Monday, January 23, 2017

TANZANIA NA UTURUKI ZASAINI MIKATABA TISA YA MAENDELEO

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo na mgeni wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (kulia) Ikulu leo jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mazungumzo na mwenyeji wake Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (hayupo pichani) Ikulu leo jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akikagua gwaride mara baada ya kupokelewa na mwenyeji wake Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (hayupo pichani) Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majali (katikati) na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Balozi John Kijazi.
 Baadhi ya viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Miuungano wa Tanzania (waliokaa upande wa kulia) wakiweka saini katika mikataba na wawakilishi kutoka Serikali ya Uturuki leo jijini Dar es Salaam. Jumla ya mikataba tisa imetiwa saini, ikiwemo ushirikiano wa kimaendeleo.
 Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Tanzania akibadilishana hati ya makubaliano na Waziri wa Fedha wa Uturuki leo jijini Dar es Salaam.
UT5b: Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Dkt. Ayoub Ryoba akibadilishana hati ya makubaliano na mwakilishi wa Serikali ya Uturuki leo jijini Dar es Salaam.

  Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Dkt. Augustine Mahiga  akibadilishana hati ya makubaliano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki leo jijini Dar es Salaam.
 Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akiwapungia mkono wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliofika kumlaki katika viwanja vya Ikulu leo.Kushoto kwake ni Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
 Baadhi ya wananchi wakimlaki Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alipowasili katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam leo. Rais huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo katika ziara hiyo Tanzania na Uturuki wameingia makubaliano katika mikataba tisa kwa lengo la kushirikiana na kusaidiana.
 Baadhi ya wageni walioambatana na Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan wakiingia katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam leo.
 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Moses Nnauye akiteta jambo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe walipokuta wakati wa ugeni wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan( hayupo pichani) leo jijini Dar es Salaam.
 Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa ndani ya gari na mgeni wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan mara baada ya kumaliza mazungumzo Ikulu jijini la Dar es Salaam leo.
 Rais Dkt. John Pombe Joseph Maguli na mgeni wake Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan (walioshikana mikono) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mawaziri na viongozi kutoka Serikali za Tanzania na Uturuki leo jijini Dar es Salaam.

Picha na: Frank Shija – MAELEZO.


Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uturuki zimesaini mikataba tisa ya makubaliano ya kiuchumi inayolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo baina ya nchi hizo.

Mikataba hiyo inahusisha sekta za uchukuzi, mawasiliano, habari, elimu, utalii, utafiti, viwanda, afya na ulinzi.

Akizungumza mara baada ya kusaini kwa mikataba hiyo  leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alisema ujio wa Rais wa Uturuki na ujumbe wake ni kielelezo cha ukuaji wa mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki katika nyanja ya biashara na kimaendeleo baina nchini hizo.

Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake aliyofanya na Rais Recep Erdogan kuhusu ujenzi wa Reli ya Standard Gauge nchini, alimjulisha kiongozi huyo kuwa miongoni mwa wakandarasi walioomba zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuwa ni kampuni kutoka Uturuki, hivyo endapo itashinda zabuni hiyo itasaidia kukuza uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inatarajia kuomba  mkopo kupitia Benki ya Exim ya Uturuki katika kujenga sehemu ya kipande cha ujenzi wa reli hiyo.

Rais magufuli alisema Tanzania inaendelea kunufaika na uwepo wa Shirika la Ndege la Uturuki kwa kufanya safari zake za moja wka moja kutoka nchini Uturuki, kwa kuwa utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake Rais wa Uturuki, Recep Erdogan alisema kuwa uwepo wa mikataba hiyo baina ya Tanzania na Uturuki itasaidia kupata matokeo mazuri ya uhusiano pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano katika nyanja ya Kilimo, Utalii, Ulinzi, Reli ambazo zitawezesha kukuza uchumi wa mataifa hayo.

Rais Erdogan alisema kuwa Uturuki imelenga kukuza ushirikiano uliopo baina yake na  Tanzania kupitia makongamano ya wafanyabiashara yenye malengo ya kukuza uchumi, kuongeza ajira pamoja na kukuza ujasiriamali baina ya Tanzania na Uturuki.

“Kiwango cha Biashara ya uwekezaji katika nchi ya Uturuki ni Dola za kimarekani 150 ambapo lengo letu ni kufika Dola za kimarekani 500” alisema Rais huyo.

Aidha Rais Erdogan alisisitiza kuwa kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia nchi hizi kusonga mbele na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali.

Nae Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe alisema kuwa makubaliano ya mkataba baina ya Tanzania na Uturuki katika Sekta ya Utalii yatasaidia katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini, kubadilishana wataalamu, kubadilishana taarifa na kuongeza idadi ya watalii nchini.


Prof. Magembe aliongeza kuwa makubaliano hayo yatakuza sekta ya utalii katika kuvutia uwekezaji wa katika maeneo ya hoteli, fukwe na mbuga za wanyama zilizopo nchini. 

No comments: