Masuala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji yameendelea kuwa tatizo
kwa taifa na ulimwengu mzima na ili kukabiliana na tatizo hili, kumekuwa na mwitikio
mkubwa wa kimataifa na kitaifa katika kukabilana na vitendo vya ukatili wa
kijinsia.
Akiongea na vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam leo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Watoto wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Margaret Mussai amesema Serikali
inalaani na kukemea vikali ukatili kwani unadhalilisha na kunyanyasa hadhi na
utu wa mwanamke na mtoto wa kike akisema jambo hili halikubaliki.
Aidha aliongeza kuwa ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe na wadau
wote kuhakikisha kuwa tunashiriki kwa pamoja kuzuia na hatimaye kutokomeza
ukatili wa kijinsia katika jamii zetu, hususan kuzua ukeketaji.
Aidha kulingana na takwimu za Tafiti ya Idadi ya
Watu na Afya (TDHS 2010) inakadiriwa
kuwa ukeketaji kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15- 49 ni asilimia
14.6, hii imepungua kidogo ukilinganisha
na asilimia 17.9 mwaka 1996. Aidha,
takwimu hizo kwa mwaka 2015/16 zinaonyesha kiwango cha ukeketaji kwa wanawake
na watoto kimepungua kutoka asilimia 14.6 ya mwaka 2010 hadi kufukia asilimia 10.
Margaret ametaja mikoa inayoongoza kwa vitendo vya
ukeketaji ni Manyara (58%), ikifuatiwa na Dodoma (47%) na Arusha (41%) akitaja
kuwa kupunguwa kwa vitendo vya ukeketaji kunatokana na kampeni za uhamasishaji, uelewa na
kujitambua kwa wasichana wanaofanyiwa vitendo hivyo, hofu ya kufungwa kutokana
na uwepo wa sheria zinazotekelezwa, hivyo mangariba na wazee wa kimila kwa
kiasi kikubwa wanaamua kuacha mila hii ya ukeketaji.
Aidha Serikali inahimiza kuendeleza mila zenye
manufaa na kujenga utamaduni chanya kwa jamii. Amewaomba wadau mabalimbali wakiwemo wana habari,
mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za dini, sekta binafsi na mamlaka za
serikali za mitaa kuendelea kuongeza juhudi za kuelimisha jamii kuachana na mila
zinazochochea ukeketaji.
Aidha Serikali imetunga sera, sheria, miongozo na
kuandaa mikakati mbalimbali katika jitihada za kupambana na tatizo la ukatili
wa kijinsia,ikiwemo ukeketaji, Sera ya Wanawake na Maendeleo ya Jinsia (2000)
na Mkakati wa Maendeleo ya Jinsia (2005), Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008).
Sheria ya Makosa ya Kujamiiana -SOSPA (1998) na Sheria ya Mtoto (2009) vyote
vikiwa na lengo la kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katika kuongeza jitihada za kutokomeza
ukeketaji serikali imeandaa Mpango wa kazi wa Taifa wa miaka mitano wa kutokomeza
ukatili dhidi ya wanawake na watoto (2017/18-2021/22). Mpangokazi umeanisha
maeneo nane muhimu mojawapo ni la kuondoa mila na desturi zenye madhara.
Kupitia mpango huu serikali imedhamiria kupunguza ukeketaji kwa wanawake kwa
asilimia 50ifikapo mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment