Thursday, December 15, 2016

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA MABALOZI WA NNE KWA WAKATI TOFAUTI NA KUFANYA NAO MAZUNGUMZO

Mabalozi wa Nchi Mbili za Brazil na Kenya wameipongeza serikali ya awamu ya Tano kwa mipango na mikakati yake ya madhubuti ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania -ATCL – kwa kununua ndege mpya kama hatua ya kuhakikisha shirika hilo linakuwa bora katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchini.

Mabalozi hao wamesema hatua hiyo ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Tanzania itasaidia kukuza shughuli za utalii na pato la taifa kwa ujumla.Balozi wa Brazil nchini Carlos Alfonso Puente na Balozi wa Kenya hapa nchini Chirau Ali Makwere wametoa pongezi hizo mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ikulu jijini Dar es salaama.

Kwa upande wake, Balozi wa Brazil nchini Carlos Alfonso Puente amesema kutokana na nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa nchi kadhaa Dunia zenye viwanda wa kutengeneza ndege hivyo serikali ya Tanzania ina nafasi nzuri ya kununua ndege nchini Brazil hasa kulingana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi hizo mbili.

Kufutia wito huo wa Balozi wa Brazil Nchini, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi ya Brazil kuja nchini kutangaza bidhaa wanazotengeneza hasa ndege kama hatua ya kuimarisha mahusiano ya biashara kati ya Brazil na Tanzania.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kutokana na nchi ya Brazil kupiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari na Tanzania ni moja ya nchi yenye maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji huo hivyo ni muhimu kwa wafanyabiasha wa Brazil kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.

Kuhusu kilimo cha Pamba nchini, Balozi wa Brazil Carlos Alfonso Puente amesema serikali ya nchi hiyo imeanzisha mradi kabambe unaolenga kusaidia uzalishaji bora wa pamba katika mikoa ya kanda ya ziwa mradi ambao utagharimu dola za Kimarekani milioni Sita kwa miaka minne nchini.

Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika mazungumzo yake na Balozi wa Kenya hapa nchini Chirau Ali Makwere amesisitiza kudumishwa na kuendelezwa kwa mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya hasa katika uimarishaji wa biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo Mbili.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito maalum kwa Watanzania kuchangamkia fursa ya kufanya biashara na nchi ya Kenya kutokana na nchi mbili kuwa na mahusiano mazuri ya kibiashara.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini Hebogand Jensen ambaye amemweleza Makamu wa Rais nia ya nchi hiyo kwa ushirikiano na nchi nyingine ya kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea wilayani Kilwa.

Balozi huyo wa Denmark nchini amesema anaimani kiwanda hicho kitakachojengwa nchini kitafanya uzalishaji mkubwa na kutoa ajira kwa mamia ya wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda imeweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini kama hatua ya kukuza uchumi wa nchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Kenya Nchi Mhe. Ali Makwere, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Brazil Nchi Mhe. Carlos Alfonso Puente, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Denmark Nchi Mhe. E. Hebogand Jensen, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mhe. Maniza Zaman, mara baada ya kumaliza mazungumzo,Ikulu jijini Dar es Salaam.

No comments: