Na Teresia
Mhagama
Vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini watafaidika na mafunzo yatakayotolewa
na kampuni ya Empower kutoka Korea yatakayohusu utengenezaji vifaa Umeme Jua
ambavyo vinatumika kuwasha taa na kuchaji simu huku gharama yake ikiwa ni nafuu.
Hayo yamebainika jijini Dar es Salaam wakati wa kikao baina ya
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Balozi wa Korea nchini, Song Geum-Young na watendaji wa kampuni ya
Empower, inayotengeza vifaa hivyo.
Watendaji wa kampuni hiyo
walifika na baadhi ya vifaa hivyo vya Umeme Jua ili kuionesha Wizara
namna vinavyofanya kazi.
Dkt. Hong Kyu Choi, kutoka kampuni ya Empower alisema kuwa wamepanga
kutoa mafunzo hayo sehemu mbalimbali nchini ili vijana hao waweze kujiajiri na
pia kuwezesha wananchi hasa wa vijijini kupata huduma ya umeme.
Alisema kuwa mafunzo hayo pia yatatolewa kwa walimu wa Sayansi
nchini ili nao waweze kuwafundisha wanafunzi kuhusu teknolojia na hivyo kuwa endelevu.
“ Vijana wa Tanzania wana uelewa mkubwa sana hivyo wanachohitaji ni
kupata fursa ya kupata mafunzo kama haya na nyenzo ili waweze kujiajiri na pia
kuweza kufundisha watu wengine, hii itawasaidia wao kujiajiri pia,” alisema
Dkt. Choi.
Kwa upande wake, Profesa Muhongo alisema kuwa vifaa hivyo ni muhimu
sana hasa katika sehemu ambazo hazijafikiwa na nishati ya umeme na kwamba suala
la kutoa mafunzo hayo kwa vijana ni muhimu kwani itawawezesha kupata uelewa wa
teknolojia inayotumika kutengeneza vifaa hivyo pamoja na kujiajiri.
“Napata simu nyingi sana Watu wakilia, Umeme, Umeme, hii teknolojia
ni nzuri na itawasaidia wananchi wetu kupata mwanga na pia kuchaji simu zao,
hivyo nawakaribisha kuanza kutoa mafunzo hayo mwezi Machi mwakani,” alisema Profesa
Muhongo.
Hii ni mara ya Pili kwa Profesa Muhongo kukutana na Watendaji wa
kampuni hiyo ambapo mara ya kwanza alikutana nao mwishoni mwa mwezi Novemba
mwaka huu ambapo Balozi wa Korea hapa nchini alifika kuitambulisha kwa Waziri
wa Nishati na Madini na pia kueleza shughuli za kampuni hiyo katika sehemu
mbalimbali duniani.
Katika Kikao hicho cha mwezi Novemba, Mtendaji wa Empower, Dkt. Choi alisema kuwa, kampuni hiyo imekuwa
ikitengeneza vifaa hivyo vya Umeme Jua kwa kutumia teknolojia ya kisasa tangu
mwaka 2011 na kwamba lengo lake ni kusambaza huduma hiyo vijijini ili
kuwasaidia vijana na wananchi kupata huduma ya umeme na kwa gharama nafuu.
Alitaja baadhi ya kazi ambazo wameshazitekeleza kuwa ni pamoja na
kubuni na kutengeneza Mfumo wa Umeme Jua katika Kituo cha ‘City Christian
Center (CCC)’ kilichopo Dar es Salaam pamoja na kutengeza Paneli za Umeme Jua
za gharama nafuu katika sehemu
mbalimbali Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment