Friday, February 10, 2017

HOTUBA YA MHE. WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA SITA WA BUNGE

HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SITA WA BUNGE LA KUMI NA MOJA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 10 FEBRUARI, 2017


UTANGULIZI:

1.           Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehma kwa kutujaalia afya njema na kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Sita wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 31 Januari, 2017. Mwenyezi Mungu ameendelea kuitikia Dua ya kuliombea Bunge lako Tukufu kwa kutuongezea hekima na maono kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania. Tumshukuru kwa Baraka hiyo!

MAJANGA MBALIMBALI

2.           Mheshimiwa Spika, wakati mkutano huu ukiendelea, wapo Watanzania wenzetu waliokutwa na masahibu mbalimbali kama vile mafuriko yaliyotokea wilayani Mpwapwa, kimbunga huko Njombe, Ileje na Nyamagana, ajali ya treni eneo la Ruvu mkoani Pwani. Aidha, zimekuwepo ajali mbalimbali za barabarani. Hivyo, napenda kutumia fursa hii kutuma salamu zangu za pole kwa wale wote waliopoteza wapendwa wao na kuwaombea uponaji wa haraka kwa wale waliopata majeraha kwenye ajali hizo.

3.           Mheshimiwa Spika, aidha itakumbukwa kuwa tarehe 26 Januari, 2017 ilitokea ajali ya kuporomoka kwa kifusi katika machimbo ya dhahabu ya Nyarugusu, mkoani Geita ambapo vijana wetu 15 waliofukiwa na kifusi kwenye machimbo hayo waliokolewa. Ninawashukuru na kuwapongeza kwa ujasiri na uzalendo wa hali ya juu waliofanikisha uokoaji huo. Yapo mambo mengi tunayoweza kujifunza kutokana na ajali hiyo, na hususan hatua za kuchukua kuzuia ajali kama hizo kujitokeza siku zijazo na jinsi ya kufanya uokoaji pindi zikitokea. Natoa rai, kwa kila Taasisi inayohusika, ifanyie kazi funzo ililolipata kwenye zoezi hili, ili kuepuka ajali za migodini, na endapo zikitokea, kuwepo na utayari katika uokoaji.

Pongezi na teuzi mbalimbali

4.           Mheshimiwa Spika, kwenye Mkutano huu, Bunge lako Tukufu limepokea na kuwaapisha Wabunge wapya wanne, ambao ni Mheshimiwa Abdallah Majura Bulembo (Mb), Mheshimiwa Anne Killango Malecela (Mb), Mheshimiwa Juma Ali Juma (Mb) na Mheshimiwa Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb). Ninawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wapya kwa heshima waliyoipata ya kujumuika nasi kwenye Bunge lako Tukufu. Kama ilivyo ada, naamini wote tutatoa ushirikiano unaotarajiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wapya ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na tija.

5.           Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Prof. Ibrahim Juma, kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais, kuwa Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania. Sina shaka Mheshimiwa Jaji Prof. Juma ataendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya mhimili wa mahakama na mihimili mingine ya dola, kama alivyokuwa mtangulizi wake Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mohammed Chande Othman. Serikali inaahidi kumpa ushirikiano unaostahili ili aendeleze maboresho kwenye mhimili huo yaliyoanzishwa na mtangulizi wake.

6.           Mheshimwa Spika, tarehe 2 Februari 2017, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, alimteua Jenerali Venance S. Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange ambaye amestaafu. Nitumie fursa hii kumpongeza Jenerali Mabeyo kwa uteuzi huo na kumshukuru Jenerali Mwamunyange kwa kulitumikia Taifa kwa uzalendo na uadilifu mkubwa.

SHUGHULI ZA BUNGE

7.           Mheshimiwa Spika, tunapohitimisha mkutano huu, tumeweza kukamilisha mjadala wa miswada miwili, kupokea Kauli za Mawaziri mbili na taarifa 14 za Kamati za Kudumu za Bunge. Itakumbukwa kuwa, awali Serikali ilipanga kuwasilisha miswada mitatu ikiwemo Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno, na Wataalamu wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016 (the Medical, Dental and Allied Health Professionals Bill, 2016), lakini tukaomba kuuondoa ili tuendelee kujipanga vizuri zaidi. Hivyo, miswada iliyojadiliwa na kupitishwa na Bunge lako tukufu kwenye mkutano huu ni ifuatayo:-

(i)         Muswada wa Sheria ya Huduma ya Msaada wa Kisheria wa Mwaka 2016 (The Legal Aid Bill, 2016) na

(ii)        Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 4 wa Mwaka 2016 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (Na.4) Bill, 2016].

8.           Mheshimiwa Rais, Miswada hii ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu, hivyo nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri kwa maslahi ya Taifa letu. Aidha, nitumie fursa hii kumpongeza Mwanasheria Mkuu wa Serikali na watendaji wote kwa kazi nzuri ya maandalizi ya Miswada hiyo. Nawasihi Waheshimiwa Mawaziri wanaohusika na Miswada iliyopitishwa, wasimamie utayarishaji wa kanuni za sheria hizo zilizopitishwa pindi Mheshimwa Rais atakaporidhia, ili utekelezaji uanze mara moja.  

9.           Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali ya msingi, ya nyongeza na ya papo kwa papo yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali.

10.        Mheshimiwa Spika, Mkutano huu pia ulipokea na kujadili taarifa mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge; na kutolewa kauli mbili za Mawaziri kuhusu hali ya chakula nchini na deni la Taifa na hali ya uchumi. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuwasilisha kwa umakini na umahiri mkubwa taarifa za kamati zao pamoja na kuzihitimisha. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango, maoni na ushauri wao mzuri walioutoa wakati wa mijadala yote ya taarifa hizo.

11.        Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kukushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Wataalam wetu kwa kufanikisha kazi zote zilizokuwa zimepangwa kwenye mkutano huu tena kwa ufanisi mkubwa. Nawashukuru na kuwapongeza sana! Nawapongeza pia na kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa maelezo mazuri ya ufafanuzi waliyotoa katika kujibu baadhi za Kamati za Kudumu za Bunge na zile zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge binafsi au kwa ujumla wao. Napenda kuahidi kuwa Serikali itazingatia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge pamoja na mapendekezo mliyotoa kwenye kamati husika.

HOJA ZA KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE

12.        Mheshimiwa Spika, naomba nami uniruhusu nitumie fursa hii kutoa maelezo mafupi ya msisitizo kuhusu baadhi ya hoja zilizojitokeza katika Mkutano huu wa Bunge.

Vita dhidi ya Dawa za Kulevya

13.        Mheshimiwa Spika, moja ya eneo lililojadiliwa na kuibua hisia kali ni kuhusu vita inayoendelea Nchini dhidi ya dawa za kulevya. Watanzania wote ni mashahidi kwamba vijana wetu wengi wameendelea kudhoofisha afya zao kutokana na matumizi ya dawa za kulevya. Dawa za kulevya ni hatari sana kwa usalama na ustawi wa Taifa letu. Vita hii inayopiganwa sasa dhidi uagizaji, uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kubwa. Sote tunapaswa kuunga mkono jitihada hizo.

14.        Mheshimiwa Spika, Kitaalamu, madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya dawa za kulevya ni mengi ikiwa ni pamoja na kuathirika kwa mfumo wa fahamu kwa mtumiaji ikiwamo kuchanganyikiwa, kuwa na ulevi usioponyeka kirahisi na kusababisha kifo kama mtumiaji atazidisha matumizi ya dawa za kulevya. Madhara ya kiuchumi ni pamoja na gharama kubwa za kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya, gharama kubwa za uchunguzi wa kimaabara kwenye Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na watumiaji wa dawa za kulevya kushindwa kujisimamia na kuendesha maisha yao wao wenyewe.

Aidha, takwimu za jumla za Watanzania waliokamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya ni kama ifuatavyo:-
·         Nchini China Watanzania walio magerezani ni zaidi ya 200;
·         Nchini Brazil Watanzania 12;
·         Nchini Iran Watanzania 63;
·         Nchini Ethiopia Watanzania 7; na
·         Nchini Afrika Kusini Watanzania 296.

Madawa ya kulevya hapa nchini, huingia zaidi kutumia njia za bandari bubu kupitia Bahari ya Hindi na mipaka yetu kwa njia ya magari binafsi na mabasi kupitia nchi za Kenya, Uganda na mpaka wa Tunduma.

15.        Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kuwasaidia walioathirika na dawa za kulevya na kuwachukulia hatua kali wale waliowaathiri kwa maana ya wauzaji na wasambazaji. Tunashukuru kwamba Watanzania wengi na Waheshimiwa Wabunge pia mmetoa mchango mkubwa na ushauri wa namna nzuri zaidi ya kupambana na janga hili. Dhamira ya Serikali ni kupambana na janga hili kwa dhahiri na kwa dhati bila kumuonea mtu yeyote na kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki.

Utaratibu wa utoaji Mikopo ya Elimu ya Juu

16.        Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyovuta hisia za Waheshimiwa Wabunge wengi ni kuhusu utaratibu wa utoaji wa Mikopo ya Elimu ya Juu. Mheshimiwa Spika, suala hili ni pana na linagusa familia nyingi za Watanzania, na hususan walio maskini. Hivyo, Serikali imeunda Kamati ya Wataalam ambao wanaupitia upya utaratibu wa sasa kwa lengo la kupendekeza vigezo muafaka kwa kuzingatia changamoto zilizopo. Azma ya Serikali ni kuanza utekelezaji wa vigezo vilivyoboreshwa katika upangaji na utoaji wa mikopo kuanzia mwaka wa masomo wa 2017/18. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha urejeshwaji mikopo hii kwa wakopaji ili kuongeza fedha kwa ajili ya kugharamia wanufaika wapya wa mikopo ya elimu ya juu ili kupunguza utegemezi kutoka katika bajeti ya Serikali.

Uhakiki wa Watumishi na madai ya Watumishi

17.        Mheshimiwa Spika, kulikuwa pia na hoja kuhusu uhakiki wa watumishi na madai ya watumishi. Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, zoezi la uhakiki wa watumishi hewa limekamilika, kinachoendelea sasa ni uhakiki wa vyeti vya kitaaluma. Kuhusu madeni, Mkaguzi wa Ndani wa Serikali amefanya uhakiki wa madai mbalimbali ya watumishi wa umma ya hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016. Katika mwaka wa fedha 2016/17, Serikali imeanza kulipa madeni hayo ambapo hadi sasa Serikali imelipa shilingi bilioni 42.35 kwa watumishi wasiokuwa walimu. Aidha, kwa upande wa walimu, Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 23.458 kwa walimu 63,955 kwa kipindi cha mwaka 2015/16 na mwaka 2016/17. Serikali itaendelea kulipa madeni yote ya waumishi wa umma yaliyohakikiwa.

18.        Mheshimiwa Spika, hoja nyingine muhimu iliyojadiliwa sana na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusu utawala bora hususan mipaka ya kimadaraka kati ya mihimili mikuu ya nchi yaani Serikali, Bunge na Mahakama. Mheshimiwa Spika, dhana ya mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili ya dola imewekwa wazi kwa mujibu wa Ibara ya 4(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Utekelezaji wa majukumu ya mihimili hiyo unategemea sana viongozi na watendaji wake kuheshimiana, kuvumiliana na kufanya kazi zao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa. Shabaha kuu ni kuwaletea wananchi maendeleo hivyo tuepuke misuguano isiyo na tija ambayo inatuondoa katika lengo la kufanya shughuli za maendeleo.

SEKTA YA AFYA

Hali ya Upatikanaji wa Dawa Nchini

19.        Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa dawa nchini inaendelea kuimarika kufuatia kutolewa kwa wakati fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Mathalan, kiasi cha shilingi bilioni 91 kimeshatolewa, kati ya shilingi bilioni 251 zilizotengwa, sawa na wastani wa shilingi bilioni 20 kila mwezi. Haya ni mafanikio makubwa na ni dhamira njema ya Serikali katika kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini. Mafanikio haya ni tofauti na miaka ya nyuma ambako tulipeleka chini ya shilingi bilioni 10.

Ununuzi wa Dawa kutoka wa Wazalishaji

20.        Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tukieleza kuhusu dhamira ya Serikali ya kununua madawa na vifaa tiba moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya mawakala. Napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba, utaratibu huo umeanza na tayari Serikali imekamilisha taratibu za kimkataba na wazalishaji watano (5) wakubwa wa ndani kwa ajili ya kununua baadhi ya dawa kutoka ndani ya nchi, wakati mikataba mingine 76 ya wazalishaji wa nje iko katika hatua za mwisho. Matarajio yetu ni kwamba, utekelezaji wa mikataba ya nje utaanza katika mwaka wa fedha 2017/18.

21.        Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ya kusambaza dawa kwa wakati kwenye Halmashauri zetu haitafanikiwa endapo Halmashauri zitachelewa kuwasilisha maoteo ya dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Hivyo, Halmashauri zote nchini, zinaagizwa kufanya maoteo na kuyawasilisha Bohari Kuu ya Dawa kabla au ifikapo tarehe 05 Machi 2017. Aidha, naomba kutoa rai yangu kwa Waheshimiwa Wabunge, kupata wasaa wa kufuatilia mchanganuo wa usambazaji dawa katika Halmashauri zenu ambao hutolewa na Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Jitihada za usambazaji dawa pia zinafanywa na Maduka ya Dawa yanayoendelea kujengwa sehemu mbalimbali nchini. Shabaha yetu ni kwamba, ifikapo mwezi Juni, 2017 usambazaji wa dawa muhimu nchini kote uwe umefikia asilimia 85.

Bima ya Afya kwa wote

22.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na maboresho kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), ambayo yatamwezesha mwanachama kupata huduma kutoka ngazi ya Zahanati hadi ngazi ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Katika maboresho hayo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utabaki na jukumu la kununua huduma (Purchaser) wakati Halmashauri zitakuwa na jukumu la kutoa huduma (Provider) tofauti na ilivyo sasa. Kwa kuanzia, Mpango huu utatekelezwa katika Halmashauri 50 katika Mikoa ya Ruvuma, Kagera, Mwanza, Mara, Singida, Tabora na Pwani ambapo Mpango huu utazinduliwa rasmi mwishoni mwa mwezi Februari, mwaka 2017.

23.        Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mwelekeo huo wa Serikali, ni vema sasa Waheshimiwa Wabunge kupitia Halmashauri zetu mkaanza kuwaandaa wananchi kupokea mpango huu wa bima ya afya kwa kila mwananchi. Aidha, anzeni kutafakari namna bora zaidi ya kutekeleza mpango huo katika muktadha na mazingira ya nchi yetu.

Uhaba wa Watumishi Katika Sekta ya Afya

24.        Mheshimiwa Spika, kuna kilio kikubwa cha uhaba wa watumishi kwenye sekta ya afya. Jambo hili tunalifahamu na kwa hakika linatugusa sote. Kama ambavyo tumeanza kwa kutangaza ajira 4,348 za walimu wa masomo ya sayansi pia tutaajiri Watumishi wa kada ya afya na kada zingine.

SEKTA YA ELIMU

Uandikishaji wa wanafunzi kwa mwaka 2017

25.        Mheshimiwa Spika, huu ni mwanzo wa mwaka 2017, tunayo matarajio ya uandikishaji wa wanafunzi wa awali, Msingi na pia kwa Sekondari, Kidato cha Kwanza. Zoezi la uandikishaji katika Kidato cha Kwanza linaendelea na linatarajiwa kufungwa tarehe 28 Februari, 2017. Naomba nitumie fursa hii, kuziagiza Halmashauri zote nchini, kuongeza kasi ya uandikishaji kwa shule za sekondari, usajili wa darasa la kwanza na pia ujenzi wa vyumba vya madarasa ili wanafunzi wote wanaostahili kuandikishwa au kuendelea na ngazi inayofuata katika shule wasipoteze fursa hiyo kutokana na ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Elimu kwa Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum
26.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kutoa elimu bora kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule. Kutokuwepo kwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu imekuwa ni changamoto kwao katika kujifunza kwa ufanisi. Ili kuboresha upatikanaji, ushiriki na usawa katika elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, Serikali imenunua vifaa vya kielimu na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, kuona na wenye ulemavu wa akili. Vifaa hivyo vinajumuisha mashine 932 za maandishi ya nukta nundu, rimu za karatasi za breli zipatazo 2,548 na shime sikio (hearing aids) 1,150. Aidha, katika kuhakikisha kwamba tunatekeleza dhana ya elimu jumuishi, Serikali imenunua pia vifaa kwa ajili ya upimaji ili kubaini mahitaji mbalimbali ya ujifunzaji kabla na baada ya usajili wa watoto katika shule za msingi. Vifaa hivyo vinajumuisha pia vifaa vya upimaji kwa ajili ya masikio; vifaa vya upimaji wa macho; na vifaa vya upimaji wa mtindio wa ubongo.
27.        Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa vifaa vya watoto wenye mahitaji maalum ambavyo vimegharimu kiasi cha Shilingi bilioni 3.6 vimekwishapokelewa na vitasambazwa katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji hayo kuanzia tarehe 1 Machi, 2017.

Natoa wito kwa Maafisa Elimu na walimu wote wanaofundisha wanafunzi wetu wenye mahitaji maalum kutumia ipasavyo vifaa hivyo. Aidha, wazazi wa watoto wenye mahitaji maalum wawapeleke watoto wao shule, badala ya kuwaficha majumbani.

Upatikanaji wa Vitabu vya Elimu ya Msingi na Sekondari

28.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada zake za kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia na hadi sasa Serikali imefanikiwa kusambaza Nakala 6,862,800 kwa vitabu vya kiada kwa Darasa la kwanza vya Mtaala ulioboreshwa kwa shule zote za msingi Tanzania Bara. Aidha, uchapaji wa vitabu vya Darasa la pili Nakala 6,862,800 unaendelea na uchapishaji wa Nakala 6,818,181 za Darasa la Tatu umekamilika. Nakala hizo za Darasa la Tatu zitasambazwa sambamba na Vifaa vya Darasa la Pili.

Kwa upande wa shule za Sekondari, Nakala 2,109,683 zimechapishwa na usambazaji umeanza tarehe 07 Februari, 2017. Natoa wito kwa Walimu wote Nchini na Wanafunzi kutunza vizuri vitabu hivyo ili vitumike kwa muda mrefu.

Usambazaji wa vifaa vya maabara

29.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mpango Maalum wa kukuza na kuimarisha ufundishaji wa masomo ya sayansi nchini. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali ilihamasisha ujenzi wa maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali imeagiza vifaa vya Maabara kwa ajili ya Shule 1,625 za Sekondari nchini. Hadi sasa Asilimia 70 ya vifaa hivyo imekwishawasili nchini na usambazaji wake umeanza hivi karibuni katika Kanda ya Dar es Salaam. Natoa wito kwa Wakuu wa Shule kuweka utaratibu mzuri wa kutunza vifaa hivyo ili viweze kudumu. Aidha, ni matumaini yangu kwamba vifaa hivyo vitakuwa ni chachu ya wanafunzi kuchangamkia masomo ya sayansi na hivyo kulifanya Taifa letu kutengeneza wanasayansi wengi zaidi.


ELIMU YA JUU

Ubora wa Elimu ya Juu

30.        Mheshimiwa Spika, mwishoni mwa mwaka 2016, Serikali, kupitia Tume ya Vyuo Vikuu, ilifanya uhakiki wa ubora wa elimu kwa Vyuo Vikuu vyote nchini. Matokeo ya uhakiki huo yatatumika katika kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha elimu ya juu ili kupandisha viwango vya taaluma ya wahitimu. Uhakiki huo utakuwa unafanyika kila baada ya miaka mitatu ili kuhakikisha ubora wa elimu inayotolewa unalingana kote nchini.

31.        Mheshimiwa Spika, sanjari na jitihada hizo, kuanzia mwaka wa fedha 2017/18, Serikali itaweka Viwango vya Ulingalifu (Benchmark Standards) vya kuainisha kozi zinazotakiwa kusomwa katika nyanja za ualimu, udaktari wa binadamu, sheria na biashara. Matarajio yetu ni kwamba jitihada hizi na nyingine zitakazokuwa zinaendelea kufanyika zitasaidia kuboresha elimu ya juu kwa kiasi kikubwa.

SEKTA YA KILIMO

Hali ya Upatikanaji wa chakula nchini

32.        Mheshimiwa Spika, kama ilivyoelezwa katika Kauli ya Serikali kuhusu hali ya chakula na lishe hapa nchini kwa mwaka 2016/2017, baadhi ya maeneo katika Halmashauri 55 yana upungufu wa chakula na bei za vyakula hasa nafaka kwenye masoko katika Halmashauri hizo imeendelea kupanda. Mheshimiwa Spika, leo sikusudii kurudia maelezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na sekta ya kilimo bali kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahamasisha wananchi kulima mazao yanayokomaa mapema kwa kutumia mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mengi hapa nchini. Pili, kuwashauri wananchi kutumia vizuri chakula walicho nacho na kuwasihi wafanyabishara wasifiche chakula bali wasaidie kuchukua chakula kutoka kwenye maeneo yenye chakula cha ziada na kukisafirisha kwenda kuuza kwenye maeneo yenye upungufu.

SEKTA YA MIFUGO
Upatikanaji na Usambazaji wa Mbegu Bora za Mifugo
33.        Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto ya migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, Serikali inahimiza wananchi kuondokana na mazoea ya uchungaji na kujikita zaidi katika ufugaji wa kisasa ambao utawawezesha kuwa na mifugo michache yenye ubora ambayo itawaongezea tija katika uzalishaji wa nyama na maziwa mengi zaidi kwa ng’ombe mmoja. Hivyo, Serikali kupitia mashamba ya mifugo na vituo vya taasisi za Serikali vilivyoko katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu itaendelea kuhakikisha kuwa mbegu bora za mifugo zinazalishwa kwa ajili ya uhamilishaji, na mitamba na madume bora yanazalishwa kwa wingi na kusambazwa ili kukidhi mahitaji ya wafugaji wetu.

34.        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha Taasisi zinazoagiza mbegu za mifugo kutoka nje ya nchi kama vile Heifer Project International (HPI) na SAGCOT - Catalytic Trust Fund (CTF) na kwa kushirikiana na mashamba makubwa ya kisasa ya sekta binafsi ili wafugaji wawe na wigo mpana wa kuchagua aina bora zaidi za mifugo. Hivyo, natoa rai kwa wananchi kuchangamkia fursa hiyo kwa kushiriki katika ufugaji wa kisasa.

Upatikanaji na Usambazaji wa Mbegu Bora za Malisho

35.        Mheshimiwa Spika, kuna uhusiano mkubwa kati ya ufugaji bora na upatikanaji wa malisho bora. Hivyo, Serikali itaendelea kuboresha na kuendeleza mashamba ya mbegu za malisho ya mifugo yaliyo chini ya Serikali katika maeneo mbalimbali nchini. Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwaagiza Maafisa Ugani wa mifugo katika Halmashauri zote nchini, kufungua mashamba darasa ya kuzalisha mbegu hizo na kuhamasisha wafugaji kupanda malisho katika maeneo yao na kutoa stadi za ufugaji bora na wa kisasa. Baada ya miaka mitatu Wizara husika ifanye tathmini ya utekelezaji wa agizo hili na kuwasilisha taarifa kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu.

SEKTA YA ARDHI

Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi
36.        Mheshimiwa Spika, katika kuongeza juhudi za kudhibiti migogoro ya matumizi ya ardhi inayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, katika Mwaka Fedha 2016/17, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi imeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji 50 katika Wilaya 19 na kuandaa Hatimiliki za Kimila 1,361 katika Wilaya ya Mvomero; hatimiliki 2,943 katika wilaya za Mkuranga (297); Ikungi (957); Karagwe (1,099) na Nachingwea (590). Aidha, Serikali imeandaa hatimiliki za kimila 44 za nyanda za malisho za wilaya za Monduli, Ngorongoro, Hanang, Simanjiro na Karatu. Hadi sasa jumla ya vijiji 1,690 vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi ambayo imeainisha pia matumizi ya kilimo na ufugaji ikilinganishwa na vijiji 12,545 vilivyopo nchini. Vilevile, upimaji wa mipaka ya vijiji 53 umefanyika katika Wilaya ya Kilombero (Vijiji 7) na Ulanga (Vijiji 5).

Upimaji na Utoaji wa Hati katika Maeneo yote ya Umma

37.        Mheshimiwa Spika, ili kulinda maeneo ya umma, ikiwemo sehemu za huduma kama vile Shule, Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali, Vyuo, Ofisi, Vituo vya Polisi, Mahakama, Maeneo ya Majeshi, Mashamba ya serikali, Hifadhi za Misitu na Wanyama Pori, Maeneo ya Makumbusho na kadhalika dhidi ya uvamizi, Serikali inaendelea na upimaji wa maeneo hayo na kuyapatia hati miliki. Aidha, Wizara zote Tanzania bara zinaagizwa kuhakikisha kuwa maeneo wanayoyamiliki na yale yaliyoko chini ya taasisi zao yanapimwa na kuandaliwa hatimiliki.

38.        Mheshimiwa Spika, ili kuharakisha zoezi la upimaji, upangaji na utoaji wa Hatimilki za maeneo ya umma, Serikali imeelekeza Wizara/taasisi za umma kutumia wapima wa Serikali au wapima binafsi waliosajiliwa na Bodi ya Wapima Ardhi nchini, yaani National Council of Professional Surveyors (NCPS) kupima maeneo yao kwa kugharimia upimaji wa maeneo hayo. Nitumie fursa hii kuzipongeza baadhi ya taasisi ambazo zimeanza kutekeleza maelekezo hayo, ambazo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mahakama Kuu ya Tanzania na baadhi ya sekretarieti za mikoa.

Mpango wa Uwekaji Mawe/Alama za Mipaka Kwenye Hifadhi na Mapori ya Akiba

39.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa kulinda usalama wa maeneo ya hifadhi na mapori ya akiba kwa kuweka mawe ya mipaka yanayoonekana, yaani Pillars, ili kuzuia uvamizi na uharibifu wa maeneo hayo kwa kushirikisha wadau wa mipaka hiyo. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakiki mipaka ya maeneo ya hifadhi na kuweka alama za mipaka.

40.        Mheshimiwa Spika, aidha Serikali imeendelea kushughulikia migogoro ya mipaka ya vijiji, wakulima na wafugaji, wanavijiji na hifadhi na mapori ya akiba inayoibuka hapa nchini. Ili kukabiliana na changamoto hii, Serikali iliunda Kamati Maalum ya kisekta ya kushughulikia migogoro ikijumuisha watendaji wa sekta mbalimbali zinazohusika kwa njia moja au nyingine kwenye masuala ya migogoro ya ardhi. Kamati hiyo tayari imepokea na kuchambua migogoro yote iliyowasilishwa kutoka Halmashauri mbalimbali nchini; na kutembelea wilaya zenye viashiria vya migogoro. Baada ya zoezi hilo kukamilika, Serikali itawasilisha taarifa ya hali ya migogoro na hatua iliyofikiwa ya utatuzi wa migogoro hiyo nchini.

41.        Mheshimiwa Spika, nimekwishatoa maelekezo mahsusi kwa Halmashauri mbalimbali na ninaomba kutumia Bunge lako Tukufu kurejea maelekezo yangu kuhusu migogoro ya mipaka kati ya Kijiji na Kijiji, Vijiji na Hifadhi, au Wilaya na Wilaya. Kwa migogoro ya mpaka kati ya Kijiji na Kijiji, maelekezo ya Serikali ni kwamba, migogoro hiyo imalizwe kupitia vikao vya vijiji husika na wataalamu wa Halmashauri wasaidie katika kumaliza migogoro hiyo. Migogoro kati ya vijiji na Hifadhi, au Wilaya na Wilaya, migogoro hiyo itatuliwe kwa kuangalia Mipaka halali inayotambuliwa na Government Notice (GN) na Wataalamu wa Upimaji na Ramani wa Halmashauri au wale wa Wizara ya Ardhi wasaidie kubainisha mipaka hiyo iliyowekwa na Serikali miaka iliyopita na kusuluhisha pande zote mbili. Nazisihi Halmashauri zote nchini zizingatie mwongozo huo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima.

KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO YA WANANCHI
42.          Mheshimiwa Spika, katika ziara mbalimbali ninazofanya Mikoani, nimebaini uwepo wa malalamiko mengi ya wananchi ambayo hayashughulikiwi kwa wakati katika ngazi za Vijiji, Mitaa na Kata. Aidha, nimebaini kuwa mikutano ya Vijiji, Kata na Mitaa imekuwa haifanyiki kama inavyotakiwa kisheria na hivyo kufanya kero nyingi kutopatiwa ufumbuzi.

43.          Mheshimiwa Spika, suala la kutotatua kero za wananchi katika ngazi ya Serikali za Mitaa ni kinyume na dhamira ya Serikali ya kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi. Aidha, ni kinyume na msimamo wa Ibara ya 146 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  inayotamka kama ifuatavyo, naomba kunukuu;
“Madhumuni ya kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki na kuwashirikisha wananchi katika mpango wa shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika Serikali zao na nchi kwa ujumla”. Mwisho wa kunukuu.
44.        Mheshimiwa Spika, Sheria ya Serikali za Mitaa inaelekeza kuitishwa kwa Mikutano Mikuu ya Vijiji kila baada ya miezi mitatu. Sheria pia inatoa fursa ya kuitishwa kwa mikutano ya dharura, endapo ipo haja ya kufanya hivyo.

45.      Mheshimiwa Spika, kutokana na msimamo huo wa kisheria na kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero za wananchi, suala la utatuzi wa kero za wananchi halitakiwi kuendelea kusubiri ziara za viongozi, badala yake, kero hizo zitatuliwe kwenye ngazi zinazohusika na zitatuliwe kwa wakati. Kwa muktadha huo, naomba kutumia Bunge lako Tukufu kusisitiza mambo yafuatayo:-

 Mosi:          Watendaji wa Kata, Vijiji na Mitaa wanakumbushwa kuitisha Mikutano ya kisheria ya Viijiji na Kata na Mitaa na kusoma taarifa za mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo katika maeneo yao. Wakurugenzi wa Halmashauri nao wanaagizwa kusimamia kikamilifu uitishaji wa Mikutano Mikuu ya Vijiji na Mitaa kwa mujibu wa Sheria na kuchukua hatua dhidi ya Viongozi wote watakaoshindwa kutekeleza sharti hilo la kisheria. Tembeleeni vijiji kusikiliza kero za wananchi.
Pili:             Viongozi na Watendaji katika ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri wajenge utamaduni wa kuwatembelea Wananchi Vijijini kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi wa papo kwa papo.
HALI YA ULINZI NA USALAMA

46.        Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama nchini ni ya kuridhisha. Vyombo vya ulinzi na usalama viko imara na katika hali ya utayari katika kulinda amani na utulivu. Operesheni za kupambana na uhalifu kama vile unyang’anyi wa kutumia silaha/nguvu, kuteka magari na matishio mengine ya kiusalama vimefanyika katika jitihada za kupambana na uhalifu nchini. Mathalan, katika kipindi cha Julai, 2016 hadi Desemba, 2016, Operesheni Kamata Magendo ilifanyika katika mikoa mbalimbali na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 109 na mali zenye thamani ya Shilingi 388,271,000.

Usalama wa Barabarani

47.        Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Usalama Barabarani kinaendelea na kusimamia usalama barabarani. Pamoja na operesheni hizo, bado kuna ripoti za vifo vinavyotokana na ajali. Licha ya takwimu kuonesha vifo vinavyotokana na ajali kupungua, bado jitihada za makusudi pamoja na umakini katika matumizi ya vyombo vya moto inabidi viongezeke.
Kila mtumia chombo cha moto, aendeshe kwa uangalifu, na Askari wa Usalama Barabarani waendelee kuchukua hatua stahiki kwa wanaovunja sheria za Usalama barabarani ili kuokoa maisha yetu na ya watumiaji wengine wa barabara.


48.        Mheshimiwa Spika, misako na doria zilizofanyika kati ya Julai, 2016 na Desemba 2016 ziliwezesha kukamatwa kwa Watanzania na wageni 6,916 kwa makosa mbalimbali ya kiuhamiaji ikilinganishwa na Watanzania na wageni 3,119 waliokamatwa katika kipindi kama hiki mwaka 2015. Hili ni ongezeko la asilimia 55. Takwimu hizi zinaonesha ama kuongezeka kwa jitihada za kuwasaka wahamiaji haramu na kuwachukulia hatua za kisheria au changamoto hii imeongezeka duniani. Hata hivyo, lazima Idara iendelee kujizatiti. Haiingii akilini kundi la wahamiaji linapita kwenye mikoa zaidi ya mitatu bila kukamatwa!. Ni lazima Idara ya Uhamiaji iendelee kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi.

Udhibiti wa Silaha

49.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na uhalifu wa kutumia silaha haramu. Aidha, imeweka utaratibu wa kuteketeza silaha zote zinazokamatwa ili zisiweze kurudi tena kutumika katika uhalifu. Hivi karibuni jumla ya silaha 5,608 ziliharibiwa huko mkoani Kigoma. Kwa upande mwingine, katika juhudi za kudhibiti uzagaaji holela wa silaha haramu, Serikali inaendelea kufuatilia mpaka ya Kigoma na Kagera ili kudhibiti silaha na uhamiaji haramu. Serikali ilifanya zoezi la kuhakiki silaha zote zinazomilikiwa kihalali, ambapo asilimia 65 ya wamiliki wa silaha walihakikiwa. Natoa rai kwa wamiliki wote wa silaha nchini, ambao bado hawajahakiki silaha zao, wafanye hivyo kabla au ifikapo tarehe 30/06/2017 vinginevyo watapoteza leseni ya umiliki kwa kukiuka Sheria.

50.        Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jukumu la ulinzi na usalama wa nchi yetu, ni la kila mwananchi. Hivyo, natoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutekeleza jukumu hili kwa kuepuka kushiriki hujuma dhidi ya nchi yetu na kwa kutoa taarifa za watu wenye nia mbaya ya kuhatarisha amani na usalama wa nchi yetu.

51.        Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, niruhusu nibainishe masuala matano ya msisitizo, ambayo ninawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwa jumla wayazingatie na wahamasishane katika kuyatekeleza. Masuala hayo ni haya yafuatayo:-

Mosi:       Usalama wa chakula unaanzia katika ngazi ya kaya, kila kaya inatakiwa iwe na utaratibu wa kuwa na chakula cha akiba. Wakati Serikali inaendelea na wajibu wake wa kuwa na hifadhi ya chakula, na kuweka utaratibu wa kutoa chakula penye upungufu, kila mwananchi anao wajibu wa kujiwekea akiba ya chakula cha kaya yake.

Pili:         Dhamira ya kuwa na Bajeti ya kujitegemea kwa asilimia 100 inategemea jitihada zetu za makusanyo ya kodi. Hivyo, kila mwananchi ana wajibu wa kulipa kodi stahiki bila kushurutishwa, na kila mnunuzi anao wajibu wa kudai stakabadhi kwa kila bidhaa anayonunua.  Aidha, kila mwananchi anao wajibu wa kufichua vitendo vya ukwepaji kodi pale anapo pata fununu za vitendo hivyo. Tulipe kodi kwa maendeleo ya nchi yetu.

Tatu:       Tunapoendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia mitaji kwa ajili ya biashara mbalimbali hapa nchini, atakayefanya viwanda na biashara hizi ziwe endelevu ni sisi Watanzania. Hivyo, pamoja na kusisitiza uzalishaji bora, tunalo jukumu la kulinda viwanda na biashara za Tanzania kwa kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Unaponunua bidhaa zilizozalishwa hapa nchini, sio tu unasaidia viwanda hivyo viendelee kuongeza ubora wa bidhaa zao, bali pia unavifanya vizidi kuimarika na kutoa ajira nyingi kwa vijana wa Kitanzania.

Nne:        Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kumtumikia kila Mtanzania popote pale alipo. Kama nilivyoeleza awali, nimebaini baadhi ya kero za wananchi ambazo zingeweza kutatuliwa katika ngazi za Wilaya, zinaletwa kwenye Ofisi za Viongozi wa Kitaifa, au zinasubiri ziara za viongozi hao.

                Nawasihi Viongozi wa Mikoa na Halmashauri, tena tembeleeni vijijini na mtatue kero za wananchi huko vijijini, aidha, hakikisheni Mikutano ya Vijiji iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria inasimamiwa utendaji wake na maazimio yake yanafika kwenye vikao halali vya Maamuzi. Waheshimiwa Wabunge, ninyi ni sehemu ya Halmashauri zenu, nawasihi toeni msukumo unaostahili kwa suala hili.

Mwisho: Mipango ya maendeleo nchini na jitihada za wananchi kujikwamua na umaskini, vitafanikiwa endapo tutaendelea kuwa na umoja na kudumisha amani na utulivu. Hivyo, kila mmoja wetu aendelee kuwa mlinzi wa amani na kuhamasisha ufanyaji kazi kwa bidii na maarifa;

HITIMISHO:

52.        Mheshimiwa Spika, tunaahirisha Bunge lako Tukufu tukiwa na habari njema kwenye tasnia ya michezo ambazo zinatupa nguvu na hamasa ya kuendelea kufuatilia na kuhamasisha uwekezaji kwenye shughuli za michezo na burudani kama moja ya maeneo ya kutengeneza ajira kwa vijana wetu. Kwanza, mwezi Januari, 2017 Mtanzania mwenzetu Alphonce Felix Simbu, aliibuka mshindi kwa kunyakua medali ya dhahabu kwenye mashindano ya riadha ya Dunia ya Mumbai Marathon. Pili, Mtanzania Nasib Abdul, maarufu kama Diamond Platnumz, alipata heshima ya kutumbuiza kwenye ufunguzi wa Fainali za Kombe la Afrika lililomalizika hivi karibuni nchini Gabon, na mwisho, lakini sio mwisho kwa umuhimu, Timu ya Taifa ya Vijana walio chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) imefuzu kwenye Fainali za Kombe la Afrika kwa vijana walio chini ya Umri wa Miaka 17 zitakazofanyika nchini Gabon tarehe 2 – 16 April, 2017. Nitambue juhudi za Bunge Sports Club kuwa ni miongoni mwa timu zilizoshiriki mashindano nchini Kenya. Tuwapongeze waheshimiwa wabunge kwa ushiriki na ushindi wenu na makombe mliyoyaleta.  Ikumbukwe kuwa mwaka huu 2017, Tanzania tutakuwa wenyeji wa mashindani ya mabunge ya Afrika Mashariki. Tupate nafasi ya kujiandaa vizuri na niwaombe wabunge wote tushiriki na hatimaye tuunde timu imara ya Bunge letu. Nitumie Bunge lako Tukufu kuwapongeza wachezaji, Benchi la Ufundi la Bunge Sports Club na Serengeti, TFF na wengine wote waliofanikisha timu zote hiyo kufikia hatua hiyo.

53.        Mheshimiwa Spika vijana wa Serengeti Boys wametimiza wajibu wao na kwa hakika wametutoa kimasomaso kwa kufikia hatua hiyo. Natoa rai kwa Watanzania wote kote ulimwenguni kuiunga mkono timu yetu ili iweze kushindana kikamilifu. Nalishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liwe na maandalizi mazuri na ya mapema, ili Serengeti Boys isiwe mshiriki tu, bali itoe ushindani na kuchukua kombe hilo. Aidha, TFF itumie mashindano hayo kama chachu ya kuongeza msukumo katika soka nchini. Binafsi sifurahishwi sana kuona Taifa letu lenye vipaji lukuki vya michezo ikiwemo soka na riadha ikiwa nyuma Afrika Mashariki.

54.        Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu, kwa kuwaombea Waheshimiwa Wabunge muwe na safari njema mnaporejea majimboni kwenu. Mwenyezi Mungu awajaalie na siha njema katika kipindi chote mtakachokuwa majimboni ili muweze kuchukua maoni ya wananchi mnaowawakilisha kwa lengo la kufikisha maoni yao kwenye Mkutano ujao, ambao utakuwa ni mahsusi kwa ajili ya Bajeti.  

55.        Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 4 Aprili, 2017, siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.


56.        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: