Wednesday, December 21, 2016

WIZARA YA AFYA YAENDESHA MAFUNZO YA KUPAMBANA NA MAGONJWA YASIOAMBUKIZA NCHINI

 Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Margaret Mhando akipitia baadhi ya nyaraka za kufundishia kabla ya kufungua mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
 Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasioambukiza Dkt. Sarah Maongezi akiongea na madaktari na watoa huduma hawapo pichani wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
 Mratibu wa Magonjwa yasioambukiza Mkoa wa Dar es salaam Dkt. Digna Riwa akitoa mafunzo kwa waganga na watoa huduma hawapo pichani wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
 Baadhi ya madaktari kutoka mikoa tofauti nchini wakifuatilia kwa makini mafunzo kutoka kwa mkufunzi hayupo pichani wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya yaliyofanyika Mkoani Morogoro.
Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Margaret Mhando katikati waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madaktari kutoka mikoa tofauti nchini wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya yaliyofanyika Mkoani Morogoro.

Na Ally Daud
WIZARA ya Afya ,Maendeleo  ya Jamii ,Jinsia ,Wazee na Watoto kupitia kitengo cha Magonjwa yasioambukiza (NCD) chini ya Kurugenzi ya Tiba inaendesha mafunzo ya kupambana na magonjwa yasioambukiza kwa watoa huduma ngazi za mikoa na wilaya.

Akifungua mafunzo hayo leo jijini Morogoro Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Margaret Mhando amesema kuwa wameamua kuanzisha mpango huo ili kuwapa nguvu na uwezo watoa huduma kwa ajili ya kupambana na magonjwa hayo.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakiongezeka kwa kasi sana duniani na haswa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hivyo hatuna budi kuongeza juhudi za kupambana nayo” alisema Dkt. Mhando

Aidha Dkt. Mhando amesema kuwa pamoja na juhudi zinazofanywa na Wizara katika kupambana na magonjwa hayo kila mkoa na wilaya lazima ziangalie uwezekano wa kuifanya NCD kuwa kipaumbele katika mipango yao ya  maendeleo.

Kwa mujibu wa Dkt. Mhando amesema kuwa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza imeonyesha kuongezeka kwa hali ya juu ambapo  idadi ya watu wanaovuta sigara ni asilimia 15.9 wanaokunywa pombe ni asilimia 29.3, wenye uzito uliopita kiasi 34.7, shinikizo la damu ni asilimia 25.9 na wagonjwa wa kisukari ni asilimia 9.1.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa yasioambukiza Dkt. Sarah Maongezi amesema kuwa wanatakiwa kupunguza moja ya tatu ya vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa kukinga, kutibu na kuzingatia afya ya akili Kufikia mwaka 2030.

Aidha Dkt. Maongezi amesema kuwa  wanatarajia waganga wa ngazi za mikoa na wilaya kufanya kazi kwa nguvu na kwa ukaribu zaidi na kitengo cha magonjwa yasiyo ya kuambukiza cha Wizara ili huduma hizi ziwafikie watu wote hadi ngazi ya jamii.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanayofanyika jijini Morogoro yanalenga kuwafundisha madaktari na watoa huduma kuhusu kupambana na ya magonjwa yasioambukiza ikiwemo kisukari, magonjwa ya moyo, shinikizo la damu, kansa, ajali za barabarani  na uzito kupita kiasi.

No comments: