Na Karama Kenyunko
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeitupilia mbali hati ya kiapo ya mkuu wa upelelezi Ilala, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Denis Mujumba na kumuachia Tundu lissu kwa dhamana.
Lissu yuko nje kwa dhamana ya shilingi milioni ishirini na mdhamini mmoja.
Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa mashtaka kumsomea Lissu ambaye ni Mbunge na mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani, mashtaka yake na kuwasilisha hati ya kiapo kupinga mbunge huyo kupewa dhamana.
Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo alisema kuwa kiapo kilichowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka kina mapungufu makubwa sana.
Amesema kuwa kukosekana kwa namba ya kesi na mahali ambapo inaonyesha muapaji wa kiapo hicho aliapa ni mapungufu makubwa.
Ameongeza kuwa mshtakiwa Lissu anahaki ya kupata dhamana kwa kuwa shtaka analokabiliwa nalo linadhaminika licha ya kuwa na kesi tatu tofauti mahakamani hapo kama ambapo kiapo kilivyosema.
Amesema kuwa, licha ya kuwa Lissu kweli anav mashtaka mahakamani hapo lakini hakuna shtaka hata moja ambalo amekutwa na hatia na alilokutwa nalo na hatia Kabla ya kiapo hicho jopo la mawakili wanne likiongozwa na wakili Mwandamizi wa Serikali Mutalemwa Kishenyi aliyekuwa akisaidiana na Wakili Easter Martin, Jackline Nyantori na Clementina Masawe walimsomea mshtakiwa mashtaka yake manne yanayomkabili ya kutoa lugha ya uchochezi.
Lissu ambaye amefikishwa katika viwanja vya mahakama hiyo leo majira ya saa 11.42 asubuhi akiwa ndani ya land lover ya polisi pamoja na msanii maarufu wa uigizaji nchini Wema Sepetu na watuhumiwa wengine alikamatwa juzi mara baada ya kutoka kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma. Saa 12:24 mchana, Lissu alipandishwa kizimbani Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa manne ya kutoa lugha ya uchochezi.
Katika kesi hiyo namba 48 ya mwaka 2017, Lissu anatetewa na mawakili watano, Peter Kibatala, Omary Msemo, John Mallya na Fredrick Kihwelo.Jeremiah Ntobesya.
Wakili Kishenyi alidai kuwa Januari 11, mwaka huu maeneo ya Kibunju Maungoni maeneo ya Magharibi B wilaya ya Mjini Magharibi mkoa wa Zanzibar Lissu alitoa matamko mbalimbali ya uchochezi
Moja kati ya mashtaka hayo ni kwamba mshtakiwa Lissu akiwa kama Mtanzania kutoka Bara, kabla ya uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Dimani, ambapo akiwa kwenye Kampeni alisema kuwa “…Tangu mwaka 1964 Tanganyika ndiyo inayoamua nani atawale Zanzibar…”. Kishenyi alidai kuwa maneno hayo yangesababisha uvunjifu wa amani.
Mshtakiwa Lissu alipoulizwa kama ni kweli ametenda makosa hayo, alikubaliana na makosa yote na kudai kuwa ni kweli alisema hayo maneno lakini kusema ukweli sio kosa la jinai, hivyo jibu lake ni hapana.
Matamko mengine anayodaiwa kutamka Lissu ni kuwa, “…Tangu mwaka 1964 Zanzibar inakaliwa Kijeshi na Tanganyika, nane anaye bisha…Tangu mwaka 1995 ikifika uchaguzi askari wa Tanganyika wanahamia Zanzibar ili kuja kuhakikisha vibaraka wao wa Zanzibar hawaondolewi madarakani na wananchi wa Zanzibar mnapigwa,
Mnateswa, mnauawa kwa sababu ya ukoloni wa Tanganyika kwa Zanzibar….,Marehemu Karume alipoanza kushtakiwa mwaka 71, 72 akauawa…itakapofika tarehe 15 mwezi wa kwanza muadhimishe miaka 53 ya kukaliwa kijeshi na Tanganyika…,”.
Aidha inadaiwa kuwa, siku na mahali hapo Lissu akiwa kwenye kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Dimani alisema kuwa “…Jumbe aliondolewa Dodoma, na Ally Hassan Mwinyi alipewa urais wa Zanzibar Dodoma, na aliyempa ni Nyerere na si Wazanzibar…, marais wa Zanzibar wote ni made in Tanganyika…, wametengenezwa Tanganyika, wako madarakani kwa sababu ya Tanganyika,”.
Katika shtaka la mwisho la kutoa lugha ya uchochezi kwa kutamka kuwa
“…Zanzibar wanatawaliwa na Tanganyika kwa kivuli cha Tanzania, Tanzania ni Tanganyika…, Tanzania ni kivuli tu cha kuikalia Zanzibar, cha kuigeuza Zanzibar koloni, na makoloni uwa yananyonywa,
Yananyonywa kisiasa, kiuchumi na yanakandamizwa kijeshi…Metawaliwa na Tanganyika kisiasa miaka yote hii…, Mohamed Shein hana lolote ni kibaraka tu siku watawala wakisema hatufai ataondolewa tu kama alivyo ondolewa Aboud Jumbe…,”.
Kishenyi alidai kuwa maneno hayo ya Lissu yangesababisha uvunjifu wa amani.
Baada ya kusoma mashtaka hayo upande wa serikali ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kesi hiyo iahirishwe.
Aidha aliomba mahakama kuzuia dhamana kwa mshtakiwa, maombi ambayo yanaungwa mkono na kiapo kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Ilala, ASP Mujumba.
Kiapo hicho kimewasilishwa kikiwa na hoja kadhaa ya kutaka Lissu akose dhamana ikiwemo ya kukabiliwa na kesi tatu katika mahakama hiyo ikiwemo namba 279/2016, 218/2016 na 233/2016.
Hata hivyo Hakimu Shahidi baada ya kupitia hoja zote zilizotolewa na upande wa utetezi na ule wa serikali alifikia uamuzi kuwa,mshtakiwa anahaki ya kupata dhamana kwa kuwa shtaka linalomkabili inadhaminika na kwamba hati hiyo ya kiapo inamapungufu sana.
Tundulisu akishuka kwenye gari akiwa amebeba suti yake
Tundu Lisu akielekea Rumande kwa ajili ya kusubiri kupandishwa kizimbani.
No comments:
Post a Comment