Tuesday, January 10, 2017

UWANJA WA NDEGE WA MWANZA KUKAMILIKA NOVEMBA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi anayejenga na  kukarabati uwanja wa ndege wa Mwanza Beijing Construction Engineering Group (BCEG), kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo Novemba mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa mnara wa kuongozea ndege, jengo la kuhifadhia mizigo, eneo la kuegeshea ndege na jengo la umeme litakalotoa huduma katika uwanja huo, Profesa Mbarawa amesema tayari Serikali imeshamlipa mkandarasi huyo kiasi cha shilingi bilioni saba kwa ajili ya ujenzi huo.
“Sisi tumeshamlipa pesa yake yote na hivyo tunachotaka kwake ni kukakamilisha kazi yetu kwa wakati ili kuupa hadhi inayostahili uwanja wa ndege wa Mwanza amboa ni kiungo muhimu katika kanda ya Ziwa”, Amesema Profesa Mbarawa.
Prof. Mbarawa amemuagiza Meneja wa uwanja wa ndege wa Mwanza Bi .Easter Madale kuhakikisha vikwazo vyote vinavyomkabili mkandarasi vinaondolewa ili kumuwezesha kufanya kazi kubwa kabla ya kipindi cha mvua za masika zinazotarajiwa kuanza mwezi machi.
Kwa upande wake Mhandisi Lili Ang aneyesimamia ujenzi huo  kutoka kampuni ya BCEG amemhakikishia Prof. Mbarawa kuwa baada ya kupokea malipo wamejipanga  kukamilisha kazi hiyo kwa wakati  na viwango ili waweze kupata fursa nyingine za ujenzi hapa nchini.
Naye Meneja wa Uwanja wa ndege wa Mwanza Bi .Easter Madale ameyataka mashirika ya ndege kuongeza safari za ndege kwenye uwanja wa Mwanza kwa kuwa sasa utakuwa na hadhi ya kimataifa na kusisitiza umuhimu wa wawekezaji wa hoteli, vituo vya mafuta na maduka makubwa  kuwekeza karibu na uwanja huo ambao ndio lango la uchumi wa kanda ya ziwa.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na  Mawasiliano ameelekea  mkoani Simiyu kuanza ziara ya siku mbili mkoani humo amabapo pamoja na mambo mengine anatarajiwa kushiriki katika ufunguzi wa barabara ya Bariadi- Lamadi iliyojengwa kwa kiwango cha lami.

No comments: