Monday, March 6, 2017

HATUTAKUBALI TLS KUJIINGIZA KATIKA SIASA-MWAKYEMBE

Waziri wa Mambo ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt Harrisson Mwakyembe amesema Serikali haiwezi kuona Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kinajiingiza katika siasa na kama TLS wanataka hivyo, basi Serikali haitasita kuifuta Sheria ya TLS Sura ya 307 iliyoanzisha chama hicho cha Wanasheria.

Amesema kuwaingiza wanachama ambao wana nasaba za siasa au viongozi wa vyama vya siasa ndani ya TLS ni kuruhusu mgongano wa maslahi na yeye kama mwanasheria hawezi kulikubali jambo hilo. DKt Mwakyembe alikuwa akizungumza hayo na ugeni wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) uliokuja kumtembelea Ofisini kwake mjini Dodoma ukiongozwa na Rais wao Bw. John Seka

“Kama Wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa Sheria yenu iko chini yetu, mkiharibu kwa lolote Wizara ndio yenye wajibu wa kuwatolea maelezo, katika hilo mnalotaka kulifanya sasa kuna mgongano wa maslahi, je nyinyi kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?, alisema Mhe Mwakyembe.

Alisema Serikali haina shida na wanachama wa TLS kuwa wanachama wa vyama vya siasa ila ni lazima wafahamu kwamba viongozi wanaowachagua ambao ndio watakaobeba sura ya TLS na mwelekeo mzima wa chama kama wanataaluma hawapaswi kuwa na nasaba za kisiasa ili kuepusha mgongano wa maslahi unapoweza kujitokeza.

“Serikali haina shida na wanachama wa TLS kuwa wanachama wa vyama vya siasa ila tatizo linakuja pale mnapotaka kuchagua viongozi ambao tayari wanazo kofia mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa, hao ndio watakaobeba sura na mtazamo au mwelekeo wenu hapo hatuwezi kukubali kwa kuwa watatenganishaje uongozi wao katika chama husika na uongozi wao ndani ya TLS, huo sasa ndio mgongano wa maslahi alisema Dkt. Mwakyembe na kuongeza kuwa ndio maana mwanasheria yoyote akiingia katika utumishi wa umma uwakili wa kujitegemea anauweka pembeni ili kuepuka mgongano wa maslahi.”
Alisema TLS sasa imekuwa na haihitaji muangalizi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma nchi ilipopata uhuru, kwani ina wasomi wengi na vijana wengi wamekuwa wanachama pia na kwa hiyo ni bora tuifute hii Sheria yenu na tuwape mwanya mkajisajili kama NGO ambako kiongozi yeyote wa chama cha siasa anaweza kuwa kiongozi wao.

Amewataka wafahamu kuwa dhamira ya Serikali ni njema huku ikizingatiwa kwamba Sheria kama zilizvyo taaluma nyingine nchini bado zinahitaji uangalizi hasa ukizingatia uingiaji wa nchi katika utengamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Akizungumza katika kikao hicho Katibu Mkuu wa Wizara Prof. Sifuni Mchome alisema kila taaluma ina namna ya uangalizi wake. alisema kama wanasheria lazima kuhakikisha hatutoi vipaumbele kwa siasa kama zilivyo fani nyingine nchini. Alitaka wajiulize kama kweli hawauoni mgongano wa maslahi huku wakizingatia kuwa wanapaswa kuhudumia jamii ya watanzania bila ya kuwabagua.

“Kama wanasheria lazima tuhakikishe hatutoi vipaumbele kwa siasa kama zilivyo fani nyingine, jiulizeni kama kweli hamlioni jmabo hilo kama ni kikwazo huku mkizingatia kuwa tunatakiwa kuhudumia jamii bila ya kuwabagua sasa tukijiingiza katika siasa tutaihudumiaje jamii husika? TLS kutojihusisha na siasa ni miongoni mwa kanuni za kutuimarisha kama wanataaluma,”alisema Prof Mchome

Alisema Wizara ipo kuiangalia TLS, na ndicho ilichofanya, imewastua jamani mnaenda wapi? tunataka muende katika mstari sahihi, nawataka mjiulize hivi kweli kamati ya uchaguzi haijaona kama kuna mgongano wamaslahi hapo?

“Tupo hapa kuwangaalia, na ndicho tulichofanya, tumewashtua jamani mnanenda wapi? Hatuna nia mbaya ila tunawataka muwe katika mstari, hivi kweli kamati ya uchaguzi haijaona kama kuna mgongano wa maslahi hapo?

Alisema Serikali haitasita kuchukua hatua ya kuifuta Sheria ya TLS kama chama hicho kitaendelea na msimamo wa kujihusisha na masuala ya siasa au kiuharakati chama hicho katika siasa na hawana budi zaidi ya kuangalia namna wanavyoweza kujikwamua katika hilo.

Kama hamuwezi kuendeleza misingi ya kitaaluma ya kutojihusisha na siasa au vyama vya siasa basi serikali haitakuwa na namna zaidi ya kuifuta sheria ya TLS na TLS ya sasa itabidi ikajisajili kama NGO ili iendeleze harakati zake na Serikali itaunda sheria nyingine itakayoanzisha chombo kitakachosimamia misingi ya kitaaluma.

Naye Rais wa TLS bw. John Seka akizungumza katika kikao hicho alisema ameelewa maoni ya Serikali na kwamba kuonekama kwa TLS kama inajiingiza katika siasa kunatokana na wanachama ambao ni viongozi au wanachama katika vyama vya siasa ambao kwa sasa wanataka uongozi wa chama hicho.

Ameiahidi serikali kuwa TLS itaendelea kuzingatia kanuni na miongozo ya kuanzishwa kwake ambapo pia haina mpango wakuwa chama cha siasa au chama cha kiharakati na hivyo kuiomba Serikali kuifanyia marekesbisho Sheria yake ili iweze kukabili changamoto inazokabilian nazo kama ilivyotokea sasa ambapo mwanachama ni kiongozi wa chama cha siasa na hivyo kuwa na haki ya kuomba uongozi wa TLS

Amesema anaiomba wizara na watendaji wake kuendelea katika mazunguimzo na TLS ili kuweza kuhakikisha inatekeleza na kufikia malengo yote ya kuanzishwa kwake huku akiahidi kuwa siku zote TLS haitogwanyika, itasimamia na kuongoza wanachama wake ipasavyo na kuhakikisha misingi na maadili ya taaluma ya sheria inazingatiwa ili TLS iendelee kubaki kama ilivyo sasa na kutokupendelea upande wowote.

No comments: