Sunday, December 25, 2016

Viongozi wa Vijiji watakiwa kujiridhisha Miradi ya Umeme Vijijini

 Na Mohamed Saif
 Mkandarasi wa Kampuni ya Derm Electric Limited anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) Mkoani Mara ameagizwa kukutana na Uongozi wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoani humo pamoja na Viongozi wa Vijiji vinavyopitiwa na mradi huo ili wajiridhishe kabla hajaukabidhi. 
Agizo hilo lilitolewa hivi karibuni na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alipofanya ziara ya Kikazi ya kukagua utekelezaji wa Miradi umeme Vijijini katika Kijiji cha Kwikuba Kata ya Busambala, Wilaya ya Musoma Vijijini. 
Aliagiza ifikapo Tarehe 5 Januari 2017, wakutane kukagua mradi huo ili kujiridhisha kama mradi huo umekamilika katika kiwango kilichokubaliwa. 
"Msiporidhishwa na namna mradi huu ulivyotekelezwa; kama kutakuwa na mapungufu msikubali kuupokea na hii pia itakua ni sababu ya Mkandarasi huyu kutopewa kazi nyingine," alisema.

Alisema Mkandarasi anapaswa kuwa amekamilisha kutekeleza mradi huo ifikapo tarehe 31 Desemba mwaka huu na hivyo alimuagiza kuhakikisha anakamilisha ndani ya muda huo na kwa ubora unaostahili. 
Alisema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha umasikini unatokomezwa, na kwamba kupitia nishati ya umeme dhamira hiyo itaweza kutimia. “Hakuna Nchi iliyoachana na umasikini bila kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika,” alisema Profesa Muhongo. 
Vilevile alizungumzia suala la bei ya kuunganishwa na nishati hiyo kuwa ni shilingi 27,000 ambayo alisema ni sawa na bei ya jogoo wawili. 
Aidha, Waziri Muhongo aligusia Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) na kusema kwamba umelenga kuhakikisha Vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya nishati ya umeme na wakati huo huo aliwaasa wananchi kuchangamkia kuunganishwa na huduma husika kwa maendeleo endelevu. 
“Tunawaletea huduma hii ya umeme, ndugu zangu wananchi nawasihi mchangamkie, msikubali fursa hii ikawapita. Tunavyozungumzia maendeleo tunazungumzia umeme”, alisema Waziri Muhongo.”

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkandarasi ambaye ni Mhandisi wa Mradi huo, Mhandisi Hussein Ayubu alisema mradi huo ulianza Septemba 2013 na kuwa utakamilika ifikapo Januari, 2017. 

Alisema katika utekelezaji wake, changamoto mbalimbali zilijitokeza ambazo baadhi yao hadi hivi sasa zinaendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kufanya shughuli za utekelezaji wake kuwa ngumu. 
Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni wananchi kugomea usimikaji wa nguzo ama upitishaji wa nyaya kwenye maeneo yao hadi hapo watakapolipwa fidia. 
Aliongeza kuwa ubovu wa miundombinu hususan ya barabara imekuwa ni kikwazo katika utekelezaji wa mradi kwani kipindi cha mvua usafirishaji wa vifaa unakuwa mgumu na hivyo kusababisha kusimama kwa baadhi ya shughuli katika baadhi ya maeneo. 
Mhandisi Ayubu alisema hamasa ya kuunganishiwa huduma ya umeme miongoni mwa wananchi ni ndogo na kwamba lengo la Mradi huo wa Mkoa wote Mara ni kuwaunganisha wananchi wapatao 14,000 lakini hadi hivi sasa wananchi waliounganishiwa ni 6,600.

No comments: