Wednesday, December 7, 2016

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya kazi yadhihirisha Tathimini ya Upimaji wa Ardhi Nchini

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani  Bw. Justo Lyamuya akitoa tathimini ya upimaji  Ardhi nchini kwa  waandishi wa Habari ( hawaonekani pichani) kulia  kwake ni Mkurugenzi Msaidizi upimaji na Ramani Bw. Simon Katambi na kushoto  kwake ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano  Serikalini Wizarani hapo Bi.  Mboza Lwandiko.
------------------------------------
Viwanja 32,303 na mashamba 76 yamepimwa nchini toka robo ya kwanza ya mwaka / Julai  - Septemba 2016, kwa maazimio ya upimaji wa vipande 400,000 vya Ardhi ifikapoJuni, 2017.
Akitoa taarifa kwa Vyombo vya habari; Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Justo Lyamuya ameeleza. Alisema, toka mwaka 1961 hadi 2016 vimepimwa viwanja 1,359,899 na mashamba 24,579. Kwa kipindi cha miaka 6 iliyopita kuanzia 2010 hadi Juni 2016 vimepimwa viwanja 558,403 na mashamba 4,314.
Bw. Lyamuya alitoa ufafanuzi wa upimaji uliofanyika wa maeneo mbalimbali nchini. Alieleza Upimaji wa ardhi chini ya maji (Hydrographic Survey) umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kwa ushirikiano na Jeshi la majini la India, kufuatia makubaliano kati ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya India tumeweza kupima bandari za Dar es Salaam, Zanzibar na Mkoani Pemba. Ramani za Bandari hizo zipo kwenye duka la ramani tayari. Mwaka huu upimaji wa bandari ya Tanga umefanyika na kazi ya uwandani imekamilika na ile ya ofisini inaendelea.
Katika eneo la Upimaji Mipaka ya Vijiji; Alisema kuwa vijiji 10,667 kati ya vijiji 12,000 vimepimwa. Chini ya Mradi wa Land Tenure Support Programme umepima vijiji 52 kwenye wilaya 3 za Morogoro (Kilombero, Malinyi na Ulanga).
Katika Upimaji wa usimikaji alama za Msingi za Upimaji, alieleza kuwa; Alama za msingi za upimaji zimesimikwa nchi nzima zikiwa katika viwango tofauti. Zero order zipo 16, First Order zipo 72 na second order 525. Baadhi ya maeneo alama hizi zimesambazwa katika umbali utakaoruhusu upimaji kufanyika kwa urahisi. Sambamba na usambazaji huo wa alama za upimaji; umbo la dunia (Tanzania Geoid) limekokotolewa kurahisisha upatikanaji wa vipimo vya miinuko.
Vile vile, katika eneo la Upimaji Mipaka ya Kimataifa, Bwn. Lyamuya alisema; “Kwa mipaka ya kimataifa mipaka yote ya baharini na majirani zetu imeandaliwa Mikataba ya makubaliano na kuridhiwa. Kwa upande wa Maziwa makubaliano ya uwekaji mpaka ndani ya Ziwa Tanganyika Kati ya Tanzania, DRC, Zambia na Burundi, yamefikiwa. Utekelezaji utaendelea baada ya fedha kupatikana”.
Bwn. Lyamuya alikiri uwepo wa changamoto mbalimbali zilizopo katika taaluma ya upimaji na kutaja baadhi ya maazimio yaliyoazimiwa katika Kongamano la wapima lililofanyika tarehe 2 na 3 Novemba 2016. Baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kila Kampuni inayotambulika na kusajiliwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia lengo la kutoa hati laki 4 kwa mwaka 2016/17 kwa kuwasilisha taarifa ya kiasi cha vipande vya ardhi iliyopima na kila kampuni kwenye mkutano ujao na kuandaa mapendekezo ya ada ya kitaaluma na gharama za upimaji wa ardhi zitakazotozwa ambazo zitasambazwa na kutumika nchini kote
Aidha, azimio jingine lililoazimiwa na wanataaluma hao ni pamoja na  kumtambua Waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi; Mh. William Lukuvi, kupewa uanachama wa heshima wa IST/ Institute of Surveyers Tanzania, kutokana na jitihada zake kubwa katika kushughulikia matatizo ya ardhi nchini, na mchango wake katika kuwatambua wapima ardhi kuwa ndio suluhisho la kuwawezesha wananchi kumilikishwa ardhi.


 Habari na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

No comments: