Tuesday, December 6, 2016

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina atembelea Bagamoyo


Na Evelyn Mkokoi - Bagamoyo 
SERIKALI imeiagiza Baraza la hifadhi ya Mazingira (NEMC ) na Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais kufanya tathimini ya awali ya kuangalia ni namna gani itaweza kuzuia maji ya bahari kuingia katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) na kuharibu miundombinu yake ambapo hadi sasa takribani mita 70 hadi 100 ya bahari imeisogelea taasisi hiyo. 
 Akizungumza jana wilayani Bagamoyo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Luhaga Mpina wakati wa ziara ya kutembelea Taasisi hiyo na kujionea ni namna gani bahari inavyosogea katika taasisi hiyo na kuanza kuathiri baadhi ya majengo. 
 Alisema kutokana na hali hiyo kuwa ya dharura ameziagiza mamlaka hizo kufanya tathimini ya awali ambapo kufikia Januari 30 mwakani watapaswa kukabidhi ripoti ya awali kwa serikali na kujua nini kifanyike katika kunusuru taasisi hiyo na kuifanya mahala pazuri pa kujifunzia masuala ya utamaduni. Mpina alisema ripoti hiyo itaweza kupelekwa serikalini ili mipango madhubuti ianze kufanyika ya kuhakikisha taasisi hiyo inakuwepo na inaendelea kutoa mafunzo yake kama kawaida bila kuathiriwa na usogelewaji wa bahari katika maeneo hayo. 
 "Januari 30 mwakani tutapata hiyo ripoti na kuipeleka serikalini na kuangalia ni namna gani tutakavyonusuru taasisi hiyo na kama kutahitajika utafiti mwingine wa kina kuhusiana na jambo hili utaweza kufanyika na kujua nini kifanyike katika maeneo haya kama kutengeneza Makinga maji au Ukuta,"alisema Mpina 
 Alisema hali ya bahari kuhamia katika maeneo ya nchi kavu inatokana na kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi yanayotokea baharini ambapo kwa sasa kina cha bahari kimeweza kuongezeka kufikia Sentimita 19 na kusababisha madhara ya maji kusogea katika maeneo ya nchi kavu. 
 Mpina alisema takribani majengo matatu ya taasisi hiyo yapo hatarini kuathirika ambayo yanajumla ya thamani ya kiasi cha sh.bilioni 1.6 ambapo yatasababisha hasara kubwa kwa majengo pamoja na taasisi hiyo. Aidha mpaka sasa kuna baadhi ya fukwe tayari zimeanza kufanyiwa utaratibu wa kujengwa kwa kingo zikiwemo fukwe za Pangani Tanga,Kilimani Zanzibar, Kisiwapanza Pemba, pamoja na fukwe za Ocean road Dar es Salaam. 
 Kwa Upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo, Dkt.Herbert Makoye alisema taasisi yao ina tatizo kubwa la kusogelewa na bahari na kusababisha athari kubwa katika baadhi ya madarasa. 
 Alisema kwa sasa bahari inazidi kusogelea chuo hali inayotishia uwepo wake endapo jitihada dhabiti hazitaweza kuchukuliwa kwani hadi sasa uoto wa asili umeanza kutoweka kidogo kidogo. 
Wakati huohuo, kufuatia malalamiko ya wakazi wa kata ya Bunju, Naibu Waziri Mpina alitembelea maeneo hayo yanayoathiriwa kwa kiasi kikubwa na maji ya mvua, na kuharibu miundombinu na mazingira na kupelekea afya za wakazi wa maeneo hayo kuwa hatarini kuathiriwa na magonjwa, hali ambayo ilimlazimu Mpina kutoa agizo kwa NEMC, Idara ya Mazingira Ofisi ya Makmu wa Rais na Manispaa ya Kinondoni kufanya Tathnini ya mazingira katika eneo hilo na kuja na mpango mkakati wa muda mfupi na mrefu ili kuweza kunusuru hali hiyo. Mpina aliwaasa wakazi wa eneo hilo pia kuzingatia ujenzi wa mipango miji na kuacha njia za maji na maeneo oevu

No comments: