Mbunge wa Rufiji Mohamed Mchengerwa wa tatu toka kushoto akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mgomba Kati katika ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitaftia ufumbuzi.
MBUNGE wa Rufiji ,Mohamed Mchengerwa (CCM),amesema viongozi wengi serikalini ni wafugaji ndio maana wanashindwa kushughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imekuwa ikisababisha madhara makubwa kwa wananchi kila kukicha.
Mchengerwa alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mgomba kati ambao walieleza jinsi wafugaji wanavyoingiza mifugo hao katika mashamba ya wananchi wakati wakiwa hawajavuna mazao yao na kwamba kila walikokuwa wanapeleka kilio chao wafugaji wanatoa rushwa wanashinda kesi.
"Wafugaji wanatuumiza mno lakini haya yote ni kwasababu viongozi wengi ni wafugaji hivyo wanashindwa kuingilia kati suala hili badala yake wanaacha wananchi wauane kila kukicha,utafika wakati tutashindwa kuyavumilia haya, tunakufa njaa na umasikini kwasababu ya watu"alisema na kuongeza kuwa
"Yametokea matukio makubwa ya kuuliwa wananchi wawili katika kijiji cha Kilimani mwezi uliopita lakini sikuona kiongozi yeyote serikalini aliyetolea tamko au hata kufika eneo la tukio vivyo hivyo hata kwa yule mwananchi wa Morogoro aliyechomwa mkuki shingoni ukatokea mgongoni viongozi wametulia tu"
Alisema sio Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ,Charles Tizeba ,Naibu wake William Ole Nasha wala Makatibu wakuu wao wawili waliofika katika maeneo yaliyoathirika au hata kutolea matamko ya makatazo dhidu ya jambo hilo na kwamba hayo ndio matunda ya viongozi wengi kuwa wafugaji hivyo kushindwa kuja na njia as kutafuta suluhisho za kudumu.
Alisema suala la kuwepo kwa mifugo Rufiji limetokana na rushwa iliyotolewa kwa viongozi waliokuwepo madarakani miaka ya 2005 kutokana na kuwa walitoa mifugo kwenye bonde ili lisiharibike na kupeleka katika bonde lingine ili kuua wananchi wa maeneo hayo.
"Mifugo hapa kwetu ilikuja Mwaka 2005 ilihamishwa kutoka bonde la Ihefu Iringa kwakuwa lilikuwa linaharibika lakini cha kushangaza ikaletwa katika bonde la Rufiji ili liharibike na sisi wananchi wa huku tupate shida na ndicho kinachotokea Leo hii "alisema Mchengerwa
Alieleza kuwa amechaguliwa na wananchi kwa ajili ya kuwawakilisha vyema kwa kutetea maslahi yao na ndicho anachokifanya na kwamba hatarudi nyuma katika kudai haki na maendeleo ya Rufiji kwani wamekuwa nyuma kwa miaka mingi kutokana na kukosa wawakilishi wenye nia ya dhati ya kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment