Monday, December 19, 2016

YATAMBUE MAMBO 10 YA KUKUSAIDIA KUPERUZI KWA USALAMA MTANDAONI

Sababu ya mtandao, Dunia ni kama kijiji kimoja.Mtandao umekuwa kitu cha muhimu kwenye maisha ya watu wengi sana,mitandao inatufanya tuwasiliane kwa urahisi na ndugu jamaa na marafiki mbalimbali,inatufanya kupata taarifa mapema zaidi kuliko vyanzo vingi vya taarifa vya ‘kizamani’ kama runinga, redio na magazeti,mitandao pia ni chanzo cha ajira kwa watu wengine.

Hapa chini nakupa dondoo kadhaa za kukusaidia walau kujihadhari na hatari ndogondogo ukiwa kama mtumiaji wa kawaida wa mtandao

1.Usisambaze taarifa zako ovyo.

Kuwa makini unapowasiliana na watu katika mitandao ya kijamii,na kuwa makini zaidi linapokuja suala la kumpa mtu taarifa zako nyeti kama akaunti za benki,au password,usidangaanyike na jumbe za kilaghai kama zinazokutaarifu kushinda bahati nasibu,kupata mkopo au mtu anayetaka kukupa dili lakini anataka taarifa hizo akuwekee kiasi fulani cha fedha,asilimia 99 huwa ni matapeli wa mtandaoni

2. Epuka malumbano yasiyo na maana mtandaoni

Moja ya sababu ya kuwa na mitandao,haswa ya kijamii ni kubadilishana mawazo na mijadala mbalimbali lakini kama ilivyo kwa imani tofauti tulizonazo,wakati mwingi mawazo huwa tofauti-wasilisha mawazo yako kwa hoja na sio mihemko,jifunze kukubali kutokubaliana na mawazo ya wengine kama hamjafikia tamati inayoendana,ni sawa kila mtu kuamua kuamini anachoamini.

La pili ni kukaa mbali na wazinguaji wa mtandaoni(Trolls) hawa ni watu ambao aidha hukataa kila kitu kwa ajili ya ubishi tu au hufanya hivyo kutafuta sifa na ‘likes’ kwa kuonekana wanaenda tofauti na mawazo ya wengine,hapa hata ukiwa na hoja za maana ni kazi bure kwani kwao ubishi wa mtandaoni ni kama mchezona zaidi ya yote epuka matusi,kumbuka kuna sheria za mitandao hivyo unaweza kujikuta mikononi mwa dola kwa sababu ya malumbano yasiyo na mantiki.

3. Usisambaze taarifa usizojua chanzo chake.

Umeamka asubuhi umekutana na taarifa kwenye kundi la WhatsApp mtu fulani maarufu amekufa,bila kuwa na uhakika sana unasambaza kwa makundi yako mengine 8 na jamaa zako kadhaa kwenye simu yako.Unakosea,mtandao ni kama bahari kubwa sana ya taarifa zipo taarifa za ukweli,za uongo za utanina kadharika,na kwa kukusaidia tu kama hujui kuna baadhi ya blogu na tovuti ambazo ni maalumu kwa ajili ya kuchapisha taarifa za utani/uongo(Mfano huzzlers.com)-NDIO,yaani taarifa zote utakazosoma humo ni za kutunga na kufikirika hivyo unapoona taarifa mpya jiridhishe kuhusu chanzo chake kabla ya kusambaza kwa wengine na kuendeleza upotoshaji.

4. Chunguza mtu unayewasiliana naye.

Kweli mitandao ya kijamii imetengenezwa kwa ajili ya kukutanishwa na marafiki,wale tunaowajua toka zamani mashuleni au wapya,lakini kuwa na utaratibu wa kumfahamu mtu unaejuana nae mara ya kwanza mtandaoni kabla ya kuanza kubadilishana nae taarifa zako muhimu na nyeti,kumtumia picha zako au za familia,kuna akaunti nyingine za mitandao ya kijamii ni za watu wanaotumia taarifa za uongo kuonyesha ni mtu au jinsia fulani kumbe sio hivyo inabidi utumie akili ya kuzaliwa katika kujiridhisha na uhalisia wa mtu unayewasiliana naye.

5.Kutana kwa tahadhari.

Umepata rafiki mtandaoni,mmewasiliana sana sasa mmekubaliana kukutana uso kwa uso,au umekubaliana na mtu uliyewasiliana nae kwenye mitandao ya kubadilishana,kununua na kuuziana vitu mbalimbali.Je,unachukua tahadhari gani?Inashauriwa kuwa makini sana linapokuja suala la kuamisha mawasiliano ya mtandaoni kuwa ya uso kwa uso,hakikisha mahali mlipokubaliana kukutana ni sehemu ya wazi au sehemu ya watu wengi na iliyo bize ili kukusaidia kupata msaada endapo jambo lolote la tofauti litatokea.

Zingatia muda-epuka kukutana na mtu unayemuona mara ya kwanza mida ya jioni sana au usiku sana,panga muda wa asubuhi mpaka mchana,muda ambao inapunguza hatari zozote zisizotegemewa,kama itawezekana pia jitahidi uwe na mtu wa kukusindikiza kwenye kuonana huko,anaweza kuwa ndugu au rafiki wa karibu kama inashindikana walau umpe mtu yoyote wa karibu taarifa za awali kuhusu unapokwenda na unayeenda kukutana nae ili iwe rahisi kupata msaada inapotokea dharura walau kuna mtu ana taarifa zinazoweza kusaidia.

6. Chunguza jumbe unazotumiwa kabla hujafanya lolote
Unafungua kifaa chako, unapata taarifa mpya kutoka Facebook..unafungua ni msichana mrembo anaomba urafiki,picha zake ni machachali na zinatia hamasa,unathibitisha na baada ya dakika kadhaa anakutumia ujumbe,eti muwasiliane zaidi kupitia anwani pepe au anakuambia ubofye link fulani kuona picha zake zaidi!Usiingie mtegoni

Yawezekana una rafiki Facebook aliyeomba samahani kuwa picha na video alizosambaza siku kadhaa zilizopita sio yeye na kwamba akaunti yake ilidukuliwa?Au Pengine ni wewe yalikukuta hayo?Kwa kiwango kikubwa ni matokeo ya kubofya link za ajabu ambazo huruhusu programu mbalimbali kuchapisha taarifa kwenye akaunti yako bila wewe kujua lakini ulifanya hivyo pale ulipobofya link, picha za ajabu au za taarifa fulani ya kuvutia.

Mifano hiyo ni kuonyesha jinsi programu kadhaa za kompyuta zilivyotengenezwa kifasaha kukudangaya kuwa ni kitu fulani mradi tu ubonyeze kitufe fulani au link,na hapo waendeshaji wa programu hizo huwa na uwezo wa kuchapisha taarifa kwa niaba yako,kutuma ujumbe na picha kwa marafiki au tu kuchukua taarifa zako na baadae kuzitumia kwa jinsi wanavyojua wao.


7. Jua walau virefu kadhaa vya mafaili muhimu unayotumia sana mtandaoni na kwenye kifaa chako
Je,we ni mpenzi wa muziki,video au programu za simu na kompyuta?Unajua programu za mfumo wa Windows zina kirefu gani(Mfano .exe,.msi) vitu hivi ni vya kitaalamu kidogo kwa mtumiaji wa kawaida ila ni muhimu kujua walau juu juu au kwa uchache,ili kuepusha kuweka faili ambalo sio katika mfumo wa kifaa chako na kumbe faili hilo ni kirusi au programu chafu,mfano ma faili ya muziki mengi ni .mp3,.aac,.wav hivyo unapotaka kupakua faili la muziki na unaona kirefu chake kinaonyesha .exe ambayo unajua ni kirefu cha faili la programu,achana nalo!yawezekana ni programu iliyotengenezwa kwa mfano wa na jina la muziki fulani ulioutafuta mtandaoni kukudanganya ili uweke kwenye mfumo wako.

Kingine cha muhumu ni kupakua ma faili kutoka vyanzo husika na vinavyojulikana ,kama wewe ni mtumiaji wa android pakua programu zilizopo playstore au tovuti zenye uhakika,windows vilevile pakua kutoka windows market na ios(iphone/iPad) kutoka itunes na appstore yao.

8. Usiache taarifa zako kwenye vifaa
Njia pekee ya kuhakikisha taarifa zako muhimu ziko kwenye mikono salama ni kukaa nazo mwenyewe tu,hivyo unapouza/gawa simu au kifaa kingine chenye picha zako,ama za familia au zako za falagha na taarifa nyingine hakikisha umezifuta na kutumia mfumo wa kufuta simu kuwa kama ilivyonunuliwa(wipe data),usijidanganye kuuza/kugawa simu na kumwamini unayemuuzia/gawia kufanya kazi hiyo kamwe hii itasaidia kuhakikisha taarifa zako unabaki nazo na haziendi kwenye mikono isiyo salama.

Kama ilivyo kwenye uuuzaji,unaponunua pia au kupokea kifaa kutoka kwa mtu ni muhimu kuondoa taarifa zake kama bado zipo ili kuondoa mkanganyiko linapotokea jambo lolote(Mfano aliyekuuzia kafanya uhalifu na taarifa zake za mtandaoni zimefuatiliwa mpaka ulipo wewe,utaisaidia polisi)

Iwapo una akaunti ya mtandao fulani wa kijamii hutaki kuitumia ni vyema pia kutumia njia iliyowekwa na mtandao husika kufuta,tofauti na kuitelekeza tu na kama akaunti ilidukuliwa na ukafungua mpya,fanya kutoa taarifa katika mtandao husika ili ifungiwe kabisa isije kutumika kwa jina lako kufanya utapeli na mambo mengine ya ajabu.

Kabla hujaondoka kwenye kifaa cha jumuiya unachotumia kuperuzi,hakikisha ume log out ili kuepusha matumizi mabaya kwa wengine watakaokuja na kukuta akaunti yako bado ipo hewani.

9.Toa taarifa za unyanyasaji,udhalilishaji au utapeli
Inapotokea picha zako au taarifa zinatumika ndivyo sivyo mtandaoni,umetapeliwa au unadhalilishwa toa taarifa kwa wahusika,inaweza kuwa kwa mtandao husika kama jambo lenyewe linahusika huko au kwa chombo kinachosimamia jambo lenyewe(Mfano TCRA ) hii ni muhimu kwako pamoja na wengine ambao watapona baada ya hatua madhubuti kuchukuliwa kwa wahusika.

Kumekuwepo na matukio mbalimbali nchi za jirani na hata hapa nchini ya watu kujiua au kuuliwa,kudhulika na sababu kuja kujulikana baadaye kuwa ni unyanyasaji ulioanzia mitandaoni

10.Zingatia utunzaji wa password.

Hakikisha password yako ina nguvu kwa kuwa na tarakimu angalau sita zikiwa ni mchanganyiko wa maneno na namba,usitumie password rahisi kama jina lako,jina la mtu au namba zilizozoeleka kama 123,1234,0000 sababu ni rahisi kukisia au kudukuliwa.

Usihifadhi password kwa kuandika kwenye vikaratasi ambavyo ni rahisi kupotea,khifadhi kama message kwenye simu yako,weka kumbukumbu kichwani au tumia program maalumu za uhifadhi kama 1password,LastPass zinazokuwezesha kuwa na password kuu moja unayokumbuka(Master) na nyingine kuzihifadhi kwa urahisi mpaka pale unapohitaji,program hizi pia hukusaidia kutengeneza password mpya au kubadili ulizonazo kwa kuzingatia vigezo vyote vya password madhubuti.

Kuwa chonjo!

Kama jinsi tunavyosema kuwa mtandao unafanya dunia kuwa kama kijiji kimoja hivyo basi kama jijiji cha kawaida kilivyo,kuna watu wa aina mbalimbali katika kijiji hichi cha .com, waongo, matapeli, wezi n.k.Hakikisha unachukua tahadhari muda wote unapoperuzi.

No comments: