Na Rajab Mkasaba, Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein ameweka jiwe la msingi Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali na
keleza kuwa bado kuna tatizo la ukusanyaji, utumiaji na uhifadhi wa takwimu
hapa nchini hivyo kuna haja ya kuwekwa mfumo madhubuti katika kuondoa hitilafu
hiyo.
Dk. Shein aliyasema
hayo, katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kuweka jiwe la msingi Ofisi ya
Mtakwimu Mkuu wa Serikali iliyopo huko Mazizini, Wilaya ya Mjini, Unguja ikiwa
ni miongoni mwa shamrashamra za miaka 53 ya Mapinduzi ya matukufu ya Zanzibar.
Katika maelezo yake,
Dk. Shein alisema kuwa udhaifu katika utoaji wa takwimu na taarifa, ni ukiukaji
wa maadili ya uongozi na utumishi wa ummma kwa msingi huo aliagiza kwa kila
Wizara ihakikishe inakuwa na mtaalamu wake wa takwimu katika Idara ya Mipango
na Sera, ili kuimarisha utoaji wa takwimu.
Dk. Shein alisema kuwa
taarifa sahihi haziwezi kupatikana bila ya kuwa na mfumo mzuri wa kitaalamu wa
ukusanyaji wa takwimu huku akisisitiza kuwa suala la kuwapa wananchi habari na taarifa sahihi za Serikali ni haki
yao ya kikatiba na halina budi kutekelezwa ipasavyo.
“Mimi mwenyewe ni
mtumiaji mkubwa wa takwimu, lakini unapohitaji takwimu kutoka Wizarani basi kwa wakati mmoja tarajia kupata takwimu
tofauti’,alisema Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein
alisisitiza kuwa kuna haja ya kuondokana na utaratibu uliopo hivi sasa wa kila
mmoja kuwa na mamlaka ya kutoa takwimu za Serikali na kueleza kuwa utoaji wa
takwimu muhimu za Serikali una taratibu zake.
Hivyo, alieleza haja
kwa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoa miongozo kwa Wizara na Serikali
juu ya njia bora za kukusanya, kutoa na kutumia takwimu na nani katika ngazi ya
Wizara anaweza kutoa takwimu.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein alisisitiza haja kwa hiyo kuhakikisha kuwa inaandaa utaratibu wa kutoa
elimu kwa wananchi kuhusu takwimu na umhimu wake kwa jamii, kwenye ngazi mbali
mbali.
Pia, alitumia fursa
hiyo kuiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuongeza kasi ya kuwasomesha
wafanyakazi wanaohusika na takwimu, ili kupatikane wataalamu wa kutosha,
watakaoweza kukusanya na kutoa tafsiri mbali mbali za takwimu na uhusiano wake
wka maendeleo hapa ya hapa nchini.
Kutokana na umuhimu wa
takwimu Dk. Shein alieleza azma ya Serikali kutoa semina maalum kwa viongozi wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuelewa suala zima la takwimu na
hatimae kusaidia kufanya kazi kwa haraka na ufanisi zaidi.
Sambamba na hayoeleza
kuwa katika suala zima la kulitafutia soko zao la karafuu, Zanzibar imekuwa
ikishindana na nchi nyingi zinazozalisha zao hilo duniani kwenye bei na ubora
sambamba na sifa ya karafuu, hivyo Zanzibar ni lazima ijidhatiti katika
kuhimili ushindani.
Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kuiopongeza Ofisi hiyo kwa ujenzi huo kwa mashirikiano ya pamoja na
SMZ, SMT na Benki ya Dunia nhuku
akisisitiza kuwa takwimu ndizo zinazowezesha kujipima na kujitathmini kwani
ndio kiii cha nchi.
Nae Waziri wa Fedha na
Mipango Dk. Khalid Salum Mohammed alieleza
kuwa ujenzi huo ni agizo la Rais Dk. Shein la kutaka kila taasisi ya Serikali
iwe na jengo linalokwenda na wakati uliopo huku akieleza azma ya kuzipatia
Ofisi za takwimu ofisi Pemba katika
majengo mapya ya Ofisi yanayotarajiwa kuejengwa kisiwani humo.
Pamoja na hayo, Dk.
Khalid alieleza mikakati iliyowekwa na Wizara yake katika utekelezaji wa suala
zima la takwimu huku akieleza jinsi Wizara ilivyofanikiwa kuzigundua taasisi
zinazovujisha mapato ya serikali na kumuahidi Rais kuwa ataziwasilisha kwake
mara tu baada ya kumaliza sherehe za Mapinduzi.
Nae Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Ashatu
Kijaji alitumia fursa hiyo kueleza kuwa ujenzi huo unakwenda sambamba na ujenzi
wa jengo jengine kama hilo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania huko Dodoma.
Dk. Kijaji alitumia
nafasi hiyo kumuomba Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia kuendelea kuzisaidia
taasisi hizo za takwimu ili kwa pamoja ziweze kukamilisha miradi yote miwili na
kueleza kuwa takwimu ndio masikio na macho ya Serikali ya Awamu ya
Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025
kwa Tanzania Bara na 2020 kwa Zanzibar.
Alitoa pongezi kwa
kutekeleza kwa kasi kubwa kauli mbiu ya Serikali ya HAPA KAZI TU!! Na kuishukuru Benki ya Dunia, Shirika la
Maendeleo la Uingereza DFID, Canada na Umoja wa Ulaya kwa kuunga mkono tasinia
ya takwimu hapa nchini.
Nae Mwakilishi wa
Benki ya Dunia Elizabeth Ann Talbert alieleza umuhimu wa takwimu katika
maendeleo ya nchi huku akiahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi
za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha takwimu.
Mapema Mtakwimu Mkuu
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bi Mayasa Mahfoudh Mwinyi alileza kuwa
kiini cha ujenzi wa jengo hilo la takwimu ni kuongezeka kwa mahitaji ya takwimu
katika sekta za kiuchumi na kijamii.
Alisema kuwa mahitaji
hayo yamepelekea kuongezeka kwa idadi ya wataalamu wa fani ya takwimu sambamba
na kuongezeka kwa mahitaji ya vifaa na nafasi za kufanyia kazi ikiwemo
mazingira bora ya kazi.
Bi Mayasa alieleza
historia ya kuazishwa kwa Ofisi hiyo pamoja na viongozi walioongoza ambapo
alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo umeanza rasmi mwezi Oktoba 2015 na unatarajiwa
kukamilika mwezi Aprili mwaka huu ambapo ujenzi huo unakadiriwa kugharimu jumla
ya shilingi bilioni 7.9 hadi kukamilika kwake.
Ujenzi huo umejengwa
na Mkandarasi “Messrs World Class Engineering and Contractors Limited” pamoja
na Msimamizi wake Y & P Architects (T) Limited zote ni Kampuni za Kizalendo
zilizopo Tanzania ambapo jengo hilo litakuwa na ghorofa nne.
Viongozi mbali mbali
walihudhuria hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif
Ali Idd, Spika wa Baraza la Wawakilishi na viongozi wengine wa Serikali,
Mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Zanzibar, viongozi wa dini na wananchi
mbali mbali.
No comments:
Post a Comment