Wednesday, February 22, 2017

Dar es Salaam ya viwanda inawezekana

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya makabidhiano hayo eneo la Kisarawe II wilaya ya Kigamboni leo jijini Dar es Salaam. Picha na Emmanuel Masaka.

Na Benjamin Sawe.
Sekta ya Viwanda na Biashara hutoa ajira kwa asilimia 62 ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam, ambao una jumla ya wakazi 4,364,541 kati yao watu wenye umri wa kufanya kazi (miaka 15 - 64) ni asilimia 66.3 (2,893,691); wengi wao wanafanya kazi za biashara na ajira viwandani.
Awali Tanzania iliweza kutoa ajira kwa vijana wengi kupitia viwanda vyake vya nguo vilivyokuwa katika mikoa mbalimbali kama kile cha Urafiki cha Dar es Salaam na vinginevyo ambavyo hata hivyo kwa sasa viko hoi kutokana na kuhujumiwa na watendaji wasio waaminifu.
Sekta ya viwanda ni sehemu muhimu katika uchumi wa Taifa. Mkoa wa Dar es Salaam una viwanda vingi vya aina mbalimbali kufuatana na bidhaa zinazozalishwa.
Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna bidhaa za aina mbalimbali pamoja na huduma zinazouzwa kwa kiwango kikubwa na kupelekwa nje ya Mkoa.
Bidhaa hizo ni pamoja na zinazozalishwa katika viwanda viliyopo hapa Mkoani na zile zinazoagizwa toka nje ya nchi.
Tanzania haiwezi kubadilika ikiwa mawazo ya watu hayatabadilika katika ujenzi wa viwanda vidogo nchini kote na kuondoa mawazo ya kujenga viwanda vikubwa kama vya wafanyanyabiashara wakubwa, kwa kuwa vinahitaji mtaji mkubwa wakati ajira zake ni chache.
Ama kwa hakika kila mmoja wetu anaifahamu dira na dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya Dr. John Pombe Magufuli ya kuifuta historia yetu ya aibu ya muda mrefu ya kuwa na taifa la wachuuzi kwa kuligeuza kuwa taifa la wazalishaji kupitia kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya kutosha chini ya mwamvuli wa sera ya Tanzania ya viwanda.

Ni kwasababu hiyo tu, watendaji wake aliowaamini na kuwapa  dhamana, hawana budi kuendelea kuwaza zaidi, kutenda zaidi na kushirikisha washirika wengi zaidi ili kwa pamoja waikamilishe  ndoto hii ya Rais wetu mpendwa. 
Ushirikiano baina ya Makonda na Azimio Housing Estate kampuni ambayo imekubali  kutoa eneo lililopo Kigamboni lenye ukubwa wa ekari 1500 la thamani ya zaidi ya bilioni 121 na milioni 470 litakalotumika kama eneo maalumu mbalo litagawiwa kwa wajasiriamali zaidi ya 3,000 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vidogo ni mfano wa kuigwa na kupongezwa kwani hii inaonyesha wazi dhamira ya Mheshimiwa Makonda ya kuwakomboa wajasiriamali wadogo wa jiji la Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengineyo mpango huo unakusudia kuwasaidia wamiliki wa viwanda vidogo kupata maeneo yao ya kufanyia kazi ili kuwapunguzia gharama za kukodi maeneo, kuwaepusha na usumbufu wa kukaa maeneo yasiyo rasmi pamoja na kuwapatia uhakika wa kuwa na anuani (address) za kudumu.
Kutokana na kauli ya Mheshimiwa Makonda kuna matumaini kwamba neema inawajia wanadar es salaam ya ajira na soko la bidhaa zao kutokana na ujio wa viwanda hivyo.
Watu wenye viwanda vidogo wana changamoto nyingi za maeneo na wengine kulazimika kuweka katika maeneo ya watu na kusababisha kero kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo.
Kwa ujumla, ujenzi wa viwanda si kitu kidogo, unahitaji muda na rasilimali nyingine nyingi kufanikisha hatua inayotarajiwa na umma.
Ndoto ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, inaelekea kutimia baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kuonesha kwa vitendo dhamira yake ya kuhakikisha ndoto hiyo inatimia.
Mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Paul Makonda anastahili pongezi kubwa na za dhati kabisa kwa mkakati wake wa kujenga Dar es Salaam mpya. 

No comments: