Wednesday, December 14, 2016

MAWAKILI NCHINI WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande akiongea mbele ya mawakili 258 hawapo pichani wakati wa sherehe ya 55 ya uhapisho huo iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande katikati akiongoza Majaji wengine kupokea salamu ya utiifu kutoka kwa mawakili 258 waliopishwa hawapo pichani wakati wa sherehe ya 55 ya uhapisho huo iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Mawakili wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande hayupo pichani baada ya kuapishwa wakati wa sherehe ya 55 ya uhapisho huo iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya Mawakili wakiwa wamesimama kusubiri kula kiapo kutoka kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande wakati wa sherehe ya 55 ya uhapisho huo iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Othman Chande katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Mawakili waliopishwa wakati wa sherehe ya 55 ya uhapisho huo iliyofanyika leo jijini Dar es salaam.



Na Lydia Churi-Mahakama 


Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman amewataka Mawakili nchini kuzingatia Maadili na kufuata misingi ya haki katika kutekeleza majukumu yao ili kesi ziendeshwe kwa haki, haraka na kwa wakati ili kuongeza imani ya wananchi kwa Mahakama.

Akizungumza wakati wa sherehe za kuwapokea na kuwaapisha Mawakili leo katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amesema endapo Mawakili watatekeleza wajibu wao kwa kutenda haki watasaidia kupunguza mlundikano wa kesi zilizopo kwenye Mahakama mbalimbali nchini kuanzisha zile za Wilaya mpaka mahakama ya Rufani.

Aidha, Jaji Mkuu amewataka Mawakili kushirikiana Mahakama pamoja na wadau wengine katika kuutekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ambao pamoja na mambo mengine pia unalenga kupunguza mlundikano wa kesi kwenye mahakama mbalimbali nchini.

Mhe. Othman pia amewashauri Mawakili walioapishwa leo kujiendeleza kielimu ili waweze kuongeza ujuzi utakaowasaidia kupambana na changamoto mbalimbali za kitaaluma na kwenda na wakati.

Amewataka Mawakili hao kusambaa na kufanya kazi mikoani ili na raia walioko huko nao wapate haki badala ya wengi wao kung’ang’ania kwenye miji mikubwa pekee kama vile Dar es salaam, Arusha, na Mwanza.

Naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Fednand Wambali amesema suala la ushiriki wa dhati katika utoaji wa haki nchini limesisitizwa kwa Mawakili walioapishwa leo.

Mhe. Wambali pia amewataka Mawakili hao kuwa waaminifu kwa Mahakama ya Tanzania na kwa wateja wao ambao n iwananchi wanaotafuta haki zao.Aliongeza kuwa bila ya Mawakili hao kuwa na maadili hawataweza kufanya kazi.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili hao wapya kufanya kazi zao kwa kufuata maadili ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.Alisema kupitia kamati ya malalamiko, amepokea malalamiko 71 kati ya mwaka 2015 na 2016 yaliyowahusu Mawakili kukiuka taratibu na misingi ya kazi yao.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, baadhi ya malalamiko yalihusu Mawakili kutokuwatetea wateja wao ipasavyo, kufanya kazi ya uwakili bila ya kulipia kibali, na kutoa siri za wateja wao.

Jaji Mkuu wa Tanzania amewakubali na kuwaapisha Mawakili wapya 285 na kuifanya Tanzania kuwa na Mawakili zaidi ya 6080. Sherehe za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili hao zimefanyika kwa mara ya 55 tangu kuanzishwa kwa sherehe hizo mwaka 1986 hapa nchini.

No comments: