Thursday, February 23, 2017

MREMA AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KWA MATIBABU NCHINI INDIA


Na Eliphace Marwa -Maelezo

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanikisha safari ya kwenda nchini India kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Dkt. Mrema ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waaandishi wa habari kuhusu uteuzi uliofanywa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba kwa kuwateua wajumbe wawili wa bodi hiyo.

“Nachukua nafasi hii kumshukuru Rais Magufuli , Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Wizara ya Afya na Ikulu, kwa kunipeleka nchini India kufanyiwa uchunguzi wa afya yangu na kupatiwa matibabu na sasa afya yangu imeimarika na niko tayari kutekeleza majukumu yangu”, alisema Dkt. Mrema.

Akizungumzia uteuzi uliofanywa na Waziri Nchemba, Mrema amesema kuwa toka alivyoteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi hiyo haikukaa vikao kutokana na baadhi ya wajumbe wa Bodi hiyo kumaliza muda wao.

“Nilipoteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Bodi ilikuwa bado haijakutana na kufanya vikao kwasababu kuna wajumbe walikuwa wamemaliza muda wao na Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa bado hajateua wajumbe wengine lakini kwa sasa amakwisha fanya kazi ya uteuzi”, alisema Dkt. Mrema.

Mrema aliwataja walioteuliwa kuwa wajumbe wa Bodi ya Parole Taifa ni pamoja na Bwana Francis Kistola na Bwana John William Nyoka.

Aidha Mrema amempongeza Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kukamilisha kazi ya uteuzi na amewapongeza wajumbe walioteuliwa na kuwakaribisha kwa mikono miwili kwenye bodi hiyo na kuomba ushirikiano wao na uzoefu wao ili kukamilisha majukumu ya bodi ya Parole.

Vilevile Mrema amesema kuwa kikao cha kwanza cha bodi mpya ya parole kitafanyika tarehe 3 na 4 Machi 2017 jijini Dar es Salaam na bodi hiyo mpya itazinduliwa siku hiyo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Nchemba. 
 Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema (katikati) akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitangaza tarehe ya uzinduzi wa bodi mpya ya parole taifa tarehe 3 na 4 Machi 2017 mapema hii leo jijini Dar es Salaam, kushoto ni Msaidizi wake Bw. Clemence Munisi na kulia ni Mkewe Bi. Rose Augustino Mrema.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Taifa, Dkt. Augustine Lyatonga Mrema (katikati mwenye kofia) wakati akitangaza tarehe ya uzinduzi wa bodi mpya ya parole taifa tarehe 3 na 4 Machi 2017 mapema hii leo jijini Dar es Salaam.Picha na Eliphace Marwa - Maelezo

No comments: