Tuesday, February 7, 2017

Migogoro ya ardhi haiwezi kumalizwa kwa makatazo-Nyanduga

Sehemu ya maliasili zinazotokana na miti ya mikoko zilizokamatwa na Idara ya Misita Wilayani Rufiji kwa madai ya kuvunwa bila kufuata utaratibu.
Sehemu ya msitu wa Mikoko katika eneo la Rufiji- Delta
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Bahame Tom Nyanduga aliyeinua vijitabu juu ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa taarifa hiyo ya uchunguzi wa hadharani kuhusu mgogoro wa ardhi katika Kata ya Salale. Kulia ni Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwanasheria, Ndugu Mohamed Magati na kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibiti, Ndugu Sanga, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Tume, Ndugu Francis Nzuki ( aliyeshika kipaza sauti) na wa tatu kushoto ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyamisati, Ndugu Jumanne Kikumbi.
Baadhi ya Wazee wakiwa na vitabu wakati wa uzinduzi rasmi wa taarifa hiyo ya uchunguzi wa hadharani kuhusu mgogoro wa ardhi katika Kata ya Salale



Na Mbaraka Kambona,

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Mheshimiwa Bahame Tom Nyanduga amesema kuwa migogoro ya ardhi nchini haiwezi kumalizwa kwa makatazo bali majadiliano.

Nyanduga aliyasema hayo Februari 6, 2017 alipokuwa anazindua taarifa ya uchunguzi wa hadharani kuhusu mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Nyamisati, kata ya Salale, Rufiji, Mkoani Pwani.

Wakati anazindua taarifa hiyo ya uchunguzi, Nyanduga alisema kuwa migogoro ya ardhi nchini inaweza kutatuliwa kwa majadiliano na mahusiano mazuri ikiwemo kila upande kutambua majukumu ya mwenzake kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Mwenyekiti huyo wakati akiongea alitaja azimio la Umoja wa Mataifa la Septemba 2015 lililohusisha nchi 194 ambalo linataja misingi 17 ya maendeleo endelevu, mojawapo ni ushirikishwaji wa wananchi hususan katika kupiga vita umasikini na njaa.

“Ukivamia na kukata mazao ya watu unasabisha njaa na hivyo itakuwa umekiuka haki za binadamu na ni kinyume na azimio la Umoja wa Mataifa, katika mivutano kama hii lazima ushirikishwaji uwepo tena unaotambua jinsia zote” alisema Nyanduga,

Kauli hiyo ya Mwenyekiti inafuatia taarifa ya uchunguzi huo uliofanywa na Tume mwaka 2013 baada na kubaini vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu na misingi ya utwala bora vilivyofanywa na mamlaka dhidi ya wananchi. 

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kati ya Oktoba 25 hadi 29, 2011 wananchi wa vijiji vya Nyamisati, Kiomboi, Mchinga na Mfisini vya Kata ya Salale walivamiwa na maafisa wa Polisi wakiwa na silaha pamoja na wafanyakazi wa Mamlaka ya Misitu na kuwatishia wakazi wa vijiji hivyo kwa kuchoma moto na kuharibu nyumba, mashamba ya mpunga, minazi na miti ya kudumu ya matunda ikiwemo miembe na mikorosho wakiwatuhumu wanakijiji hao kwa kujihusisha na kilimo kisicho halali na kuharibu msitu wa Mikoko uliopo katika eneo hilo la Rufiji Delta.

Kufuatia tukio hilo wanakijiji walipeleka lalamiko lao kwa Tume kuwalalamikia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya Rufiji pamoja na uongozi wa mamlaka ya misitu katika Kata ya Salale kwa kutumia nguvu kutaka kuwazuia kuendesha shughuli za kilimo cha Mpunga kwa madai kuwa wamevamia eneo hilo la hifadhi ya Mikoko na kuharibu mazalia ya samaki.

Agosti 13, 2013 Tume ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Manento pamoja na maafisa walifanya uchunguzi wa hadharani kuhusu mgogoro huo wa Kata ya Salale na kutoa mapendekezo katika taarifa hiyo kadhaa. 

Moja ya mapendekezo hayo ni kwamba, Wanakijiji hao wa Kata ya Salale wasihamishwe kwakuwa ushahidi uliopatikana unaonesha jinsi wanavyoshiriki katika kulinda mazingira yaliyowazunguka, na pili, Tume itaendelea kuhusisha wadau wote katika mgogoro huu na hivi karibuni itafanya mkutano na wadau wote ili kufanikisha mpango uliosawa wa usimamizi wa maliasili katika eneo hilo.

Vilevile, Tume imependekeza kwa serikali, mamlaka zote na wakala wafanye kazi kwa pamoja wakishirikiana na wananchi wa Kata ya Salale katika kulitafutia ufumbuzi wa kudumu tatizo lililopo ili watu waendelee na maisha yao ya kila siku kwa amani na wahakikishiwe usalama chini ya sheria jambo ambalo ni msingi katika serikali inayoamini utawala wa sheria.

Aidha, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwanasheria, Ndugu Mohamed Magati alisema kuwa taarifa hiyo imekuja katika wakati muafaka hivyo wataitumia kama muongozo katika kushughulikia matatizo yalipo ikizingatiwa Mkoa wa Pwani kwa sasa umekuwa kinara kutekeleza kwa vitendo sera ya uchumi wa viwanda.

“Taarifa ya Tume imekuja wakati muafaka na sisi tutatekeleza yale yote ambayo Tume itakayoelekeza kusimamiwa ili kutatua mgogoro uliopo” alisema Magati

“Muingiliano wa uchumi wa viwanda katika mkoa wetu ni mkubwa, hivyo ni muhimu kwa wananchi na viongozi tukawajibika kwa kuzingatia utawala bora na sheria”, aliongeza Magati.

No comments: