Tuesday, February 28, 2017

MAKALA: WIKI YA SHERIA NA SIKU YA SHERIA NCHINI, 2017

Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akikagua gwaride maalum lililoandaliwa, ukaguzi wa gwaride hili huashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika.

Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania

Nchi yoyote yenye kuzingatia misingi ya Utawala wa Sheria, huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta amani na Maendeleo ya kiuchumi katika taifa husika.

Hii inajidhihirisha kupitia Kaulimbiu ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini, 2017 ambayo ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’

Kauli mbiu hii ina maana ya kuwa kukamilishwa mapema kwa mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.
Hivi karibuni Mahakama ya Tanzania iliadhimisha Siku ya Sheria nchini, ambayo huashiria kuanza rasmi kwa mwaka wa Mahakama ambapo shughuli za usikilizaji wa Mashauri huanza rasmi.

Kwa mwaka huu, sherehe za Siku ya Sheria nchini ziliadhimishwa rasmi tarehe 02.02.2017, ambapo kila Mkoa uliadhimisha, kwa upande wa Dar es Salaam, Sherehe hizi zilifanyika katika Kiwanja cha Mahakama kilichopo Chimala karibu na Hospitali ya ‘Ocean road’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akihutubia watumishi na wageni waalikwa katika Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02, 2017.

Aidha; Sherehe za Kilele cha Siku ya Sheria nchini zilitanguliwa na Maonyesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza rasmi Januari, 28 hadi Februari 01, 2017, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika nchi nzima lengo kuu likiwa ni kutoa elimu ya Sheria kwa Wananchi juu ya huduma na taratibu mbalimbali za Kisheria.

Kwa upande wa Dar es Salaam, Maonyesho ya Wiki ya Sheria yalifanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini humo, Wadau walioshiriki ni pamoja Mahakama yenyewe kama mwenyeji, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mahakama Kuu Zanzibar, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Mahakama (AGC), Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Mkemia Mkuu wa Serikali, Chuo cha Uongozi wa Mahakama IJA, Mkuu wa Kitivo cha Sheria, Chuo Kikuu Huria, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wengine ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Taasisi zinazotoa msaada wa Kisheria (Legal Aid), TAKUKURU (PCCB), Polisi, Magereza, Msajili, Mabaraza ya Ardhi,  Chama  cha Wanasheria
Tanganyika (TLS), Tume ya Kurekebisha Sheria, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA, Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA),  Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Sekretarieti ya Msaada wa Sheria, Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ‘Tanzania Network of Legal Aid Provider (TANLAPS),’ Legal Aid and Human Centre na NHIF.
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji Prof. Ibrahim Juma akisoma risala yake ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika Februari 02, 2017, waliopo nyuma ya Mhe. Kaimu Jaji Mkuu ni baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Tanzania.

Katika maonesho hayo kulikuwa na uwakilishi wa ngazi zote za Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama ya Rufaa ambapo taratibu/huduma mbalimbali za Kimahakama zilitolewa kwa wananchi waliopata fursa ya kutembelea mabanda ya Maonesaho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Lengo la kufanyika kwa Maonesho hayo ilikuwa ni kutoa fursa kwa wananchi kufahamu shughuli za Mahakama pamoja na Wadau wa Sekta Sheria kwa ujumla, vilevile kuwawezesha wananchi kupata elimu juu ya taratibu mbalimbali Mahakama katika upatikanaji wa haki.

Aidha, Sherehe za kilele cha Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Wageni mbalimbali akiwepo Spika wa Bunge la Tanzania, Waziri wa Katiba na Sheria, Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini, Mwendesha Mashtaka (DPP), TLS, Majaji Wastaafu,  Mabalozi, Viongozi wa dini mbalimbali n.k.

Aidha katika Sherehe hizo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumzia masuala kadhaa ambayo ni pamoja na:-
Kutoa pongezi kwa kasi nzuri ya Uondoshaji wa Mashauri, ambapo katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Jaji Mkuu alisema kuwa ‘Pamoja na changamoto inayotukabili ya uwiano usio sawa wa idadi ya Majaji na Mahakimu na Watumishi wengine kama Wasaidizi wa Kumbukumbu; wastani wa jumla ya umalizaji wa mashauri upo wa asilimia 101 (101%), yaani kwa tafsiri ya kila mashauri mia moja (100) yanayosajiliwa uwezo wa kuyamaliza ni asilimia 101 (101%).
Kwa mwaka wa Mahakama ulioisha Desemba, 2016, jumla ya mashauri 276,147 yalisajiliwa na mashauri yaliyosikilizwa na kukamilika yalikuwa ni 279,331.
Viongozi wanaoiwakilisha Mihimili mitatu ya Dola wakiwa katika picha ya pamoja katika Siku ya Sheria nchini, wa pili kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, wa kwanza kushoto ni Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji, Prof. Ibrahim Juma, wa pili kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na wa kwanza kulia, Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali.

Mashauri ambayo yapo bado Mahakamani ilipofika Desemba, 2016 ni jumla 56,531 na kati ya hayo, yenye sifa ya kuitwa ya zamani (backlogs) ni mashauri 3,618 na ambayo ni sawa na wastani wa  asilimia sita (6%) tu.

Mhe. Prof. Jaji Juma aliongeza kuwa kati ya mashauri 249 yaliyosajiliwa Mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ambapo ya Ubunge yalikuwa 53 na Udiwani 196. Hadi kufikia Desemba 30, 2016 mashauri 52 yaliyohusu ubunge yaliamuliwa, hivyo kubaki na shauri moja (1) tu. Mashauri ya udiwani yalisikilizwa na kuamuliwa yote. Mashauri ya uchaguzi wa Ubunge yalisikilizwa mfululizo kuanzia mwezi Juni mpaka Oktoba, 2016 yakijumuisha Majaji 29 kwa yale ya Ubunge; na Mahakimu kwa mashauri ya Udiwani.

Ari hii ya Kasi ya usikilizwaji wa Mashauri mbalimbali, ilimfurahisha Mhe. Rais na kupelekea kutoa pongezi kwa Mahakama kwa kazi nzuri waliofanya katika mwaka wa Mahakama uliopita.

Mbali na pongezi, Mhe. Rais alitoa changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na ‘Mashauri ya kodi na fedha zilizokwama kutokana na wadaawa na masjala za Mahakama kufanya mchezo maarufu wa ‘Parking’ kuzuia mashauri yasimalizike na kuikosesha serikali mapato.’ Katika hili Mhe. Rais aliiomba Mahakama kutilia mkazo katika mashauri haya ili kuingizia Serikali mapato.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama na Wageni wengine waalikwa wakiwa katika sherehe za Siku ya Sheria nchini, iliyofanyika Februari 02, 2017.

Hata hivyo; Mahakama pamoja na jukumu lake kuu la kutoa haki,imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha nchi inajenga na kuweka mazingira bora ya biashara shindani ili kuvutia uwekezaji.

Kwa upande wake, Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma, katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini, alisema kuwa Mahakama ya Tanzania imedhamiria kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha wadaawa wanapata nakala ya hukumu ndani ya siku 21 na mwenendo wa shauri ndani ya siku 30 tangu hukumu iliposomwa.

“Wananchi wanastahili kupata nakala za hukumu kwa wakati. Sheria inataka kila Jaji au Hakimu asome hukumu ndani ya siku 90 tangu kesi ilipomalizika kusikilizwa,” alisisitiza Kaimu Jaji Mkuu.

Miongoni mwa masuala ambayo Kaimu Jaji Mkuu aliyatilia msisitizo/mkazo katika hotuba yake pia ni pamoja na matumizi ya TEHAMA Mahakamani ili kurahisisha taratibu mbalimbali za Mahakama.

“Ifikapo Desemba, 2018, kulingana na ramani (Road map) ya matumizi ya TEHAMA, kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (E-govt Agency), tuweze kuanza matumizi kamili ya TEHAMA kwenye kazi za Kimahakama na Kiutawala,” alisema Jaji Juma.

Aliongeza kuwa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kisasa ya Mahakama pia unaenda sanjari na matumizi ya hatua kwa hatua ya TEHAMA, vilevile kuhakikisha taratibu za masuala ya fedha ndani ya Mahakama zinaendeshwa kwa kutumia mifumo ya kisasa ya TEHAMA mpaka kwenye ngazi ya Mikoa/Wilaya.

Alienda mbali na kuongeza kuwa Mfumo wa TEHAMA wa ukusanyaji wa Takwimu za Mashauri (JSDS) utaboreshwa kuwa sehemu ya mfumo wa kisasa. Matumizi makubwa ya Watanzania ya simu za kisasa (smart phone) yanarahisisha sana azma hii ya kuleta mabadiliko makubwa ya utendaji kazi wa kizamani na wenye tija hafifu.

Jitihada mbalimbali zifanywazo na Mahakama kwa sasa kama ujenzi na ukarabati wa miundombinu, matumizi ya TEHAMA n.k zinalenga katika kuboresha na kusogeza huduma ya utoaji haki kwa wananchi.

Naye, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju katika hotuba yake ya Siku ya Sheria nchini aliitaka Mahakama kukamilisha mapema mashauri ya jinai, Rushwa na Uhujumu Uchumi ambayo yanaendeleza amani na usalama katika jamii ni chachu ya maendeleo ya uchumi.

“Majaji, Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa Serikali, Mawakili wa Kujitegemea na wadau wengine wa Mahakama, ikiwemo vyombo vya upelelezi wa jinai, Rushwa na Uhujumu uchumi, Mabaraza ya kodi, Ardhi, Ushindani na mengineyo wazingatie matakwa ya Katiba ya nchi, Sheria na Kanuni katika utoaji haki kwa wakati,” alieleza Masaju.

Siku ya Sheria nchini, hutoa nafasi kwa Mahakama pamoja na wadau wake wakuu ambao ni Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Chama cha Mawakili Tanganyika kutoa hotuba juu ya Mafanikio na changamoto zinazoikabili Sekta ya Sheria katika mwaka husika.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika, Bw. John Seka aliihakikishia Mahakama kupitia hotuba yake kuwa Chama hicho kipo tayari wakati wowote kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha kuwa utoaji haki unatamalaki.

Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini hutumika kama njia mojawapo ya kukutana na Wadau ili kupata michango/maoni mbalimbali ya Wadau na wananchi kwa ujumla yote yakitumika na Mahakama kujitathmini na kuona wapi imepwaya ili kuendelea kufanya maboresho katika suala zima la utoaji haki nchini.

Akiongea na Mwandishi wa Makala hii, Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati alisema kwa mwaka huu mpya wa Sheria, Mahakama imejipanga kuhakikisha inaendelea kushughulikia mlundikano wa kesi/mashauri ya muda mrefu ‘case backlog’.

“Kama unavyojua kwa sasa, Mahakama imejikita katika kufanya maboresho kadhaa wa kadhaa, miongoni mwa maboresho hayo ni pamoja na kushughulikia mashauri ya muda mrefu, na jitihada hizi zimezaa matunda hata kwa mwaka jana ambapo hadi tunamaliza mwaka tulikuwa mlundikano sifuri (zero cases) katika ngazi za Mahakama za Mwanzo na za Wilaya,hivyo jitihada hizi zinaendelea hata kwa sasa,” alieleza Mhe. Revocati.

Msajili Mkuu huyo aliendelea kusema kuwa Mahakama imejiwekea muda maalum wa kushughulikia kesi hadi kumalizika kwake, ambapo alieleza kuwa kwa ngazi ya Mahakama za Mwanzo kesi inabidi iwe imekamilika kwa kipindi cha miezi sita, Mahakama za Wilaya/Hakimu Mkazi, mwaka mmoja na kwa upande wa Mahakama Kuu/Rufani miaka miwili (2), na suala hili tunalisimamia kwani pia Mpango Mkakati wetu wa Mahakama kupitia moja ya nguzo zake inaelekeza kuboresha suala zima la utoaji haki nchini.

Mahakama ya Tanzania huadhimisha Siku ya Sheria nchini ndani ya wiki ya kwanza wa mwezi Februari kila mwaka, siku hii huashiria mwanzo wa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika, maudhui ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini kwa mwaka huu ni ‘Umuhimu wa Utoaji Haki kwa wakati kuwezesha Ukuaji wa Uchumi.’

Kwa mara ya kwanza, Mahakama ya Tanzania iliadhimisha rasmi Siku ya Sheria nchini mwaka 1997 ambapo Viongozi wa Dini walitoa dua ya kuombea Majaji, Mahakimu na Wanasheria ili watimize wajibu wao mzito wa utoaji haki nchini. Hata hivyo mnamo Machi 1, 1996 kulifanyika ibada maalum ya kuwaombea Majaji na Mahakimu ili wasikilize vyema mashauri yoyote na hasahasa ya uchaguzi Mkuu uliofanyika 1995. Huu ulikuwa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi na hivyo kulikuwa na mashauri mengi ya uchaguzi.

Aidha; mnamo mwaka 2007, Sherehe za Siku ya Sheria nchini zilihudhuriwa na Mheshimiwa Rais kwa mara ya kwanza na Mheshimiwa Rais alipata nafasi ya kutoa hotuba na huu ndio ulikuwa mwanzo wa mgeni rasmi kutoa hotuba.

No comments: