Wednesday, December 21, 2016

MKAPA FOUNDATION YAKABIDHI NYUMBA 28, MAJENGO MAWILI YA UPASUAJI MKOANI SIMIYU

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu(wa tatu kulia) akikata utepe katika ufunguzi wa Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Ngulyati lililokabidhiwa kwa Serikali na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (kushoto) akisoma Jiwe la ufunguzi wa Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Ngulyati lililokabidhiwa kwa Serikali na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.

Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu(wa pili kulia) akikagua baadhi ya vifaa tiba mara baada ufunguzi wa Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Ngulyati lililokabidhiwa kwa Serikali na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.
 Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu(kushoto) akisaini vitabu vya wageni mara baada ya kuwasili Mjini Bariadi kwa ajili ya  ufunguzi wa Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Ngulyati lililokabidhiwa kwa Serikali na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, (kulia)Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka.
 Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation,Dkt.Hellen Mkondya Senkoro akiwasilisha taarifa ya mradi wa ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Ngulyati lililokabidhiwa kwa Serikali na Taasisi hiyo.
Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu (wa nne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi wa Wilaya ya Bariadi,Mkoa wa Simiyu na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation mara baada ufunguzi wa Jengo la Upasuaji (pichani) katika Kituo cha Afya.


Na Stella Kalinga 
Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation imekabidhi Serikali jumla ya Nyumba 28 kati ya 48 zinazotarajiwa kujengwa kwa ajili ya watumishi wa Idara ya Afya na Majengo Mawili ya Upasuaji kwa ajili ya huduma za akina mama wajawazito Mkoani Simiyu.

Akipokea na kufungua Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya cha Ngulyati Wilayani Bariadi na Nyumba za Watumishi katika Hospitali ya Mkula wilayani Busega, Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto , Mhe.Ummy Mwalimu ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuuunga mkono Serikali katika uboreshaji wa huduma za Afya, hasa katika ujenzi wa miundombinu ya Afya.

Mhe.Waziri amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuboresha huduma za Afya kwa kuongeza kiwango cha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, miundombinu ya Afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali, Vituo vya Afya, Zahanati na Majengo ya Upasuaji, hivyo upatikanaji wa majengo hayo utasaidia wananchi wa maeneo husika kupata huduma zinazotakiwa. 

Mhe.Waziri ameongeza kuwa Serikali imeanza kwa kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa kuongeza bajeti, ambapo kwa Mwaka 2015 zilitengwa jumla ya shilingi bilioni 31 na mwaka 2016 zimetengwa shilingi bilioni 51.

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine imejipanga kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa Mkoani Simiyu, hivyo pindi kiwanda hicho kitakapokamilika dawa za Vituo Mbalimbali vya kutolea huduma za Afya zitanunuliwa Simiyu.

Aidha, Mhe.Ummy Mwalimu ameutaka Uongozi wa Mkoa uhakikishe unasimamia ukusanyaji wa mapato katika Vituo vyote vya kutolea huduma za Afya, ili sehemu ya mapato hayo itumike kununulia dawa na vifaa tiba kwa lengo la kuwahakikishia wananchi upatikanaji wa huduma bora za afya.

Katika kukabiliana na tatizo la vifo vya akina mama wajawazito na watoto wakati wa kujifungua, Mhe.Ummy Mwalimu amewataka akina mama wajawazito kujifungulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na kituo cha Afya cha Ngulyati mahali ambapo Jengo la Upasuaji na wodi kwa ajili ya akina mama wajawazito vimejengwa. 

Sanjari na hilo Mhe.Ummy Mwalimu akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa Ngulyati wilayani Bariadi na Mkula wilayani Busega, amewahakikishia kuwa Wizara yake italeta watumishi wa idara ya afya ili kukabiliana na upungufu uliopo na akazitaka Halmashauri zote mkoani Simiyu kutengeneza mazingira mazuri ambayo yatawapa motisha watumishi watakaoletwa na kuendelea kubaki Simiyu.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya nyumba za watumishi na majengo ya Upasuaji, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Dkt.Hellen Mkondya Senkoro amesema, Taasisi hiyo imekamilisha majengo hayo yote na akaiomba Serikali kuweka miundombinu iliyosalia kama maji, vifaa vya kutolea huduma na watumishi ili wananchi waweze kunufaika na miradi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka ameishukuru Taasisi ya Mkapa Foundation na akaahidi kuwa Serikali itajitahidi kuhakikisha changamoto zote zinatatuliwa katika miradi ya Benjamin Mkapa Foundation ili itekelezwe kwa tija na manufaa kwa wananchi.

Aidha,Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Waziri wa Afya,Maendeleo yaJamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu kwa kutoa magari ya kubebea wagonjwa (Ambulance) nane(08) kwa Vituo vya Afya,Hospitali za Wilaya na Hosptali Teule ya Mkoa kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma.

Wakati huo huo Mbunge wa Busega,Mhe.Dkt.Raphael Chegeni amemshukuru Mhe Waziri kwa jitihada zinazoendelea kufanyika katika kuboresha huduma za Afya Mkoani Simiyu na akamuomba aupe kipaumbele Mkoa wa Simiyu, hususani Wilaya za Busega na Itilima ambazo ni mpya kila Wizara yake inapogawa rasilimali au miundombinu mingine ya Afya.

Wilaya za Mkoa wa Simiyu zilizonufaika na Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya Upasuaji sambamba na wodi ya wazazi Bariadi na Busega ambayo yamejengwa kwa thamani ya shilingi milioni 435, kwa upande wa Nyumba za Watumishi wilaya ya Busega (Nyumba 10),Itilima (Nyumba 10) na Bariadi ni Nyumba 08 ambazo zimegharimu jumla ya shilingi bilioni 1.47.

No comments: