Tuesday, December 20, 2016

MWIGULU NCHEMBA AINGILIA KATI SAKATA LA MAUAJI YA WAKULIMA NA WAFUGAJI MKOANI PWANI

 Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba kushoto akiwa na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka wakizungumza jambo baada ya kulikagua gari ambalo lilikamatwa likiwa na wahamiaji haramu 150  Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ambao ni raia wa Ethiopia(PICHA NA VICTOR MASANGU) 
Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba wa kulia na kushoto kwake ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha  mjini Silvestry Koka  wakiangalia gari ambayo ilikamatwa Wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani ikiwa na wahamiaji haramu wapatao  150 ambao ni  raia  kutoka nchini Ethiopia ambao walikamatwa wakati wakiwa  wapo safari kuelekea miko ya kusini. (PICHA NA VICTOR MASANGU)




NA VICTOR MASANGU, PWANI


KUTOKANA na kuwepo kwa ongezeko la wimbi la migogoro ya ardhi kila kukicha katika baadhi ya maeneo katika Mkoa wa Pwani kati ya jamii ya wakulima na wafugaji na kupelekea wakati mwingine kuibuka kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe ambayo yanasababisha hali ya uvunjifu wa amani na baadhi ya viongozi na wananchi wengine kupoteza maisha kikatili kimeundwa kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kuweza kukomesha kabisa vitendo hivyo.

Matukio ya namna hiyo katika Mkoa wa Pwani yanaonekana kumsikitisha na kumlazimu Waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba kuingilia kati sakata hilo kwa kutangaza rasmi kupambana vilivyo na watu wote ambao watabainika wanajihusisha na vitendo hivyo vya mauaji ili waweze kukamatwa haraka na kuweza kufikishwa katika vyombo vya dola ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Waziri nchemba ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya kuwatembelea askari polisi, magereza, uhamiaji pamoja zimamoto wa Mkoani Pwani kwa ajili ya kuweza kukagua shuguli mbali mbali za utekelezaji ya majukumu yao ya kila siku ikiwemo na kuweza kubaini changamoto zinazowakabili pamoja na kuweka mikakati kwa ajili ya kuweza kuzitafutia ufumbuzi.

“Kumekuwepo katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani kuna baadhi ya viongozi wa vijiji pamoja na wakulima na wafugaji kupoteza maisha, kwa hili sisi kama Wizara hatuwezi kulivumilia hata kidogo kwani kwa sasa tumejipanga ii kuweza kuwabaini watu ambao wanahusika katika vitendo hivyo,”alisema Waziri.

Alisema kuwa anasikitishwa kuona mauaji yanafanyika kitu ambacho ni kinyume kabisa na sheria na taratibu za nchi, kwa mwananchi yoyote kuamua kujichukulia sheria mikononi kwa kufanya vitendo vya mauaji hivyo ameahidi kulivalia njuga suala hilo na wale wote watakaobainika wataweza kuchukuiwa hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Aidha Waziri Nchemba alibainisha kuwa kutokana na kuwepo kwa wahamiaji haramu ambao wanaingia nchini bila ya kuwa na vibali Wizara yake imeweka mikakati kabambe ya kuongeza doria usiku na mchana katika sehemu mbali mbali ikiwemo mipaka, fukwe za bahari pamoja na bandari bubu amabzo zimekuwa zikitumika kuwapitisha raia hao wa kigeni.

“Tatizo lawahamiaji haramu katika Mkoa wa Pwani bado ni tatizo kubwa kwani imekuwa ndio kama lango la kuingilia pindi wanapokuja hasa katika maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo pamoja na Wilaya ya Kibaha, hivyo sisi katika hili tumeshajipanga ili kuweza kuthibiti njia zote ambazo wamekuwa wakizitumia katika kupita,”alisema Nchemba.

Pia katika hatua nyingine Nchemba alitoa wito kwa wananchi wote kushirikiana bega kwa began a serikali pamoja na vyombo vya dola katika kuwabaini na kuwafichua watu ambao wanakuwa na mashaka nao kwani wengine wanaingia nchini kwa ajili ya kufanya matukio mbali mbali ya uharifu wa kutumia siraha.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameiomba serikali ya awamu ya tano kupitia 
Wizara ya mambo ya ndani kuhakikisha inaongeza vitendea kazi pamoja na kuongeza ujenzi wa vituo vingine vidogo vya polisi ambavyo vitaweza kusaidia kuimarisha hali ya ulinzi na usalama pamoja na kupamba na waharifu ambao wanaingia Mkoa wa Pwani kinyemela na kujificha.

Pia Koka alimwomba waziri wa mambo ya ndani kuweka utaratibu wa kuhakikisha vituo vidogo vya polisi vilivyojengwa vinakuwa wazi wakati wote lengo ikiwa ni kuweza kupambana na matukio mbali mbali ya uharifu ambayo yanakuwa yanajitokeza bila ya kuwa na muda maalumu hivyo vituo vikiwa wazi kutaweza kusaidia kupunguza hali ya uharifu.

MATUKIO ya vitendo vya mauaji katika baadhi ya maeneo Mkoani Pwani ambayo yanawahusisha wakulima na wafugaji pamoja na baadhi ya viongozi wengine bado yanaonekana kuwa ni tishio na kuendelea kufanyika hivyo kunahitajika jitihada za makusudi zifanyike kutoka serikalini ili kuweza kutatua migogoro hiyo na kurudisha hali ya amani na utulivu kwa wananchi.

No comments: