Thursday, February 23, 2017

Serikali yaunga Mkono uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (TDF).

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo  Mhe. Nape Moses Nnauye akiongea na wadau wa michezo katika  ufunguzi  wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ulioanzishwa na  Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo  Jijini Dar es Salaam.
  Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw.Jamal Malinzi akisoma risala wakati  wa ufunguzi  wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ulioanzishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu lengo ikiwa ni kubuni vyanzo mbalimbali vya rasilimali ili kuwezesha shirikisho hilo katika kutekeleza kazi zake.
  Mkuu wa Kitengo cha Ufundi  wa Maendeleo ya Soka nchini Bw. Kim Poulsen akiongea na wadau wa michezo katika uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) leo Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo  Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akijadiliana jambo na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw.Jamal Malinzi katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) leo Jijini .
 Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) kushoto ni  Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa Meshack Bandawe, Katikati ni Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Beatrice Singano na kulia ni Meneja Mwandamizi wa Benki ya NBC Salmi Rupia.
  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akimkabidhi nyaraka za Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) kwa  Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa Meshack Bandawe (kushoto), ambaye ni mjumbe wa bodi hiyo ,katikati ni  Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw.Jamal Malinzi.Leo Jijini dar es Salaam.
 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akimkabidhi nyaraka za Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) kwa  Meneja Mwandamizi wa Benki ya NBC Salmi Rupia(kushoto), katikati ni   Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Bw.Jamal Malinzi.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF)  mara baada ya kuuzindua leo Jijini Dar es Salaam .(Picha na Lorietha Laurence-WHUSM).

Na Lorietha Laurence-WHUSM
Serikali imeunga mkono uwanzishwaji wa Bodi ya Maendeleo ya Mpira wa Miguu (TDF)  wenye lengo la kuratibu vyanzo mbalimbali vya mapato ili kutekeleza maendeleo ya mpira nchini ikiwemo  kukuza vipaji vya michezo kwa vijana wa kike na wa kiume.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye alipozindua Bodi hiyo iliyo chini ya uratibu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania leo Jijini Dar es Salaam ambapo aliwataka wadau wa michezo,wananchi na sekta binafsi kuunga mkono jitihada  hizo.
“Jambo hili ni jema sana katika sekta  ya michezo nchini hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha tunaunga mkono juhudi hizi zenye lengo la kuleta matokeo chanya katika sekta hii muhimu mfano mzuri ni vijana wetu wa Serengeti Boys  wameshatuonyesha kuwa tunaweza kufika mbali” alisema Waziri Nnauye.
Aidha, aliitaka Bodi hiyo kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu ili kuhakikisha mfuko huu unakua na hivyo kuwezesha utendaji fanisi wa kukuza vipaji vya michezo wa kike na wa kiume na kwa wale watakaokiuka miiko ya kazi uongozi usisite kuchukua hatua za kinidhamu dhidi yao.
Naye, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa Tanzania (TFF) Bw.Jamal Malinzi  alieleza kuwa lengo la kuunda mfuko huo ni kusaidi katika kuendesha shughuli za Shirikisho ambapo kutakuwa na utaratibu maalum wa kuomba fedha kutoka katika mfuko huo.
“Kiutaratibu Sekretrarieti ya TFF ikiwa na mahitaji itakuwa inatuma maombi kwenda bodi na pale bodi inaporijiridhisha na uhalali wa maombi hayo itatoa ruhusa kwa Shirikisho kuendelea na utaratibu wa kupatiwa fedha “alisema Bw.Malinzi.
Bw. Malinzi aliongeza kwa kuahidi kuwa TFF itahakikisha Tanzania inang’ara kimataifa katika mpira wa miguu kwa kufuzu kucheza fainali za kombe la Dunia mwaka 2026 kwa upande wa wanaume (Taifa Stars) na kwa upande wa wanawake (Twiga Stars) 2019.
Akiongea kuhusu kuwekeza katika mpira wa vijana Bw. Malinzi alisema kuwa Msingi mkubwa wa mafanikio ya timu za taifa duniani kote ni kuwekeza katika mpira wa vijana ili kuhakikisha wanafundishwa mpira kwa kiwango cha kimataifa katika umri mdogo utakaowasaidia kuwa imara.
Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) ulirasimishwa rasmi katika Mkutano Mkuu wa TFF wa mwaka 2015 hivyo mfuko huo upo katika katiba ya TFF huku jukumu lake kubwa ikiwa ni kubuni vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo vitasaidia Shirikisho hilo katika kutekeleza kazi zake mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

No comments: