wote wa Kitanzania kielimu na hatimaye kuangalia uwezo wao badala ya kanda zao, dini zao au kabila zao, kwa kuwapa zana zote stahiki za kuwafikisha wanapotaka kufika. Najua dhana hii haipo, lakini ni ushauri na nasaha kwa kizazi chetu na kizazi kijacho.
- Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli aendelee kuzuia wananchi wa hali ya chini kabisa wasitozwe kodi kama alivyotangaza kuhusu wakulima wadogo wadogo sana na hali kadhalika wasitozwe kodi, kwasababu hii ni njia moja wapo ya kuchochea uchumi wa nchi na kuwapa wananchi wa hali ya chini maisha mazuri na kujiinua kiuchumi. Nchi nyingi duniani, huchukua hatua hizi kama alizozichukuwa mheshimiwa rais kwa kuachia maeneo fulani fulani kutokutoza kodi, siyo kwasababu hawazioni, bali ni kwa makusudi ya kwamba maeneo hayo ni vyanzo vya kuchochea uchumi wa taifa na wakati huo huo ni manufaa kwa wananchi.
- Tanzania iendelee kukaribisha wawekezaji nchini kwa mfumo maalum wa kusaidia wananchi wa hali ya chini na kuvitawanya viwanda vya wawekezaji katika maeneo na mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa kugawa ajira. Kwa kuzingatia pia muwekezaji anapata faida yake katika uwekezaji wake, lakini pia wafanyakazi na wananchi kwa ujumla wanafaidika katika uchumi wa viwanda.
- Serikali na chombo chake cha TIC, lazima kitafakari upya katika uwekezaji na kuhakikisha kwamba kuna sheria maalum za kuweka maslahi ya wananchi wazawa na taifa kwanza. Kwa kuongezea mantiki hii, ningependa kuweka wazi kwamba, hakuna mzawa aliye ndani ya nchi au nje ya nchi atakayependelea kuhudumiwa kwa kupata huduma nchini mwake kwa kuwekewa vigezo sawa kama mgeni ambaye si mzawa. TIC iwe ya wawekezaji wageni kama ‘wageni’. Na mfumo wa chombo kipya uwekwe kwa jicho la huruma kupitia bunge tukufu kwa wazawa waliopo ndani na nje ya nchi mfumo wa kuwapa huduma katika kuijenga nchi yao kwa manufaa ya wazee wao, vizazi vyao, ndugu zao, jirani zao, marafiki zao na Watanzania wenzao kwa ujumla kwa kufuata sheria, kanuni za serikali na kuheshimu viongozi wa taifa. Serikali siku zote ina nguvu!
Sina shaka kwamba awamu zote zilizopita zilizingatia hii misingi, lakini ni wajibu wetu kwa sasa kuangalia hapa tulipo na tunapoelekea kama taifa moja la Watanzania.
Mwisho ningependa kugusia hasara ya uchumi ya utandawazi kwenye mfumo wa kipesa duniani na athari zake zilizo wazi. Nisingependa sana kufananisha umoja wa nchi za Ulaya, EU (European Union), na umoja wa nchi za Afrika Mashariki, EAC (East African Community). Lakini kuna elements ambazo ningependa ziangaliwe kutokana na mifano iliyotokea hivi karibuni kutokana na utandawazi, hususan kwenye mfumo wa kipesa.
Mfumo wa kipesa na mapinduzi ya utandawazi yaliopo hivi sasa ulijaribiwa mwaka 2008 wakati ulipotokea mtikisiko wa kiuchumi duniani (financial crisis). Nchi nyingi ziliathirika kwasababu mfumo wake wa muingiliano wa kipesa unategemeana, nchi-kwa-nchi. Ndiyo maana hata nchi za Ulaya (EU) zilipata mtikisiko wa namna hiyo na kusababisha nchi nyingi zilizoshikana za Ulaya kwa mfano Ugiriki, Hispania na Italia na nyinginezo kwenda chini kiuchumi na mpaka hii leo zinataabika kurudisha uchumi wake lakini inashindikana kwa njia moja au nyingine. Vilevile tunaanza kuona mshike-mshike wa mtazamo wa kiuchumi wa nchi za Ulaya, baada ya Uingereza kutangaza kujitoa kwenye umoja wa nchi za Ulaya (Brexit).
Kwahiyo, tunasoma kwamba nchi zenye umoja zenye kushirikiana kipesa na kiuchumi hatari yake ni kwamba nchi moja ikienda chini kwa njia moja au nyingine, nchi zote zinadidimia na zinausikia mtikisiko huo na hitamaye zote kuangukiana.
Kwa ushirikiano wa kimataifa kwenye dunia hii ya utandawazi, nataraji nchi tajiri zilizoendelea zitatafakari njia nzuri yenye kuwafaidisha, lakini bila ya kuathiri mtikisiko katika nchi nyingine mara tu pale unapotokea mtikisiko wa kiuchumi.
Kwa ufupi, tumeona faida ya Watanzania kuwa na elimu ya kutosha, tumeona faida ya kuwa na miundombinu ya kutosha, tumeona faida ya viwanda vya ndani, tumeona faida ya uwekezaji wa ndani na faida za wananchi wa hali ya chini na wawekezaji kwa ujumla. Tumeona baadhi ya faida na baadhi ya hasara za utandawazi kwa ujumla na nataraji mchango wangu utasaidia njia moja au nyingine katika kuleta maendeleo ya nchi na wananchi wote kwa ujumla.
Huu ni mchango wangu na ushauri wangu katika uchumi wa Tanzania kwenye dunia ya utandawazi.
Samahani kama nimekosea popote.
Ndugu yenu,
Saleh Jaber
07/03/2017
MAREJEO:
Jinping, X. (2017) Davos, Switzerland:
May, T. (2017) Philadelphia, USA:
Trump, D. (2017) Washington, D.C., USA:
Source: https://sjposters.wordpress. com
No comments:
Post a Comment