Siku
16 za kupinga ukatili wa kijinsia ni kampeni ya kimataifa
inayoadhimishwa kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 kuelimisha
jamii kuzuia ukatili wa kijinsia. WiLDAF inashirikiana na mtandao wa
mashirika yanayopinga ukatili wa kijinsia (MKUKI), wadau wa maendeleo na
mashirika mengine kuadhimisha kampeni hizi kitaifa.
Yafuatayo
ni matukio mbalimbali ya kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili kama
yalivyofanyika sehemu mbalimbali nchini Tanzania chini ya kauli mbiu:
Funguka! Pinga ukatili wa kijinsia. Elimu salama kwa wote.
Maandamano
ya amani kupinga ukatili wa kijinsia Uzinduzi wa siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia kwa jiji la Dar es salaam ulianza kwa maandamano ya
amani ambapo maelfu walishiriki maandamano hayo kutoka Biafra hadi
Millenium towers jijini Dar es salaam. Maandamano hayo yalifanyika
tarehe 25 Novemba 2016.
Waziri
Ummy Mwalimu mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu alikua
mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho hayo yaliyofanyika tarehe 25
Novemba 2016, jijini Dar es salaam.
Akizungumza
katika uzinduzi huo Mhe. Ummy alisema serikali ya awamu ya tano
imefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha kwamba watoto wanapata elimu
salama bila aina yoyote ya ukatili wa kijinsia ikiwemo kutoa elimu bora
bila malipo. "Lengo kuu la elimu bila malipo ni kuhakikisha kuwa watoto
wetu hususan wa kike wanapata fursa ya kwenda shule kusoma na kufikia
ndoto zao katika maisha."
Aidha
alitoa wito kwa wadau na serikali kwa ujumla kutumia nafasi zao kupinga
vitendo vyote vya udhalilishaji na ukiukwaji wa haki za binadamu
vilevile kwa jamii kuwa na malezi bora na kuzingatia maadili kwa watoto
na vijana wetu.
Mama
Anne Makinda mgeni rasmi katika kongamano la kitaifa la Haki za
Wanawake. Aliyekuwa spika wa Bunge la Tanzania mama Anne Makinda alikuwa
mgeni rasmi katika kongamano la kwanza la kitaifa la Haki za wanawake
lililofanyika ukumbi wa Millenium Towers jijini Dar es salaam tarehe 28
Novemba 2016.
Kongamano
hilo lililoratibiwa na shirika lisilo la kiserikali la LSF lilikuwa na
lengo la kujadili namna mbalimbali za kuwawezesha wanawake kisheria na
kiuchumi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
Jamii
imeaswa kuhusika kikamilifu katika mapambano ya kupinga ukatili dhidi
ya wanawake na watoto na kuhakikisha watoto wanapata elimu bora na
salama. Kongamano hilo lilipambwa na kauli mbiu isemayo; Jitambue!
Jiamini, Simamia Haki yako. Wageni mbalimbali wanaharakati wa Haki za
binadamu walihudhuria kongamano hilo la aina yake wakiwemo Dr. Helen
Kijo Bisimba, Mary Rusimbi, Edda Sanga na Dr. Judith Odunga.
Mkuu
wa Wilaya ya Rungwe azindua maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mhe. Challya Julius alizindua maadhimisho ya
siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika wilaya yake na kuahidi
kusimamia katika kutokomeza ukatili wa kijinsia wilayani humo.
Uzinduzi
huo ulifanyika 29 Novemba 2016. Uzinduzi huo ulienda sambamba na kutoa
msaada wa kisheria kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia uliotolewa na
wasaidizi wa kisheria (Paralegals) wa wilaya ya Rungwe wakishirikiana na
shirika la WiLDAF Tanzania.
Wanafunzi
wa kidato cha 1, 3, 5 na 6 kutoka shule za sekondari za Benjamin Mkapa,
Jangwani, Tandika, Turiani na Temeke walihudhuria jukwaa lilioandaliwa
kwa ajili ya wanafunzi ili wapate fursa ya kutoa maoni juu ya mambo
mbalimbali yanayowakabili mashuleni. Jukwaa hilo lilifanyika 30 Novemba
2016 katika ukumbi wa Millenium Towers jijini Dar es salaam. Jukwaa
hilo liliandaliwa na shirika la WiLDAF Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo kauli mbiu ya mwaka huu
ni Funguka! Pinga Ukatili wa Kijinsia. Elimu Salama kwa wote. Siku ya UKIMWI Duniani
Januari
mosi kila mwaka hutumika kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani. Maambukizi
ya virusi vya UKIMWI kwa asilimia kubwa yanatokana na vitendo vya
ukatili dhidi ya Wanawake vinavyopelekea maambukizi ya VVU kama vile
ubakaji, mila mbalimbali ambazo zimepitwa na wakati kwa mfano: - - Ndoa
za utotoni ambapo mtoto wa kike hulazimishwa kuolewa na mtu mzima ambaye
pengine ana maambukizi ya VVU.
-
Mume kumlazimisha mke kufanya tendo la ndoa iwapo mume ameathirika bila
kutumia kinga. - Mjane kulazimishwa kufanya ngono na mzee anayetakasa
wajane. - Na wajane kulazimishwa kurithiwa na ndugu wa mume wake bila
kujali afya ya wote wawili. Jamii inapaswa kuacha na kukemea mila
zilizopitwa na wakati ili kupunguza maambukizi ya UKIMWI.
Mdahalo
wa wadau wa maendeleo kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia. Wadau wa maendeleo kutoka mashirika, serikali na taasisi
mbalimbali walikutana pamoja ili kujadiliana mambo mbalimbali
yanayohusiana na ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya
siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia. Mdahalo huo ulifanyika Desemba
1, 2016.
Hizi ni baadhi ya nukuu kutoka katika mdahalo huo;
"Ukatili
wa kijinsia huanzia nyumbani, shuleni na kwenye jamii. Jamii ipatiwe
elimu ya kutokomeza ukatili." "Wazazi wawe na ukaribu na watoto katika
malezi na kujua mienendo ya watoto wao." "Hakuna mtoto anayezaliwa akiwa
mtukutu ila inatokana na malezi ya nyumbani na muda mwingine kupeleka
hivyo vitu shuleni na hata kuwafanyia watoto wengine vitendo vya
kikatili." "Ukatili wa watoto unafanywa na ndugu wa karibu wa nyumbani
anaweza akawa mjomba, dada wa nyumbani." "Fimbo sio solution (suluhu) ya
kumrekebisha mtoto, itafutwe njia mbadala ya kumuadhibu mtoto."
Vibanda
vya Filamu Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,
shirika la TGNP Mtandao liliandaa vibanda vya filamu ili kujenga uelewa
kwa jamii na kuibua mjadala juu ya vitendo mbalimbali vya ukatili.
Wawakilishi
wa Bodaboda wapata mafunzo ya ukatili wa kijinsia, waandamana kupinga
ukatili. Wawakilishi wa madereva wa bodaboda kutoka Wilaya za Ilala,
Kinondoni na Temeke mkoa wa Dar es salaam walipata mafunzo juu ya
ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia. Madereva bodaboda wanahusika katika kubeba abiria
mbalimbali wakiwemo wanafunzi hivyo ni muhimu kuwapatia elimu hii ili
waweze kutambua madhara ya ukatili na kusaidia kuilinda jamii dhidi ya
vitendo vya ukatili.
Aidha madereva hao waliungana na shirika la WiLDAF kuandamana kama ishara ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Kauli
mbiu ya maadhimisho ni FUNGUKA! PINGA UKATILI WA KIJINSIA. ELIMU SALAMA
KWA WOTE. Kauli mbiu hii inakusudia kuhamasisha jamii na taifa kwa
ujumla kuangalia ni kwa kiasi gani changamoto zilizopo katika
miundombinu, mifumo ya kibaguzi na kukosekana kwa usawa wa kijinsia, sio
tu kunachochea ukatili wa kijinsia, bali pia kunakwamisha juhudi za
serikali, asasi za kiraia na wadau mbalimbali katika kuboresha elimu na
hivyo kusaidia watanzania kujikwamua katika wimbi la ujinga na umaskini.
#UkatiliSasaBasi
No comments:
Post a Comment