Thursday, February 9, 2017

NEC yavisihi vyama vya siasa kuhusu elimu ya mpiga kura


Hussein Makame, NEC-Bukoba

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevihimiza vyama vya siasa kutoa elimu ya mpiga kura kwa wapiga kura na wanachama wao bila ya kuegemea itikadi ya vyama vyao kwani sio wote wanaowaelimisha ni wanachama wao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe wakati akitoa elimu ya mpiga kura kupitia kituo cha Redio Kasibante Fm kilichopo mjini Bukoba.

Alisema mdau namba moja wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni chama cha saisa na kwamba NEC inakutana na vyama hivyo mara kwa mara kushauriana namna ya kutoa elimu ya mpiga kura na namna ya kuwafikia wananchi wengi.

“Kwa hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi inavihimiza vyama vya siasa kutoa elimu ya mpiga kura kwa wapiga kura na kwa wanachama wao pia” alisema Bw. Kawishe na kuongeza:

“Tena tunawasihi vyama vya siasa wasitoe elimu kwa njia ya itikadi za kichama watoe elimu isiyoegemea itikadi yoyote kwa sababu kuna wengine sio wanachama wa chama chake lakini watawapigia kura”

Hivyo aliviomba vyama vya siasa viwe wadau, walimu na wawezeshaji katika kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi kupitia katika mikutano yao na wananchi na kwenye mikutano yao wenyewe ndani ya vyama.

“Ndio mana hata katika chaguzi mbalimbali tunachapisha ile karatasi ya mfano ya kura tunavipa vyama vinaenda kufundishia watu wao namna ya kupiga kura” alisema.

Bw. Kawishe alifafanua kuwa pamoja na kuvikumbusha vyama vya siasa wajibu wao katika kutoa elimu ya wapiga kura, vyama hivyo vimekuwa vikitoa ushirikiano mzuri katika kutoa elimu hiyo.

Alisema asilimia kubwa ya vyama hivyo vilitoa elimu ya mpiga kura na kuelimisha wananchi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ndio maana mwitikio wa wapiga kura kupiga kura ulikuwa mkubwa ikilinganishwa na chaguzi zilizopita.

Alibainisha kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wapiga kura walioandikishwa walikuwa Milioni 23 na waliojitokeza kupiga kura walikuwa Milioni 15.

“Kwa kweli ni asilimia kubwa sana waliojitokeza kwa sababu katika uchaguzi wa mwaka 2010 tuliandikisha wapiga kura Milioni 20 lakini wakajitokeza kupiga kura watu Milioni 8” alifafanua Bw. Kawishe.

“Kwa hiyo tumeona tofauti na kwa kweli vyama viliiitikia vizuri wito wa kuelimisha wapiga kura na vilikuwa vinafundisha kweli kweli wakipanda majukwaani” aliongeza.

Hata hivyo, Bw. Kawishe alisema pamoja na kutoa fursa hiyo kwa vyama Tume haikusita kuvirekebisha pale ambapo vilikosea katika kutoa elimu ya mpiga kura.

Kwa sasa Tanzania ina vyama vya siasa 19 vyenya usajili wa kudumu kutoka vyama 22 vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 baada ya vyama vitatu kufutiwa usajili na Msajili wa Vyama vya Sisasa mwaka jana 2016.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kutekeleza matakwa ya Kisheria ya kutoa elimu ya mpiga kura nchi nzima katika kipindi chote cha mwaka ambapo mbali na kutembelea Kasibante Fm, ilitoa elimu pia katika Shule za Sekondari za Bukoba na Kahororo zilizopo mjini Bukoba.

 . Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akitoa elimu ya mpiga kura kupitia kituo cha Redio Kasibante FM cha mjini Bukoba juzi.
. Mtangazaji wa Redio Kasibante FM ya mjini Bukoba, Tafawa Saidi akimuuliza swali Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe kwenye kipindi cha Mchakamchaka. 
 Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bukoba (hawapo pichani) wakati akitoa elimu ya Mpiga Kura shuleni hapo.Kulia kwake ni Afisa Uchaguzi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Erick Bazampola, Mkuu wa shule hiyo Bw. Raymond Mutakyawa na wasaidizi wake. 
 Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bukoba.
 Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Bukoba wakimsiliza Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, wakati akitoa elimu ya mpiga kura.
 Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bukoba Shabani Suleimani akiuliza swali kuhusu elimu ya mpiga kura.
 Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Shule ya Sekondari Bukoba baada ya kumaliza kutoa elimu ya mpiga kura shuleni hapo.Kushoto mwanaume ni Mkuu wa Shule hiyo Bw. Raymond Mutakyawa na kulia kwa Kawishe ni Afisa Uchaguzi Bw. Erick Bazampola. 
 Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Emmanuel Kawishe, akitoa elimu ya mpiga kura kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kahororo iliyoko mjini Bukoba juzi.Kushoto kwake ni Afisa Elimu Taaluma kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Arbogast Kiheka.
Mmoja wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Kahororo, akiuliza swali baada ya kupata elimu ya mpiga kura.
Picha na Hussein Makame, NEC-Bukoba 

No comments: