Waziri MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
haina kipingamizi na wazo la kuifanya hospitali ya rufaa ya Haydom kuwa ya
kanda kwani hatua hiyo itaupunguzia mzigo Serikali.
“Serikali hii ni sikivu, na kuifanya hospitali
hii kuwa ya kanda ni kazi ndogo. Kwa hiyo nitamleta Waziri wa Afya aje
awaongoze kusimamia vigezo vya kuifanya hospitali hii iwe ya kanda,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu,
Februari 20, 2017) wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa kata ya Haydom
kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kata.
"Serikali haina kipingamizi na wazo lenu,
cha msingi ni vigezo muhimu vifuatwe. Kwa hiyo, nitamleta Waziri wa Afya
awasaidie kuangalia vigezo," amesisitiza.
“Kama vigezo havipo, tushirikiane kuvikamilisha kwa
sababu uwepo wa hospitali hii kwa hadhi ya kanda kunaisadia Serikali kutokana
na nafasi yake kijiografia,” amesema Waziri Mkuu
“Nia yetu ni kupunguza gharama kwa mgonjwa
anayelazimika kutoka Simiyu hadi Bugando (Mwanza) au kutoka Arusha hadi
Muhimbili (Dar es Salaam). Hapa ni
katikati na nimearifiwa kuwa wagonjwa kutoka mikoa mitano ya Tabora, Simiyu,
Arusha, Singida na Manyara wanafika hapa kupatiwa matibabu,” amesema.
Amesema Serikali imepokea maombi kwa ajili ya
watumishi wanaotakiwa kwenye hospitali hiyo na kwamba hivi karibuni itaajiri
watumishi kati ya 5,000 hadi 6,000 wa sekta ya afya peke yake. “Tumekwishaanza
kuajiri, tumeanza na sekta ya elimu kwa kuajiri walimu 4,693 ambao wote ni wa
fani ya sayansi. Na sekta inayofuata ni ya afya, kwa hiyo hao watumishi 90
wanaohitajika watapatikana kwenye kundi hilo hilo,” amesema.
Hospitali hiyo inahudumia wananchi kutoka wilaya nane
za Mbulu, Hanang, Babati, Karatu, Mkalama, Iramba, Kondoa na Meatu.
Wakati huohuo, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Bibi Hannamarie Kaarstad
ambaye alikuwepo kwenye mkutano huo, alisema amefarijika na mchango unaotolewa
na Serikali ya Tanzania kusaidia juhudi zinazofanywa na marafiki wa hospitali
walioko Norway.
“Hospitali ya Haydom ni mahali thabiti ambapo
mshikamano baina ya Tanzania na Norway unaweza kuonekana kwa dhahiri.
Nawashukuru watumishi wa hospitali kwa moyo wao wa kujitoa kuwahudumia wananchi
wa wilaya ya Mbulu na maeneo ya jirani,” amesema.
Hospitali hiyo ambayo inaendeshwa na Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mbulu kwa ufadhili kutoka
Serikali za Tanzania na Norway, ilianzishwa mwaka 1955 ikiwa na uwezo wa kulaza
wagonjwa 50. Hivi sasa ina uwezo wa kulaza wagonjwa 420 kwa wakati mmoja.
Pia inatoa huduma za upasuaji, magonjwa ya macho, tiba
ya mifupa na mazoezi ya viungo. Ilipandishwa hadhi kuwa ya rufaa baada ya mkoa
wa Manyara kuanzishwa.
Mapema, akisoma taarifa kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji
wa Tiba wa hospitali hiyo, Dk. Emanuel Q. Nuwass alisema wameomba kibali cha
ajira kwa watumishi 90 kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017.
“Tumeomba pia hospitali ipandishwe hadhi na kuwa ya
rufaa ya kanda (Kaskazini kati au Kanda maalum) ili iweze kutoa huduma bora kwa
mkoa wa Manyara na mikoa jirani kwani wahisani wa maendeleo wako tayari
kuchangia ujenzi wa miundombinu,” alisema.
Pia aliomba waongezewe ruzuku ya dawa ikilinganishwa
na ya sasa hivi ambayo ni asilimia 15 na pia waongezwe malipo ya on call allowance kwa ajili ya madaktari
na watumishi wengine wa hospitali hiyo.
(mwisho)
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, FEBRUARI 20, 2017.
No comments:
Post a Comment