Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B.Simbachawene (MB) akifafanua juu ya kuanzisha ujenzi wa mradi wa maji ya uhakika wa kisima ambacho mkondo wake umepita chini sana, lakini pia alitoa agizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutunga sheria ndogo ndogo za matumizi bora ya ardhi na kutojenga au kulima karibu na barabara zinazopita katika maeneo yao.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. George B.Simbachawene (MB) akikagua maendeleo ya Mradi wa kituo cha Afya katika kijiji cha Winza (Makao makuu ya kata ya Massa) ambapo asilimia kubwa ya mradi huo ipo katika hatua za mwisho, kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mpwapwa Bw. Donald Ng’wenzi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George B.Simbachawene (MB) ambaye pia Mbunge wa Kibakwe akikagua maendeleo ya Mradi wa kituo cha Afya katika kijiji cha Winza, mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwakani.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George B.Simbachawene (MB) ambaye pia ni Mbunge wa Kibakwe akisalimiana na wananchi katika kijiji cha Ikuyu kata ya Ruhundwa wakati wa ziara yake ya kujionea maendeleo katika kata za Ruhundwa na Massa wilayani Mpwapwa. Nyuma yake ni Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Bw. Jabir Shekimweri.
Mkuu wa wilaya Mpwapwa Bw. Jabir Shekimweri akikabidhiwa aina ya muhogo unaolimwa katika kijiji cha Ikuyu kata ya Ruhundwa naye pia aliahidi kuwapelekea wananchi mbegu bora ya muhogo inayolimwa na Jeshi la Magereza wilayani humo. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa kijiji cha Ikuyu Bw. Emid Myowera.
Mojawapo ya barabara inasimamiwa na Halmashauri ya wilaya ikiwa imetengenezwa vizuri na kuwezesha uchukuzi wa mazao, bidhaa na watu kuwa rahisi na kuchochea kasi ya maendeleo ya wananchi. Barabara hiyo inaungansha Kata za Massa, Ruhundwa, Rudi na Kibakwe na ipo wilayani Mpwapwa, pia ipo katika Mpango wa pili wa Taifa 2018/2019 kujengwa kwa kiwango cha lami. Awamu ya kwanza ni kutoka Mbande kuja Kongwa, Mpwapwa, Gulwe hadi Kibakwe unaotarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2017/2018
Sehemu ya ardhi katika kijiji cha Mkoleko, kata ya Massa iliyopo wilayani Mpwapwa ikiwa imeharibiwa vibaya kutokana na njia mbaya za kilimo, eneo lipo katika muinuko na limezungukwa na makorongo yanayopitisha maji kipindi cha masika hali inayosababisha uharibifu wa vyanzo vya maji na rasilimali misitu na mazingira.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi),George Simbachawene ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha zinatunga sheria ndogo ndogo kwa ajili ya uhifadhi vyanzo vya maji, barabara za mamlaka hizo na njia mbaya za kilimo zinazo athiri mazingira.
Simbachawene ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kibakwe aliyasema hayo alipotembelea baadhi ya maeneo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa wilayani Mpwapwa ambapo alitembelea kata ya Massa na Ruhundwa katika vijiji vya Mkoleko, Makose, Chogola, Winza, Njia Panda na Ikuyu na alijionea hali halisi ya maendeleo ya wananchi katika vijiji hivyo.
Aidha alibaini kuwapo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira unaotokana na njia mbaya za kilimo katika kijiji cha Mkoleko na kumtaka Mkuu wa wilaya hiyo Bw. Jabir Shekimweri na timu ya wataalam wa wilaya kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali ya mmomonyoko wa udongo unayotishia kutoweka kabisa kwa kijiji hicho.
“kamati ya huduma za Jamii ifanye kazi yake, mweke kontua na kuacha kulima na kukata miti katika kingo za makorongo ili kulinda mazingira” alisisitiza Simbachawene.
Amewaasa wananchi kutumia fursa za ujio wa makao makuu ya nchi mkoani Dodoma kwa kulima mazao ya chakula na biashara kwani miundo mbinu ya lami kutoka Mbande kuja Kongwa, Mpwapwa, Gulwe hadi Kibakwe ujenzi wake unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2017/2018.
“barabara yetu inayotoka Mbande, Kongwa, Mpwapwa, Gulwe, Kibakwe, Rudi hadi Chipogoro itajengwa kwa kiwango cha lami lakini awamu hii Serikali imetangazwa barabara ya lami kutoka Mbande kuja Kongwa, Mpwapwa, Gulwe hadi Kibakwe” alisema Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene Akiwa katika kijiji cha Chogola ameziagiza Mamlaka za Serikali nchini kufuata Sera na Sheria lakini pia kutunga sheria ndogo ndogo zinazozingatia utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwani kumekuwepo na uharibifu mkubwa wa mazingira vijijini.
Aidha, ametoa agizo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mikoa nchini kuzingatia ujenzi wa mpangilio katika makazi ya watu vijijini na shughuli za kilimo kando kando ya barabara uzingatie sheria za kuacha umbali unaotakiwa ili kulinda barabara kwa matumizi endelevu.
Kuhusu ombi la wananchi wa kijiji cha Ikuyu kuanzisha kata mpya Mhe. Simbachawene amesema Serikali inapenda kubana matumizi kwa kuepuka uanzishaji wa maeneo mapya ya utawala yasiyo na tija kwa wananchi, hivyo ameshauri kata ya Ikuyu yenye vijiji vya Ikuyu, Kidenge, Mpwanila, Chang’ombe, Muungano na Ruhundwa ibaki kama ilivyo kwa kuwa eneo la kata mpya wanayoomba yenye vijiji vya Ikuyu, Chang’ombe na Muungano litakuwa dogo.
“Sisi kama Serikali ya awamu ya tano hatutaki kufanya vitu visivyo na tija kwa sababu ugawaji wa maeneo ya utawala ya vijiji, kata, halmashauri, wilaya na mikoa, hatudhani kama kufanya hivyo kunaondoa kero au shida ya wananchi, wananchi hawa wanashida za maji, barabara na kupata madawa hospitalini. Mimi nadhani tija ya wananchi sio kuigawa nchi hii katika vipande vidogo vidogo”, Alisema Mhe.Simbachawene.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Bw. Jabir Shekimweri aliwaagiza wananchi kata za Ruhundwa na Massa kupanda mazao yanayovumilia ukame kwa kuwa mwaka huu kunatarajiwa kuwa na mvua chini ya wastani pia alimwagiza Mtendaji wa Kata ya Massa kufuatilia masuala ya mazingira kwa ukaribu zaidi.
No comments:
Post a Comment