Thursday, February 2, 2017

BARAZA LA TATU LA WAFANYAKAZI MOI LAFUNGULIWA


Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Prof Bakari Lembariti akihutubia wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa MOI wakati wa Uzinduzi wa Kikao cha Tatu cha Baraza Hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman Kiloloma akiwasilisha ripoti ya Utendaji ya Mwaka 2015/2016.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa MOI wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni rasmi Prof Bakari Lembariti
Makamu mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi MOI Prof Bakari Lembariti akimkabidhi cheti Mfanyakazi bora wa MOI kwa Mwaka 2015/2016 Bwana Robert Sere

…………………………………………………………………

Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya MOI Profesa Bakari Lembariti leo amezindua vikao vya Baraza la Tatu la Wafanyakazi wa MOI katika ukumbi wa IDDI NYUNDO katika halmashauri ya Temeke jijini Dar es Salaam. Vikao vimehudhuriwa na zaidi ya wajumbe 50 kutoka katika kila idara, vitengo na chama cha wafanyakazi wa MOI (TUGHE) na wajumbe wa TUGHE mkoa.

Akizindua Baraza hilo Profesa Lembariti alisema anampongeza Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli. Alisema ” Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini MOI Mh Zakia Meghji natumia Fursa hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uongozi wake uliotukuka na jitihada zake za kuboresha huduma za afya hapa nchini, sote ni mashahidi“.

Aidha, Profesa Lembariti aliwakumbusha wafanyakazi wa MOI kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma ili kujenga imani kwa watanzania walio wengi ambao wanaitegemea MOI kama Taasisi pekee inayotoa Tiba ya kiwango cha juu cha rufaa kwenye Tiba ya Mifupa, upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu.

Pia Profesa Lembariti alisema ni vyema wajumbe wa Baraza la MOI wakatumia vikao vya Baraza kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi ya MOI na kutafuta muarobaini ili Taasisi ya MOI iendelee kutoa huduma bora

Kwa upande mwingine Profesa Lembariti aliwakabidhi zawadi wafanyakazi Bora wa MOI kwa mwaka 2015/2016 ambapo Bwana Robert Sere aliibuka kidedea na kuwa mfanyakazi Bora wa MOI na kujipatia cheti na fedha taslimu kiasi cha Tshs Milioni 4, nafasi ya pili ikishikwa na Bwana Lucas Machage akijipatia cheti na kiasi cha Tshs Milioni 2 na nafasi ya tatu ikishikwa na Bi Betty Shila ambaye alijipatia cheti na kiasi cha Tshs Milioni 1.5

Kwa upande wake ,akiwasilisha ripoti ya utendaji wa Taasisi ya Kaimu Mkurugenzi wa MOI Dkt Othman Kiloloma alisema kutokana na ongezeko kubwa la ajali ambazo zimepelekea ongezeko kubwa la wagonjwa MOI, Taasisi ya MOI iko kwenye mpango mkakati kabambe wa kushirikiana na baadhi ya hospitali za rufaa za pembezoni kwa kuwapeleka wataalamu kutoa huduma katika hospitali hizo na kupunguza kama si kuondoa kabisa wimbi la wagonjwa wanaopokelewa MOI

Dkt Kiloloma alisema kwamba Taasisi ya MOI imeendelea kuwa Kitovu cha Weledi katika matibabu ya Mifupa ,Ajali ,Ubongo na Mishipa ya Fahamu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na kati ambapo mwaka 2015 MOI ilitoa utafiti bora wa mfupa mrefu wa paja duniani ,ambapo utafiti uliwasilishwa katika Taasisi ya kimataifa ya upasuaji wa mifupa duniani ya Marekani (AOTA)

Vilevile, Dkt Kiloloma aliwaomba wajumbe wa Baraza la MOI kutoa michango yenye tija ili kupata matibabu ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Taasisi ili Taasisi iendelee kutoa huduma bora kwa watanzania

No comments: