Saturday, February 18, 2017

DCP KIDAVASHARI AWAANIKA WA MADAWA YA KULEVYA,GONGO,MALI ZA WIZI NA SHAMBA LA BHANGI LATEKETEZWA KWA MOTO MBEYA



TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA TAREHE 17.02.2017.

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Kufuatia mapambano yanayoendelea nchi nzima dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji na utumiaji wa dawa za kulevya, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanya misako na Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-

KUPATIKANA NA DAWA ZA KULEVYA [BHANGI].

Mnamo tarehe 11.02.2017 hadi tarehe 16.02.2017 kwa nyakati tofauti, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya misako dhidi ya watu wanaojihusisha na uuzaji, usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya. Katika misako hiyo iliyofanyika maeneo  mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya, watuhumiwa wanne walikamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi misokoto mitatu yenye uzito wa kilogram 15 na gram 685

Watuhumiwa waliokamatwa wakiwa na dawa za kulevya aina ya Bhangi ni:-
1. GEOFREY ADAMSON [35] Mkazi wa Mabatini
2. ZUBER MWAMBENYA [24] na 3. GWAKISA ANYOSISYE [20] wote wakazi wa Mama John na
4. PHILIBERT MOSES [35] Mkazi wa Nonde
5. MPOKI IBRAHIM [37] Mkazi wa Kitongoji cha Igogwe Wilaya ya Rungwe
6. AGUST KIHAULILO @ KIDEVU [63] Mkazi wa Igawa Wilaya ya Mbarali
7. CALVINS MOHAMED [25] Mkazi wa Ilemi.
8. NASSORO OMARI [17] Mkazi wa Mwambene
9. OTHMANI SAIDI [24] Mkazi wa Mwambene
10. KENEDY BROWN [21] Mkazi wa mwambene

KUTEKETEZA SHAMBA KUBWA LA BHANGI

Mnamo tarehe 16.02.2017 majira ya saa 16:20 jioni Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kamati Kuu ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kipolisi Mbalizi lilifanya Oparesheni ya pamoja katika Kijiji cha Jojo kilichopo Kata ya Santilya, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata UPE NDUTA [30] Mkazi wa Jojo akiwa amelima shamba la bhangi lenye ukubwa wa ekari moja.

Aidha katika Oparesheni hiyo zaidi ya miche 2,000 iliyokomaa ilikutwa shambani. Pia nyumbani kwake alikutwa na bhangi kilogram 2 na gram 145. Mtuhumiwa ni mkulima, muuzaji/msafirishaji na mtumiaji wa dawa za kulevya [Bhangi].


KUPATIKANA NA MALI ZA WIZI.

Tarehe 15.02.2017 na 16.02.2017 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11 waliohusika katika kosa la kuvunja Ofisi za Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya na kuiba kompyuta 12 ambazo zilikuwa zikitumika kufundisha.

Aidha katika msako huo vitu mbalimbali vimekamatwa vinavyosadikiwa kuwa vya wizi pamoja na watuhumiwa ambao kati yao wapo wanaohusika katika matukio ya uvunjaji na ununuaji wa vitu vya wizi ambao ni:-

1.     GABRIEL MMASY [28] Mkazi wa Uhindini
2.     ITIKA KYEJO [Mwanamke] miaka 41 Mkazi wa Janibichi
3.     PETER MWAIPOPO [19] Mkazi wa Sinde
4.     WILLIAM JOSEPH [18] Mkazi wa Sinde
5.     RASHID SHABAN @ CHIDY [30] Mkazi wa Sinde
6.     FRANK CHAULA [25] Mkazi wa Sokomatola
7.     SALVATORY MTEGA [25] Mkazi wa Sokomatola
8.     KEFASY MWAMBENJA [31] Mkazi wa Kabwe
9.     RAPHAEL NGAILO [19] Mkazi wa Iyunga
10.  ABDUL RASHID [44] Mkazi wa Mbalizi
11. ZAKARIA RASHID KENSE [23] Mlinzi wa Kampuni ya New Imara Security na Mkazi wa Isanga

Katika msako huo Kompyuta 11 kati ya 12 zilikuwa zimeibiwa katika Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya zimepatikana.

Pia katika upekuzi uliofanyika katika makazi ya watuhumiwa walipatikana na mali mbalimbali zidhaniwazo za wizi ambazo ni:-
1.     Kompyuta 11 na Monitor 01 aina ya HP zilizotambuliwa kuwa ni mali za Chuo cha Utumishi wa Umma Tawi la Mbeya
2.     Monitor za Kompyuta 16 aina mbalimbali
3.     Digital Camera aina ya Canon
4.     Adapter 51 aina mbalimbali
5.     Kompyuta [Desk Top] 37 aina mbalimbali
6.     Laptop 10 aina ya HP, IBM, Samsung na Toshiba
7.     Mouse za Kompyuta 07
8.     Keyboard 11
9.     Kompyuta aina ya DELL [Working Station] 08
10.  Power Supply 23
11.  Hard Disk 64
12.  DVD ROM 14
13. Lamp Holder 01
14. Bulb World Star Lighting pcs 11
15. Spika moja
16. DVD Deck mbili aina ya Sony na Singsung
17. Sub Woofer mbili aina ya Sea Piano na Pintech
18. Stendi ya TV moja

Watuhumiwa baada ya kuhojiwa walikiri kuhusika katika matukio ya kuvunja Ofisi Usiku na kuiba pamoja na kununua mali mbalimbali za wizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito wa wananchi na wakazi wa Mbeya kufika kituo kikuu cha Polisi Kati kwa ajili ya utambuzi wa mali zao.

KUPATIKANA NA POMBE MOSHI [GONGO]

Mnamo kuanzia tarehe 01.02.2017 hadi tarehe 15.02.2017 kwa nyakati tofauti, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya misako katika maeneo ya Mafiati, Ilomba, Forest ya Zamani, Itiji, Igogwe, Ngonga na Ikolo Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita wakiwa na Pombe Moshi [Gongo] yenye jumla ya ujazo wa lita 39.

Watuhumiwa waliokamatwa wakiwa na Pombe Moshi ni:-
1. FRANCIS NDEZI [32] Mkazi wa Forest
2. JAMES KAJANJA [38] Mkazi wa Forest ya Zamani
3. MATRIDA CHABWELA [49] Mkazi wa Igogwe
4. MOSSES MWAKABENDE [51] Mkazi wa Ikolo
5. MARTIN MWAMBILYA [45] Mkazi wa Ngonga Wilaya ya Kyela
6. EMANUEL BROWN [21] Mkazi wa Itiji.
7. GEORGE BROWN [57] Mkazi wa Itiji
8. ITIKA KYEJO [41] Mkazi wa Janibichi
Upelelezi unaendelea.


KUPATIKANA NA MITAMBO YA KUTENGENEZEA POMBE MOSHI [GONGO].

Tarehe 16.02.2017 majira ya saa 10:00 asubuhi Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendelea na msako katika maeneo ya Mtaa wa Kagera, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aliyefahamika kwa jina la CLARENCE SUKARI [20] Mkazi wa mtaa wa Kagera akiwa na pombe haramu ya moshi lita 53.

Mtuhumiwa alikamatwa akiwa na mitambo miwili [mapipa] ya kutengenezea pombe hiyo. Aidha Pombe hiyo ilikutwa ikiwa imehifadhiwa katika vidumu 11 vya lita 5. Mtuhumiwa alikiri kuwa ni mtengenezaji, muuzaji na mtumiaji wa pombe hiyo haramu.


KUPATIKANA NA SILAHA SHORT GUN NA RISASI ZAKE.

Mnamo tarehe 13.02.2017 majira ya saa 18:02 jioni huko check point ya Igawa, iliyopo barabara kuu ya Mbeya-Njombe, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, Askari Polisi waliokuwa doria eneo hilo walimkamata mtu mmoja aitwaye  NAWAB HUSSEN [35] Mkazi wa DSM akiwa na silaha aina ya Short gun (greener marker) yenye namba ya usajili 26515 iliyokuwa imehifadhiwa kwenye mfuko wa salpheti na risasi mbili ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye mfuko mweusi wa Rambo.

Askari Polisi waliokuwa doria eneo la Check Point ya Igawa walilitilia shaka Gari lenye namba za usajili T 289 BWQ Toyota Hiace na baada ya kufanya upekuzi ndipo walimkuta mtuhumiwa akiwa na silaha hiyo. Mtuhumiwa alikuwa akisafiri kwa gari hilo kutoka Mbeya kwenda DSM. Gari hilo ni mali ya Kampuni ya KVD and Supplier LTD inayosambaza magazeti ya NIPASHE na THE GUARDIAN mikoa ya nyanda za juu kusini. Upelelezi unaendelea.


KUKAMATA WATUHUMIWA WA UHALIFU

Mnamo tarehe 04.02.2017 hadi 16.02.2017 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya Misako/Operesheni ya kukamata watuhumiwa wa matukio mbalimbali ya uhalifu katika maeneo ya Ilemi, Isanga, Nonde na Airport ya Zamani – Iyela. Katika Operesheni hiyo watuhumiwa wawili walikamatwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu ambao ni 1. VICTOR EBO @ TOLINGA [23] Dereva Bodaboda na 2. ADAM PHILIMON [21] Dereva Bodaboda, Wote wakazi wa Ilemi Jijini Mbeya.

Katika upekuzi watuhumiwa hao walikutwa na vifaa mbalimbali ambavyo hutumia katika matukio ya uhalifu ambavyo ni:-
1.     Mizura [mask]
2.     Shati ya kaki yenye muonekano wa jeshi
3.     Panga moja
4.     Kapelo
5.     Koti

Katika mahojiano na watuhumiwa walikiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu ambayo majalada yake ya uchunguzi yalikuwa tayari yamefunguliwa ambayo ni UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA – PANGA na KUJERUHI.


WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kuwafichua watu na mtandao wa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ili wakamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. Aidha Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kufanya kazi na kuacha kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwani inasababisha kupotea kwa nguvu kazi ya taifa na kurudisha nyuma maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.



Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.





MATUKIO KATIKA PICHA:-
Shamba la Bhangi likiteketezwa
 Askari wa Jeshi la Polisi wakiifungua mifuko iliyosheheni Bhangi
 Askari na wananchi wakiwa kwenye msako wa madawa ya kulevya na bhangi Mkoani Mbeya
Mitambo ya kutengenezea Gongo na Mali za wizi zikionyeshwa kwa waandishi wa habari


No comments: