Na Salum Vuai,
MAELEZO - Zanzibar
MAELEZO - Zanzibar
JUMATATU ya
tarehe 27 Machi, 2017, niliamua kuakhirisha mambo yangu mengine yaliyokuwemo
kwenye ratiba yangu na kuamua kufunga safari hadi mtaa wa Chumbuni, Wilaya ya
Mjini Unguja.
Nia yangu
ilikuwa kwenda kumjulia hali msanii mkongwe wa Zanzibar, Mzee Haji Gora Haji,
ambaye kwa miezi kadhaa sasa nyendo zake zimekatika kutokana na kusumbuliwa na
maradhi.
Gwiji huyu
wa sanaa mbalimbali ikiwemo ushairi, uandishi wa vitabu vya hadithi fupi, tenzi
na mashairi ya nyimbo, ni miongoni mwa watu muhimu katika tasnia ya usanii hapa
nchini.
Kwangu mimi,
na ninaamini kwa wengine wanaopenda sanaa, Mzee Gora aliyezaliwa mwaka 1933
kijijini Tumbatu, ni mwalimu na mlezi katika kuwafinyanga washairi chipukizi na
wa makamu ambao bado wanaendelea kujifunza kwa kuamini kwamba sanaa ni
utamaduni endelevu unaokuja kivyengine kadiri siku na mambo yanavyobadilika.
Ingawa
nilikuwa nikipanga kumtembelea siku nyengine isiyokuwa tarehe 27 Machi
niliyoitaja awali, lakini nililazimika kubadili mpango huo na kuamua kuwahisha
ziara yangu hiyo kutokana na jambo maalumu liliougusa mtima wangu usiku wa
Machi 26, mwaka huu.
Ni jambo
gani hilo? Endelea kusoma makala haya mstari kwa mstari, neno kwa neno, herufi
kwa herufi ili ulijue.
Niliraghibika
kuharakisha kwenda kumuona baada ya usiku huo wa Machi 26, 2017, kuusikia wimbo
wake mashuhuri alioutunga miaka mingi kiasi, ukiimbwa katika tamasha la kumpongeza
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein.
Tamasha hilo
lililofanyika katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Mnazimmoja mjini
Zanzibar, lilikuwa maalumu kwa ajili ya kumpongeza Dk. Shein kwa kutimiza mwaka
mmoja tokea alipoapishwa kuendelea na kipindi cha pili cha uongozi wake
visiwani humu Machi 24, 2016.
Wakati
nikifuatilia matangazo ya moja kwa moja ya tamasha hilo kupitia redio ya
Shirika la Utangazaji Zanzibar, masikio yangu, na bila shaka mtima wangu pia,
vikavutwa na sauti ya mshereheshaji wa kikundi cha Culture Musical Club, Iddi
Suwedi, alipotangaza kuimbwa kwa wimbo uitwao, ‘Mpewa Hapokenyeki’.
Hapo ndipo
iliponijia picha ya Mzee Haji Gora, ambaye kwa sasa ni mgonjwa na hana tena
safari zilizokuwa zikimtoa ndani ya nyumba yake kwenda kwenye harakati zake za
maisha.
Baada ya
kufika njia ya Daraja bovu karibu na kituo cha afya maarufu Kundi, nikaegesha
chombo changu cha usafiri, na nikaanza kukatisha vichochoro kwa miguu hadi
nikafika nyumbani kwa mkongwe huyu wa sanaa.
Kwanza
nilipokelewa na mjukuu wake wa kiume aliyekuwa akicheza mpira na watoto
wenzake, na akanishindikiza hadi nyumbani kwao takriban mita 40 kutoka
nilipomkuta.
Wakati
tukiwa njiani na mtoto huyo, alinidokezea kuwa babu yake yupo lakini amefichwa
chumbani, kauli iliyonipa mshtuko nikidhani labda amezidiwa na maradhi na
nikapata wasiwasi kuwa huenda sitaruhusiwa kumuona.
Lakini
nilipofika nilishusha pumzi kwani binti yake mmoja anayetarajia kuanza chuo
wiki ijayo, alifungua mlango na kumjulisha juu ya ugeni wangu.
Nilishukuru
kumuona Mzee Gora akiwa ametoka ndani mwenyewe huku akivaa kanzu kuja kunilaki
ukumbini na hapo tukasalimiana vizuri tukiulizana habari za harakati na mambo mengine.
Binti yake
akiwa pembeni, Mzee Gora alianza kulalamika akisema, “Mimi sitaki kupigana na
wala sipendi kupigana”.
Nilipomuuliza
alikuwa na maana gani kwa kauli hiyo, akasema akiwalaumu watoto wake kwa
kitendo cha kumfungia ndani, huku akimtaka binti yake amuite daktari kwa ajili
ya kumpima ili awathibitishie kwamba ana akili zake na hakuna haja ya kumzuia
kutoka nje.
Lakini
ghafla, katikati ya mazungumzo yetu, Mzee Gora akanitaka ninyamaze akiniambia
nisikilize huku naye akiwa ametulia kimyaa kama anayesikiliza sauti itokayo
mbali.
Sijui
alikuwa amesikia kitu gani ambacho mimi pamoja na kutega sikio vizuri sikuweza
kunasa sauti yoyote zaidi ya zile za watoto waliokuwa nje ya nyumba wakicheza.
Hapo ndipo
nilipobaini, na kwa kusimuliwa na binti yake, kwamba Bwana Haji Gora, pamoja na
kuambiwa alipata homa, lakini pia ameanza kupoteza uwezo wa kufikiri na
kurudisha kumbukumbu.
Masikini,
Mzee huyu aliyetumia zaidi ya nusu ya umri wake akifanya kazi za kiuandishi
bila ya kuwa na elimu kubwa ya skuli, sasa umri unamrejesha katika utoto kiasi
cha kuhitaji kuwekwa ndani kwa wasiwasi wa kupotea.
Ndio, lazima
wawe na wasiwasi kwani nilipokuwa kwake, nilimshuhudia akiinuka kitini na
kwenda kusimama mlango wa nje huku akinadi kuwaita watu asiowaona kwa majina
ambayo hata mimi sikuweza kuyasikia vyema wala kuyahafahamu.
Na hata
nilipoaga kwa ajili ya kuondoka, Mzee Gora alikuwa wa kwanza na kama
aliyeinuliwa ghafla kitini alipokuwa amekaa na kutoka nje haraka huku binti
yake na mama mmoja aliyekuwa akisuka ukili, wakijaribu kumzuia lakini
walipomuona hashikiki wakamuachia.
Nilipotoka
nikauliza amepita njia gani ili nimfuate, lakini nikaambiwa ameingia nyumba
jirani na yake.
Sasa Mzee
Gora anahitaji matunzo na uangalizi wa hali ya juu, na hili si jambo la
kuachiwa familia yake pekee, ikifanya kazi ya kumchunga asipotee mbele ya macho
yao.
Kwa namna
Mzee huyu alivyoitangaza nchi hii kwa kutumia fasihi andishi na simulizi, na
kuandika vitabu mbalimbali vikiwemo vya watoto vinavyofundisha akhlaki njema,
mila na maadili ya Kizanzibari kidini, si mtu wa kuachwa augue bila ya msaada
maalumu angalau kuthamini juhudi zake za kuinua utajo wa Zanzibar nje ya mipaka
yake.
Nikirudi
nyuma katika wimbo ‘Mpewa Hapokonyeki’, ni ukweli usio shaka kwamba ni miongoni
mwa nyimbo zake zinazopendwa sana na unaoendelea kuishi ingawa miaka mingi
imepita tangu alipoutunga.
Ingawa Mzee
Gora alitunga wimbo huo kwa mnasaba wa wanajamii walivyo na sio kwa mtazamo wa
kisiasa, lakini ni wazi umewakuna wengi ambao wameamua kuunasibisha katika
mambo yao na hivyo kila wanapousikia roho zao huwa kwatu.
Na ni ukweli
usiofichika kwamba uongozi wa Culture Musical Club unajua fika kwamba wimbo huo
hauwezi kuachwa bila kupigwa kila wanapokuwa wanatumbuiza kwenye hafla
mbalimbali za ki-nchi.
Ni wimbo
unaowavutia wengi kutokana na ujumbe uliobeba na pia muziki na ufundi wa
wasanii wa Culture katika kucharaza vinanda.
Sina hakika
kama Mzee Gora ameusajili wimbo huu katika Idara ya Hakimiliki, lakini hata
kama amefanya hivyo, anastahiki kufaidika na tunza zinazopatikana kila pale
unapopigwa kwenye hadhara, ikizingatiwa hali yake ya sasa.
Na kwa kuwa
wanaoupiga pia hawafanyi hivyo bure bileshi kwa maana wanalipwa chochote, ni
vyema wanapogawana mapato wamkumbuke mtunzi wa wimbo huo angalau kwa ‘juisi’,
japo wapo watakaohoji vipi kuhusu nyimbo za watunzi wengine zinazotumika!
Kwa namna
ninavyoifahamu Culture, ninaamini nyimbo zao nyingi zinatungwa na wasanii wa
ndani yaani wanamuziki wenyewe kwa hivyo bila shaka wananufaika huko.
Ninapousikia
wimbo huo ukiimbwa ukumbini, mawazo yangu huwa yanasafiri hadi nyumbani kwa
mtunzi wake, ambaye bila kujua masikini, nguvu zake zinatumika kuwafurahisha
watu huku mwenyewe akiwa amelala Chumbuni akiugua.
Uko wapi
umoja wa wasanii, kiko wapi Chama cha Washairi, Kamisheni ya Utamaduni na
Baraza linalohusika na sanaa Zanzibar, mko wapi mnaonufaika kwa namna moja au
nyengine na kazi za msanii Mzee Gora katika wakati huu anaokuhitajini sana.
Kwa muktadha
huo, niwasifu pia Chama cha Kiswahili Zanzibar (CHAKIZA) kwa kujipangia ziara
za kumtembelea ili kumfariji mzee na mwalimu wetu huyu.
Huu ndio
wakati wa kumuonesha upendo na kumthamini, chambilecho mwimbaji wa Mombasa Bi.
Zuhra Saleh aliyeimba, “Mpende bado yuko hai, Pendo alithamini. Ukimpenda yuko
kaburini umelitupa pendo lako hewani”.
Ninamuomba
Mwenyezi Mungu amponye na ampe umri mrefu Mzee Gora, lakini mtu aliyesaidia
sana harakati za kukienzi na kukisambaza Kiswahili kwa vitendo akitunga vitabu
mbalimbali likiwemo Kamusi la Kitumbatu, ni mtu wa kutunzwa sasa badala ya
kusubiri afe ndipo kila mtu amsifu kwa maneno mengi ambayo wakati huo
hayatakuwa na faida yoyote kwake.
Mapenzi yetu
kwake tuyaoneshe sasa, na asiwe mwenzetu wakati wa uzima tu, na hili litampa
faraja yeye na familia yake wakitambua jamii na nchi zinathamini mchango wake.
Kabla
sijahitimisha makala haya, napenda kumshukuru na kumpongeza kwa dhati,
mwandishi mwenzangu Ali Saleh ‘Alberto’ kwa kuwa wa kwanza hapa Zanzibar na
Tanzania kwa jumla, kuandika kitabu kuhusu maisha ya Mzee Gora ambacho
alikizindua miezi kadhaa iliyopita.
Mtu
akikisoma kitabu hicho alichokipa jina la ‘Maisha ya Haji Gora’, anapelekwa mbali
mno tangu enzi za utoto wa msanii huyo na si ajabu akajikuta anajiweka pahala
pake au kama anayemuona kwa ufundi wa lugha yenye kuonesha picha uliotumika
katika uandishi wake.
Angalau Ali
ameonesha njia, vipi kumuenzi mtu akiwa hai. Tufuate nyayo zake katika
kumsaidia gwiji huyu ambaye vitabu vyake vimetapakaa Afrika Mashariki nzima na
kwengineko Kiswahili kinakotumika.
Tel: 0777
865050
E-mail:
salumss@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment