Wednesday, December 14, 2016

KIWANDA KIKUBWA CHA MBOLEA KUJENGWA MKOANI LINDI


Benny Mwaipaja, WFM, Dar es salaam.

Kampuni moja ya Ujerumani ya Ferrostaal, inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kitakacho gharimu zaidi ya Euro Bilioni 1 nukta 2 (1.2bln) ambacho kinatajwa kuwa kitakuwa moja ya viwanda vikubwa vya mbolea Barani Afrika.
Hayo yamesemwa na Balozi wa Ujerumani hapa nchini, EGON KOCHANKE, wakati alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Jijini Dar es salaam, ambapo wawili hao wamezungumzia masuala kadha wa kadha yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani uliodumu kwa muda mrefu.
Balozi Kochanke amesema kuwa kiwanda hicho kitakachojengwa kwa ubia kati ya kampuni hiyo ya Ujerumani na wawekezaji wazawa na wengine kutoka Bara la Asia, inatokana na  hamasa kubwa ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhamasisha ujenzi wa viwanda.
“Kiwanda hiki kitakuwa kikubwa zaidi ya mara mbili ya kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mtwara na kitagharimu Euro Bilioni 1.2, kitasisimua uchumi wa nchi pamoja na kukuza ajira” alisema balozi huyo aliyeambatana  na naibu Balozi wa Ujerumani hapa nchini, John Reyels na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa nchi hiyo Julia Hannig.
“Mbali ya Kampuni hiyo ya Ferrostaal, wawekezaji wengine ni kampuni ya Mbolea ya Minjingu, na kampuni nyingine kutoka Pakistan ambayo kwa pamoja wameingia ubia wa kujenga kiwanda hicho cha mbolea kitakachokuwa uwekezaji mkubwa” Aliongeza Balozi Egon Kochanke.
Egon Kochanke, ameiomba serikali kutatua changamoto ya gharama za gesi ili kiwanda hicho kiweze kuanza ujenzi wake mapema iwezekanavyo na kuchochea maendeleo ya kilimo hapa nchini.
Ameyataja maeneo mengine ambayo nchi yake itaelekeza rasilimali zake kuwa ni kuendeleza sekta ya afya, wajasiriamali wadogowadogo, sekta ya ufundi mchundo pamoja na kuhamasisha wawekezaji kutoka nchini mwake kuja kuwekeza viwanda na biashara mbalimbali hapa nchini.
Aidha, Balozi huyo wa Ujerumani ameahidi kuwa nchi yake iko tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kuifanyia ukarabati meli ya MV Liemba, inayofanya zafari zake katika ziwa Tanganyika, ambayo ni meli ya kihistoria kwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 100, ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa watanzania na nchi jirani za Zambia, Burundi na DRC Kongo.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, ameishukuru Ujerumani kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na kwamba Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano huo.
Amesema kuwa uwekezaji wa kiwanda kikubwa na cha mfano cha mbolea huko mkoani Lindi, utachochea sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watanzania, kwa kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya wakulima na mbolea ya ziada itauzwa nchi za nje.
Dkt. Mpango, amemshukuru Balozi huyo wa Ujerumani kwa ahadi yake ya kusaidia kukarabati meli ya MV Liemba, na kiomba nchi hiyo kusaidia ununuzi wa meli mpya ili kuimarisha usafiri na usafirisha wa watu na mizigo katika eneo la maziwa makuu.
Vilevile ameiomba nchi hiyo kuendeleza misaada yake katika sekta ya ufundi kupitia mamlaka ya Ufundi Stadi (Veta) pamoja na kuendelea kutoa ufadhili wa masomo ya juu kwa wanafunzi wa kitanzania kwenda kusoma nchini humo kama ambavyo imekuwa ikifanya miaka mingi iliyopita kupitia Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Balozi Kochanke amekubali kufanya hivyo na kuahidi kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika mambo hayo na masuala mengine, ikiwemo kuishauri namna bora ya kuhamishia Serikali mkoani Dodoma, wakitumia uzoefu wa nchi hiyo ilipohamisha makao makuu yake kutoka Berlin kwenda Born.
 Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Egon Kochanke (katikati) pamoja na ujumbe wake wakisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yakitolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) (hayupo pichani),  Makao Makuu ya Wizara hiyo Jijini Dar es salaam.  
 Ujumbe wa Ujerumani ukiongozwa na Balozi wan chi hiyo nchini Tanzania, Egon Kochanke (katikati) ukiwa katika mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Kulia) wakati wa mazungumzo kuhusu uhusiano uliopo kati ya nchi hizo mbili, Jijini Dar es salaam. Kulia kwa Balozi  ni Mkurugenzi wa Ushirikiano Bi. Julia Hannig na na kushoto kwake ameketi Naibu Balozi wa Ujerumani hapa nchini Bw. John Reyels.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia) akiangalia nyaraka alizokabidhiwa na  Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Egon Kochankewakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.  Kulia kwa Waziri ni Mchumi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Melckzedek Mbise na anayefuata ni katibu wa Waziri Bw. Makamba.
 Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Egon Konchanke akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (wa pili kushoto) akielezea namna ya ushirikiano wa maendeleo kati ya nchi ya Tanzania na Ujerumani unavyoweza kuwa na tija kwa pande zote, wakati wa kikao kati yake na  Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Egon Konchanke, Makao Makuu ya Wizara jijini Dar es salaam.
 Mkurugenzi wa ushirikiano kutoka ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bi. Julia Hannig, akifafanua jambo wakati wa kikao kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango (Mb) na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke (kulia), Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (kushoto) akiagana na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Bw. Egon Kochanke (kulia) baada ya kumalizika kwa kikao kati yao, kilichofanyika  Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (Mb) (kulia) akiagana na Mkurugenzi wa Ushirikiano kutoka Ujerumani, Bi. Julia Hannig, nje ya Makao makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kumalizika kwa mkutano katika ya ujumbe huo kutoka Ujerumani ukiongozwa na Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke, Jijini Dar es salaam.


(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Hazina)

No comments: